• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Wazee wacheza kamari kuliko vijana – ripoti

Wazee wacheza kamari kuliko vijana – ripoti

Na KEVIN ROTICH

WAZEE wa zaidi ya umri wa miaka 55 wanaongoza kwa kucheza kamari nchini, imebainika.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) kwa ushirikiano na Taasisi ya Takwimu nchini (KNBS) na shirika la kufuatilia masuala ya kifedha, Financial Sector Deepening Trust (FSD), imeondoa dhana ambayo imekuwepo kwa muda mrefu kwamba vijana ndio wamezama katika mchezo wa kamari.

Idadi kubwa ya wazee wa zaidi ya miaka 55 hucheza pata potea angalau mara 49 kwa wiki ikilinganishwa na vijana ambao hucheza wastani wa mara 41 ndani ya kipindi sawa.

Wazee, hata hivyo, hutumia kiasi kidogo cha fedha kucheza kamari ikilinganishwa na vijana. Kila mzee hutumia wastani wa Sh733 kwa wiki, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Hiyo inamaanisha kuwa, wazee hucheza kamari kujifurahisha ilhali vijana hushiriki michezo hiyo kusaka riziki.

Takribani asilimia 14 ya Wakenya wanajihusisha na michezo ya kamari humu nchini huku idadi kubwa wakiwa katika maeneo ya mijini.Asilimia 19 ya wanaojihusisha na michezo hiyo ni vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 25.

Chanzo cha mapato

Asilimia 15 ya vijana wanaocheza kamari wanaichukulia kama chanzo cha mapato. Asilimia 3.1 ya wazee ndio wanaochukulia mchezo huo kuwa chanzo cha mapato.

“Idadi ya wachezaji wa kamari wanaochukulia michezo hiyo kama chanzo cha mapato imepungua kutoka asilimia 22.7 mnamo 2019 hadi asilimia 11.2 mwaka huu 2021,” inasema ripoti hiyo.

Wastani wa kiasi cha fedha ambazo kila mtu alitumia katika kamari kilipungua kutoka Sh 2,559 mnamo 2019, hadi Sh939 mwaka huu 2021.

Ripoti hiyo inasema kupungua huko huenda kulichangiwa na hatua ya serikali kukabiliana na kamari haramu nchini.

Mnamo Julai 1, 2019, Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i alifutilia mbali leseni za kamari kwa madai ya kukataa kufichua mapato kwa Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA).

Miongoni mwa kampuni zilizofungwa ni Betin na Sportpesa.

Kampuni za kamari nchini hujipatia zaidi ya Sh200 bilioni kila mwaka – kunoga huko kwa biashara ya kamari kumevutia kampuni za kimataifa kama vile Betway.

Maelfu ya vijana wamekuwa wakilazimika kukopa hela ili kushiriki michezo ya kamari.

Kati ya Machi na Septemba 2021, Wakenya walitumia Sh83.2 bilioni kucheza kamari kupitia Mpesa pekee ikilinganishwa na Sh49.2 bilioni mwaka 2020.

Hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 69.Kupungua kwa fedha zilizotumika katika kamari mwaka jana, huenda kulitokana na kusimamishwa kwa mechi kote duniani kutokana na janga la corona.

Kampuni za huduma za simu ya Safaricom, KRA na kampuni za kamari ndizo zinanufaika pakubwa kutokana na ongezeko la idadi ya Wakenya waliojitosa katika michezo ya kamari.

Mapato ya Safaricom kutokana na michezo ya kamari yameongezeka maradufu kutoka Sh1.48 bilioni miaka miwili iliyopita hadi Sh2.95 bilioni mwaka huu 2021.

KRA imekuwa ikivuna takribani Sh6.2 bilioni kutoka kwa mapato ya kamari kupitia MPesa.

You can share this post!

Mahakama yamwachilia diwani aliyefungwa jela

Huenda Uhuru atafuata nyayo za Nyerere

T L