• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Aliyekuwa kiongozi wa al Shabaab ateuliwa waziri

Aliyekuwa kiongozi wa al Shabaab ateuliwa waziri

NA AFP

MOGADISHU, Somalia

SOMALIA imemteua aliyekuwa naibu kiongozi na msemaji wa kundi la kigaidi la Al Shabaab, Muktar Robow kuwa Waziri wa Dini, Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre alisema Jumanne.

Tangazo hilo limefungua ukurasa mpya katika maisha ya Robow ambaye aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani kwa miaka minne baada ya kukosana na rais wa zamani Mohamed Abdullahi Mohamed, almaarufu Farmajo.

Robow, 53 aligura kundi hilo la kigaidi, lenye uhusiano na Al-Qaeda, mnamo Agosti 2017.

Wakati mmoja Serikali ya Amerika ilitoa zawadi ya dola 5 milioni (Sh600 milioni) kwa yeyote ambaye angetoa habari za kusaidia kukamatwa kwake.

“Baada ya kufanya mashauriano kwa siku 30 ni furaha yangu kuwasilisha wanaume na wanawake wa Somalia ambao nimewateua kwa kuzingatia vigezo vya masomo, tajriba na usawa,” Barre akasema.

“Nataraji kwamba watashughulikia mahitaji ya taifa hili,” waziri mkuu huyo akaongeza.

Robow alikamatwa mwishoni mwa mwaka wa 2018, siku chache baada ya kuwasilisha stakabadhi zake ili aruhusiwe kuwania ubunge katika eneo la kusini mwa Somalia.

Serikali ya Farmajo ilimsuta kwa kupanga mashambulio katika mji wa Baidoa ili kusababisha misukosuko katika eneo hilo.

Kukamatwa kwake kulichochea maandamano makubwa huku baadhi ya washiriki wakiteketeza sanamu za Farmajo.

Walimkashifu rais huyo kwa kuingilia masuala ya ndani ya eneo hilo.

Uteuzi wa Robow unajiri wiki chache baada ya Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kudokeza kuwa huenda serikali yake ikafanya mashauriano na Al Shabaab “wakati ufaao”.

Kundi la Al Shabaab limepambana na serikali kuu ya Somalia kwa miaka 15 iliyopita na linasalia kuwa tishio kwa usalama nchini humo. Hii ni licha ya operesheni inayoendeshwa na vikosi vya wanajeshi chini ya Umoja wa Afrika (AU).

Wapiganaji wa Al Shabaab walifurushwa kutoka jiji kuu la Somalia, Mogadishu mnamo 2011.

Hata hivyo, tangu wakati huo wameendelea kushambulia vituo vya wanajeshi, serikali na hata makazi ya raia wa kawaida.

Awali, Barre alitarajiwa kutaja majina ya wanachama wa baraza lake la mawaziri ndani ya siku 30 baada ya kuteuliwa kwake mnamo Juni 25 lakini akaomba bunge limpe muda zaidi aweze kufanya mashauriano.

Wengine walioteuliwa Jumanne ni pamoja na naibu waziri mkuu, mawaziri 25, mawaziri 24 wa majimbo na manaibu mawaziri.

Bunge linatarajiwa kupiga kura kuidhinisha baraza hilo la mawaziri lenye wanachama 75.Serikali mpya inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo kiangazi, baa la njaa na mashambulio ya wanamgambo wa Kiislamu.

Kiangazi kinachoshudiwa katika eneo la Upembe wa Afrika kimeathiri jumla ya raia 7.1 milioni.

Wengine 200,000 wanakabiliwa na uhaba wa chakula, kulingana na takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa (UN).

Mnamo Julai, Rais Mohamud alisema mbinu mbadala zinafaa kutumika kutokomeza Al Shabaab kando na mbinu za kijeshi.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Rais aseme ilipofikia hatua ya...

Kenya ya kwanza Afrika kuuza avokado China

T L