• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
ICC yampata aliyekuwa kiongozi wa LRM na hatia

ICC yampata aliyekuwa kiongozi wa LRM na hatia

Na MASHIRIKA

MAHAKAMA ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) imempata aliyekuwa kiongozi wa kundi la waasi la Lord Resistance Movement (LRM) Dominic Ongwen na hatia kwa makosa 61 ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita aliyotekeleza Kaskazini mwa Uganda kati ya Julai 1, 2002 na Desemba 31, 2005.

Mahakama hiyo ilitangaza Alhamisi kwamba majaji Bertram Schmitt, Peter Kovacs na Raul Cano Pangalangan walichambua ushahidi uliowasilishwa na kubaini kuwa Ogwen ana hatia ya kutenda aina nyingi za uhalifu.

Katika uamuzi wao uliosomwa na Jaji Kovacs, Ongwen alipatikana na hatia ya kutekeleza mauaji watu, kuwadhuluma, kuharibu mali katika kambi nne za wakimbizi wa ndani kwa ndani.

Kulingana na majaji hao Ongwen pia alipatikana na makosa ya ubakaji na dhuluma nyinginezo nyingi za kingono.

Zaidi ya hayo, kiongozi huyo wa LRM pia alipatikana na makosa ya kuwasajili watoto wenye umri chini ya miaka 15 katika jeshi na kuwatumia kutekeleza mapigano.

Majaji hao walisema kuwa makosa hayo yalifanywa wakati wa vita vya uasi vilivyoendeshwa na LRM dhidi ya wanajeshi wa serikali ya Uganda katika eneo la Kaskazini mwa Uganda.

“Wapiganaji wa LRM akiwemo Dominic Ongwen, walichukulia raia wa kaskazini mwa Uganda kama washirika wa Serikali ya Uganda. Hawa haswa ni wale waliokuwa wakiishi katika kambi za wakimbizi wa ndani kwa ndani zilizobuniwa na serikali,” ICC ikasema.

Majaji wa mahakama hiyo pia walithibitisha kuwa Ongwen alitenda makosa hayo akiwa na akili timamu na bila shinikizo zozote.

Hata hivyo, mshukiwa huyo ana muda siku 30 kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, la sivyo ahukumiwe kifungo cha miaka 30 gerezani. Pia anaweza kupewa hukumu ya kifungo cha maisha au atozwe faini.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Wahubiri waelezea hofu yao kuhusu taharuki ya kisiasa

Wabunge waachwa vinywa wazi kuambiwa Sh6.2 bilioni za...