• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Amerika yataka Afrika ikatae ‘kutumiwa vibaya’

Amerika yataka Afrika ikatae ‘kutumiwa vibaya’

NA AFP

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

WAZIRI wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika, Antony Blinken, amezitaka nchi za Afrika kukataa masharti yanayotolewa na mataifa ya kigeni.

Blinken alisema kuwa nchi yake haitaingilia masuala ya demokrasia katika nchi za Kenya na Nigeria.

Kulingana na Blinken, mataifa ya Magharibi yamekuwa yakiingilia masuala ya nchi za Afrika, hali ambayo imezifanya kushindwa kuendesha mambo yao wenyewe.

Blinken yuko ziarani Barani Afrika ambapo atazuru nchi tatu katika juhudi za kuimarisha uhusiano ambao unaonekana kufifia kutokana na kuongezeka kwa ushawishi wa China na Urusi.

Akizungumza nchini Afrika Kusini, Blinken alisema kuwa Amerika itaendelea kuunga mkono juhudi za Afrika kudumisha demokrasia na uwekezaji katika kawi na uchumi.

Waziri huyo pia alionya kundi la mamluki kutoka Urusi, Wagner, ambalo linaaminika kuendesha shughuli zake katika nchi za Libya, Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Alisema kuwa kundi hilo la mamluki linajificha katika nchi zilizokabiliwa na mapigano.Serikali ya Urusi imejitenga na kundi hilo linaloaminika kufadhiliwa na mabwanyenye wa nchini Urusi.

Uhusiano baina ya Afrika Kusini na Amerika umedidimia baada ya nchi hiyo ya Afrika kukataa kulaani Urusi kutokana na hatua yake kuvamia Ukraine tangu Februari, mwaka huu.Blinken ni afisa wa ngazi ya juu wa nchi za kigeni katika kujaribu kuvutia nchi za Afrika upande wake.

Mwezi Julai, waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, alizuru Afrika na kulaumu Amerika na nchi za Ulaya kwa kusababisha njaa Barani Afrika.

Kulingana na Lavrov, vikwazo vilivyowekwa na Amerika na nchi za Ulaya dhidi ya nchi yake vimesababisha Urusi kushindwa kufikisha nafaka Afrika.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, pia alizuru mataifa ya Cameroon, Benin na Guinea-Bissau mnamo Juni katika juhudi za kuimarisha uhusiano kati ya nchi yake na mataifa ya Afrika.

Blinken jana Jumanne alikutana na kiongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi ambapo walijadili mvutano kati ya nchi yake na Rwanda.

DRC imekuwa ikishutumu Rwanda kuunga mkono waasi wa kundi la M23.

Rwanda imekanusha kushirikiana na kundi hilo la M23.

Viongozi hao wawili walijadili ripoti ya hivi karibuni ya wataalam wa Umoja wa Mataifa iliyobaini kuwa wanajeshi wa Rwanda walijificha katika kundi la M23 kushambulia DRC.Waziri huyo wa Amerika pia anatarajiwa kuzuru Rwanda ambapo atakuwa hadi Agosti 12.

Wanaharakati wamekuwa wakishinikiza Blinken kushutumu nchi ya Rwanda kwa kile wanachodai ni ongezeko la visa vya ugandamizaji wa viongozi wa upinzani.

  • Tags

You can share this post!

Joho na Sonko walimana ngumi kituo cha kura

Usalama waimarishwa Mavoko kura zikihesabiwa

T L