• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 7:50 AM
Jeshi langu linawindwa, adai Raila kuhusu kukamatwa kwa Oparanya

Jeshi langu linawindwa, adai Raila kuhusu kukamatwa kwa Oparanya

KARIM RAJAN na WINNIE ATIENO

KINARA wa Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, amedai kuwa serikali imepanga njama ya kuwinda viongozi wa upinzani walioondoka mamlakani ili kuwatishia.

Hii ni baada ya kukamatwa kwa aliyekuwa Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya na wake zake wawili mnamo Jumatano.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Odinga alidai anafahamu serikali imepanga kuwakamata wanasiasa wengine wa upinzani walioondoka mamlakani hasa magavana, maseneta na wabunge, kwa madai ya ufisadi.

Alieleza kuwa, aliyekuwa gavana wa Laikipia, Bw Ndiritu Muriithi, na mwenzake wa Murang’a, Bw Mwangi wa Iria (Murang’a), ni kati ya viongozi ambao wanalengwa kukamatwa na serikali.

“Wanalenga viongozi ambao wanaunga mkono muungano wa Azimio ambao walikuwa mamlakani kwenye serikali iliyopita wakiwemo wabunge, maseneta, magavana na viongozi wengine wa ngazi ya juu. Wanawindwa kisiasa,” akasema Bw Odinga.

Alipoulizwa kuhusu madai yaliyoenea hivi majuzi kwamba serikali inapanga pia kumtia mbaroni aliyekuwa Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, Bw Odinga hakuthibitisha bali alisema hangependa kutegemea uvumi.

Bw Joho ni mmoja wa wanasiasa wa upinzani ambao hawajaonekana hadharani kwa muda mrefu tangu Rais William Ruto alipoingia mamlakani baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita.

Wengine ni Bi Charity Ngilu (Kitui), Cornel Rasanga (Siaya), Granton Samboja (Taita Taveta), miongoni mwa wengine.

“Sitaki kuamini uvumi, pengine watamwinda. Lakini nilikuwa nataka kusema kuwa EACC imevuka mipaka kumkamata Bw Oparanya. Kama kuna makosa aliyoyafanya akiwa mamlakani itawekwa wazi na Mkaguzi wa Fedha. Akaunti za fedha za kaunti hutathminiwa na Mkaguzi wa Fedha mara kwa mara na ripoti kuchapishwa wazi,” alisema Bw Odinga.

Hivi majuzi, Naibu Rais, Bw Rigathi Gachagua, alidai kuna magavana walitumia pesa za umma kufadhili kampeni za upinzani.

Bw Odinga alikuwa Dubai akisafiri kuelekea Nairobi, kutoka Uingereza ambako alikuwa ameenda ziara ya wiki moja. Afisi yake ilidai kuwa, ziara hiyo ilikuwa ni ya mapumziko na mikutano ya kibiashara.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), ilimhoji Bw Oparanya na wake zake wawili katika makao makuu jijini Naiorbi kuhusiana na tuhuma za ufisadi na uhalifu wa kiuchumi, anazodaiwa kutekeleza alipokuwa mamlakani kwa kipindi cha miaka 10.

Maafisa wa EACC walisema kuwa wanachunguza jinsi Bw Oparanya aliyehudumu wadhifa wa gavana wa Kakamega kati ya mwaka 2013 hadi 2022, alivyotumia Sh1.3 bilioni.

Hata hivyo, Bw Odinga alisema hatua hizo zinazoendelezwa dhidi ya viongozi wa upinzani hazitaathiri mazungumzo ya mapatanisho kati ya upinzani na serikali.

Alipuuzilia mbali viongozi wa Kenya Kwanza ambao wanadai mazungumzo hayo hayana maana.

Jumanne, Bw Gachagua alidai kuwa, Rais Ruto na Bw Odinga walikutana Mombasa hivi majuzi na Bw Odinga akaweka matakwa yake wazi.

Bw Odinga aliwataka Wakenya kupuuza matamshi hayo aliyoyataja kuwa mbegu ya chuki.

“Anazururazurura akieneza urongo na propaganda za kila aina. Anajaribu kupanda mbegu ya chuki na sumu. Anapigana na kivuli chake maanake amebanwa hana mbele wala nyuma. Hataki mazungumzo ya mapatano ndio maana anaeneza urongo,” alisema Bw Odinga.

Mazungumzo hayo ya mapatanisho yanatarajiwa kurejelewa leo.

  • Tags

You can share this post!

Wanaume wawili wauguza majeraha baada ya kushambuliwa na...

Waziri Nakhumicha ahimiza wazazi kuhakikisha watoto...

T L