• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Amerika yarai Ukraine izungumze na Urusi

Amerika yarai Ukraine izungumze na Urusi

NA MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., AMERIKA

AMERIKA imeanza juhudi za kuirai Ukraine kushusha msimamo wake mkali na kuzungumza na Urusi, ili kumaliza mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea baina ya mataifa hayo tangu Februari 24.

Kulingana na gazeti la Washinton Post, Amerika jana Jumapili, Wizara ya Kigeni nchini humo ilisema Urusi inaendelea kuimarisha mashambulio yake dhidi ya Ukraine, na haionyeshi dalili za kujitolea kushiriki mazungumzo ya kupata amani.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, ombi la Amerika halilengi kuishinikiza Ukraine kukubali matakwa ya Urusi, bali kama mkakati wa kuhakikisha taifa hilo linaendelea kuungwa mkono kutoka mataifa mengine.

Maafisa wa Amerika na Ukraine walikubali kuwa hatua ya Rais Volodymyr Zelensky kupiga marufuku mazungumzo baina yake na Rais Vladimir Putin imezua hofu katika baadhi ya sehemu barani Ulaya, Afrika na Amerika Kusini, ambako bei za vyakula zimepanda sana.

“Ni wazi Ukraine inaonekana kuchoshwa na vita hivi. Ni hali inayozua wasiwasi mwingi miongoni mwa washirika wetu,” likasema shirika hilo, likimnukuu afisa mmoja wa ngazi ya juu wa serikali ya Rais Joe Biden.

Mnamo Oktoba 4, Rais Zelensky alitoa agizo akitangaza kuondoa uwezekano wowote wa Ukraine kufanya mazungumzo na Putin, lakini akaacha mwanya kwa taifa hilo kufanya mazungumzo ya wazi na Urusi.

Baraza la Usalama la Ikulu ya White House, Amerika halikutoa taarifa yoyote kuhusu uamuzi huo.

Akaongeza msemaji wa Wizara hiyo: “Tulisema hapo awali na tutasema tena: Vitendo huwa na maana kubwa kuliko matamshi yake. Ikiwa Urusi iko tayari kwa mazungumzo, inafaa kukoma kuendeleza mashambulio yake. Inafaa kuondoa vikosi vyake nchini Ukraine. Inaendelea kuongeza mashambulio yake. Imedhihirisha haiko tayari kushiriki katika mazungumzo yoyote.”

Kuhusu kauli ya Rais Zelensky, akasema, “Tuko tayari kwa amani. Hata hivyo, lazima kuwe na haki katika pande zote mbili.”

Kwenye hotuba yake Ijumaa kwa raia wa Ukraine, alisema Zelensky: “Dunia inajua msimamo wetu. Tunaheshimu Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani na hekima kwa watu wetu.”

Mshauri wa Amerika kuhusu Usalama wa Kitaifa, Jake Sullivan, alisema kuwa Amerika itaendelea kuiunga mkono baada ya chaguzi za katikati ya muhula wa utawala wa Amerika kuanzia hapo kesho Jumanne.

Amerika ilitangaza kutoa msaada wa Sh40 bilioni kwa vikosi vya Ukraine, ikiwemo ukarabati wa vifaru aina ya T-72 kutoka Jamhuri ya Czech na makombora ya kudungua ndege na droni zinazotumiwa na Urusi kuendeleza mashambulio yake.

Kufikia sasa, Amerika itakuwa imetoa msaada wa Sh182 bilioni kwa majeshi ya Ukraine.

Kwa mara ya kwanza, Putin alionyesha dalili za kushusha msimamo wake kuhusu vita hivyo Ijumaa, baada ya kuunga mkono mpango wa kuwahamisha raia katika baadhi ya sehemu za eneo la Kherson, kusini mwa Ukraine.

  • Tags

You can share this post!

Idadi ya wahanga wa ajali ya ndege ya TZ iliyoanguka Ziwa...

PAUKWA: Bobu amtoa kijasho Harara baraza la wazee

T L