• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Ghasia zazuka Somaliland upinzani ukisisitiza kura ifanyike

Ghasia zazuka Somaliland upinzani ukisisitiza kura ifanyike

NA AFP

HARGEISA, Somaliland

WATU kadhaa waliuawa na wengine wengi wakajeruhiwa Alhamisi jioni polisi walipowashambulia waandamanaji kwa risasi katika miji kadha katika eneo lililojitenga kutoka Somalia, Somaliland, wafuasi wa upinzani na mashahidi walisema.

Mamia ya watu walifurika katika barabara za jiji kuu Hargeisa na miji ya Buwrao and Erigavo baada ya kutibuka kwa mazungumzo kati ya serikali na upinzani, kuhusu suala la uchaguzi wa urais.

Upinzani unalaumu serikali kwa kuendesha njama ya kuchelewesha uchaguzi wa urais ambao umepangiwa kufanyika mnamo Novemba 2022.

Waandamanaji walibeba mabango yenye maandishi “Uchaguzi sharti ufanywe Novemba 13, 2022” huku wakiimba nyimbo za kuikashifu serikali.

“Amani inaweza tu kudumu Somaliland kupitia kufanyika kwa uchaguzi huru na wenye haki. Hii ndio sauti ya wale ambao wanaunga mkono demokrasia,” Abdirahman Mohamed Abdullahi, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Waddani Party, aliambia umati jijini Hargeisa.

Mmoja wa waandalizi wa maandamano, Ahmed Ismail, aliambia AFP kwamba watu watatu waliuawa akiwemo mwanamke mmoja jiji Hargeisa na wengine 34 wakalazwa hospitalini.

“Watu kadha akiwemo mlinzi mmoja wa kiongozi wa chama chetu waliuawa. Bado tunaendelea na uchunguzi na huenda idadi ya wafu ikawa juu,” mwanachama mmoja wa chama cha Waddani akaambia AFP huku akiomba jina lake libanwe.

Mtu mmoja alifariki katika mji Erigavo wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na polisi, shahidi Abdullahi Mohamud, akasema, “Polisi walijaribu kuzuia waandamanaji kufika katika makutano ya barabara mjini Erigavo.”

Hata hivyo, waandamanaji waliwalemea maafisa wa polisi waliokuwa wameweka vizuizi barabarani.

“Hatutazuia maandamano haya… hadi rais Muse Buhi Abdi atakapotangaza kuwa yuko tayari kwa uchaguzi,” akasema Heybe Adan, mmoja wa waandamanaji.

Kwenye kikao na wanahabari mnamo Alhamisi jioni, kiongozi wa chama cha Waddani Abdullahi alishutumu serikali kwa kutenda “unyama” dhidi ya waandamanaji.

“Hii ilikuwa ni maandamano ya amani na tumewaongoza watu ambao walibeba mabango na firimbi pekee. Lakini serikali ilitekeleza maovu kwa kutumia nguvu kupita kiasi, risasi na vitoa machozi,” akasema.

Vurugu zimeleta wasiwasi miongoni mwa mataifa ya kigeni haswa Amerika, Umoja wa Ulaya (EU), Uingereza, Denmark na mataifa mengine.

Kwenye taarifa ya pamoja, mataifa hayo yalielezea hofu kuhusu ripoti kuhusu kuvunjika kwa utulivu na matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano ya Alhamisi.

“Tunatoa wito kwa pande zote kuhakikisha kuwa maandamano yanafanywa kwa amani. Nao polisi wanakome kutumia nguvu kupitia kiasi na wanazingatia sheria,” mataifa hayo yakasema kwa taarifa ya pamoja.

Uchaguzi wa urais katika eneo la Somaliland umepangiwa kufanyika mnamo Novemba 13 lakini upinzani umeelezea wasiwasi kwamba serikali inajivuta katika maandalizi ya shughuli hizo.

  • Tags

You can share this post!

KUMBUKUMBU ZA SPOTI: Jagina Obore aunga mkono kuundwa timu...

TUSIJE TUKASAHAU: Uvutaji wa sigara maeneo ya umma...

T L