• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Idadi ya wahanga wa ajali ya ndege ya TZ iliyoanguka Ziwa Victoria yafika 19

Idadi ya wahanga wa ajali ya ndege ya TZ iliyoanguka Ziwa Victoria yafika 19

BUKOBA, TANZANIA

NDEGE iliyokuwa imewabeba abiria 43 kutoka Tanzania ilianguka katika Ziwa Victoria mapema Jumapili kutokana na hali mbaya ya hewa, wamesema polisi nchini humo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefika eneo la tukio ambapo ametangaza kwamba jumla ya watu 19 wamepoteza maisha. Awali Daktari Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Issessanda Kaniki alikuwa amethibitisha kutokea kwa vifo vya watu watatu.

Polisi walisema ndege hiyo ilihusika katika ajali hiyo ilipokuwa ikikaribia kuwasili mjini Bukoba.

“Kuna ajali ambayo imetokea inayohusisha ndege inayomilikiwa na shirika la Precision Air. Ilianguka umbali wa mita 100 kutoka uwanja wa ndege wa Bukoba,” akasema Kamanda Mkuu wa Polisi katika eneo hilo, William Mwampaghale, kwenye kikao na wanahabari katika uwanja huo.

Kamishna wa eneo hilo, Albert Chalamila, alisema kuwa ndege hiyo ilikuwa imewabeba watu 43, wakiwemo abiria 39, marubani wawili na wahudumu wawili.

Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka jijini Dar es Salaam hadi katika mji wa Kagera.

“Tunapozungumza, tumefanikiwa kuwaokoa watu 26, ambao tayari washakimbizwa katika hospitali ya yetu ya rufaa,” akasema Chalamila.

“Harakati za uokozi zinaendelea japo tunawasiliana na marubani,” akaeleza, akiongeza kuwa wataendelea kutoa maelezo zaidi.

Shirika hilo la ndege ndilo kubwa la kibinafsi nchini humo.

“Tumetuma vikosi vya uokoaji. Tutaendelea kutoa maelezo kadri shughuli zinavyoendelea,” likasema shirika hilo kwenye taarifa.

Video iliyosambazwa mitandaoni ilionyesha ndege hiyo ikiwa imezama nusu majini, huku waokoaji wakijaribu kuwanusuru abiria.

Waokoaji hao walijaribu kuiinua ndege hiyo kwa kutumia kamba na kreni.

Rais Samia Suluhu alieleza kusikitishwa na kisa hicho, huku akitoa jumbe za heri kwa waathiriwa wa ajali hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Arsenal wazamisha Chelsea ugani Stamford Bridge na kurejea...

Amerika yarai Ukraine izungumze na Urusi

T L