• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
Waziri Nakhumicha ahimiza wazazi kuhakikisha watoto wanapewa chanjo ya polio

Waziri Nakhumicha ahimiza wazazi kuhakikisha watoto wanapewa chanjo ya polio

NA LAWRENCE ONGARO

KAMPENI ya chanjo imeanza katika kaunti nne nchini, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha akizindua rasmi zoezi hilo katika Hospitali ya Ruiru Level 4, Kaunti ya Kiambu.

Kaunti nyingine zinazolengwa ni Nairobi, Garissa na Kajiado.

Uzinduzi wa pili na wa tatu wa chanjo hiyo utaendelea Septemba na Oktoba katika kaunti sita ambazo ni Lamu, Tana River, Wajir, Mandera, Kitui, na Machakos.

Alisema serikali inalenga watoto chini ya miaka mitano wapatao 5.6 milioni.

“Wahudumu maalum watasambazwa mashinani kuona ya kwamba wanafikia watoto wote wanaohitaji chanjo,” akasema waziri Nakhumicha.

Alisema zoezi hilo la chanjo limepitishwa rasmi na Shirika la Afya Duniani (WHO), bodi ya kuidhinisha ubora wa dawa na maabara ya kitaifa yanayodhibiti maswala ya afya.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na kaimu mkurugenzi wa afya Dkt Patrick Amoth, balozi wa America nchini Kenya Bi Meg Whitman na washika dau wengine wa idara ya afya.

Waziri aliwahimiza wazazi wawe mstari wa mbele kuona ya kwamba wamepeleka watoto wao chini ya umri wa miaka mitano kupata chanjo.

Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi alisema kaunti hiyo ina vituo vya afya 114 vyenye vifaa muhimu vya afya.

“Wahudumu wa afya wa mashinani hutembelea wakazi majumbani mwao wakitoa chanjo kwa watoto,” alisema gavana huyo.

Alisema kaunti ya Kiambu itaendelea kupambana na polio ili kuangamiza ugonjwa huo.

Dkt Amoth alisema serikali itahakikisha inapambana na polio nchini kote.

Alisema utafiti umeonyesha ya kwamba watoto wengi mashambani hawajapata chanjo na serikali iko makini kutekeleza zoezi hilo.

  • Tags

You can share this post!

Jeshi langu linawindwa, adai Raila kuhusu kukamatwa kwa...

Sumu hatari zimeachiliwa ndani ya Mto Athi, bunge laelezwa

T L