• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Amerika kupunguza mapato ya mafuta yanayotoka Urusi

Amerika kupunguza mapato ya mafuta yanayotoka Urusi

Na AFP

BALI, INDONESIA

VITA vinavyoendeshwa na Urusi nchini Ukraine ni tishio kubwa kwa uchumi wa ulimwengu, Waziri wa Fedha wa Amerika Janet Yellen, alisema Alhamisi huku mawaziri wa fedha kutoka Mataifa 20 yenye uwezo mkubwa (G20) wakitarajiwa kujadili suala hilo Indonesia leo Ijumaa.

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umechangia ongezeko la mfumko wa bei wakati ambapo nchi za ulimwengu zinajikaza kukarabati chumi zao zilizoathiriwa na janga la Covid-19 na mabadiliko ya tabia nchi.

Kuna hofu kwamba vita nchini Ukraine vitachangia ongezeko zaidi la njaa na umasikini katika mataifa ya ulimwengu.

“Changamoto kubwa inayotukabili leo inatokana na vita haramu vinavyoendeshwa na Urusi dhidi ya Ukraine,” Bi Yallen alisema katika kisiwa cha Bali kabla ya kuanza kwa mkutano na mawaziri wa fedha wa mataifa tajiri ulimwenguni.

Mkutano huo, unaofanyika leo Ijumaa na kesho Jumamosi pia utahudhuriwa na magavana wa benki kuu kutoka mataifa hayo.

“Tunashuhudia madhara ya vita hivyo katika kila mahali ulimwenguni. Athari hizo, hususan, zinashuhudiwa kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta na uhaba mkubwa wa chakula,” Yallen akaongeza.

“Jamii ya kimataifa sharti ihakikishe kuwa Rais Vladimir Putin anawajibikia madhara ya kiuchumi na kibinadamu yaliyotokana na vita vyake.”

Waziri Yellen alisema ataendelea kushinikisha washirika wa Amerika katika G20 katika mkutano huo kudhibiti bei ya mafuta kutoka Urusi.

Hatua hii, akasema, itapunguza mapato ya Urusi na kuiwekea presha kusitisha vita nchini Ukraine huku ikishusha bei ya mafuta.

“Udhibiti wa bei….. ni mojawapo ya hatua za kushughulikia machungu ambayo Waamerika na familia kote ulimwenguni yanapitia katika vituo vya mafuta na vyakula,” akasema.

“Kudhibitiwa kwa bei ya mafuta ya Urusi kutamnyima Putin fedha ambazo wanajeshi wake wanahitaji,” Yellen akaeleza.

Waziri huyo alielezea matumaini kuwa India na China zitaungana na Amerika kuchukua hatua hiyo, akisema “itaendeleza haja yao” ya kutaka bei ya mafuta ishuke duniani.

Hata hivyo, Yellen alikataa kusema iwapo maafisa kutoka mataifa ya Magharibi wataondoka mkutanoni maafisa wa Urusi watakapoongea; walivyofanya katika mkutano wa G20 jijini Washington Aprili.

“Mambo hayatakuwa sasa. Nitalaani vikali uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na madhara yake kwa uchumi wa ulimwengu. Nataraji wenzangu pia watafanya hivyo,” akaonya.

Waziri wa Fedha wa Urusi Anton Siluanov atahudhuria mazungumzo hayo kupitia mtandao.

Wiki iliyopita Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov alielekezewa lawama na wenzake kutoka G20 walipolaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Ukraine huuza ngano, mahindi na mafuta ya kupikia, kwa wingi, katika mataifa ya nje. Lakini usafirishaji wa bidhaa hizo ulivurugwa kuanzia Februari 24, kufuatia uvamizi wa Urusi nchini humo.

  • Tags

You can share this post!

Fedha: Wakuu wa shule sasa waingia baridi

Masonko Saudia wamezea Ronaldo

T L