• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Kenya kujua ikiwa itapeleka polisi Haiti

Kenya kujua ikiwa itapeleka polisi Haiti

NEW YORK, AMERIKA

NA MASHIRIKA

BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) linatarajiwa kupiga kura kufanya uamuzi kuhusu ikiwa litaruhusu kikosi cha polisi cha kimataifa kitakachoongozwa na Kenya kupelekwa nchini Haiti kukabiliana na magenge ya uhalifu au la.

Baraza hilo lenye wanachama 15 linatarajiwa kubuni mkakati na kuagiza kutumwa kwa kikosi hicho kwa muda wa mwaka mmoja. Ufaafu wa kikosi hicho nchini Haiti utatathminiwa baada ya miezi tisa.

Ikiwa uamuzi huo utapitishwa na UN, basi Kenya itatuma polisi 1,000 nchini humo kufikia Januari mwaka ujao. Mataifa mengine ambayo yamesema yatatuma vikosi kama hivyo ni Bahamas, Jamaica na Antigua and Barbuda.

Kikosi hicho kinatarajiwa kuwasaidia polisi wa Haiti kujenga upya miundomsingi muhimu ambayo imeharibiwa na magenge hayo.
Amerika imeahidi kutoa Sh14.5 bilioni kufadhili kikosi hicho.

Haiti imekuwa ikikumbwa na uhalifu kwa miongo mingi lakini, wimbi la sasa la uhalifu liliongezeka baada ya mauaji ya aliyekuwa rais wa taifa hilo, Jovenel Moise mnamo Julai 2021.

Magenge hayo yamechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya nchi hiyo, yakitekeleza mashambulio makali kwa raia na kuuwa mamia ya watu.

Kupitia Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Dkt Alfred Mutua, serikali ya Kenya ilisema ilifikia uamuzi huo baada ya kufanya mashauriano ya kina na Haiti.

“Kenya imeamua kupeleka kikosi cha polisi wake nchini Haiti baada ya ombi lililotolewa kwake na Haiti na mataifa kadhaa ambayo ni marafiki wa taifa hilo,” akasema Dkt Mutua.

Dkt Mutua alisema kuwa lengo kuu la kikosi hicho litakuwa “kuwasaidia polisi wa Haiti kurejesha hali ya kawaida na kulinda miundomsingi muhimu dhidi ya kuharibiwa”.

Waziri alisema hatua hiyo ni sehemu ya uamuzi wa Kenya kuwasaidia watu wote wenye asili ya Kiafrika kote duniani.

Alisema pia hatua hiyo ni sehemu ya sera mpya ya Umoja wa Afrika (AU) kuendeleza umoja wa Kiafrika baina ya Waafrika wote kote duniani.

Hata hivyo, Dkt Mutua alisema kuwa Kenya itakituma kikosi hicho tu, baada ya kupata kibali kutoka kwa UN na taratibu zifaazo za kikatiba.

Hata hivyo, hatua hiyo imekosolewa vikali na baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu na wasomi wa sheria, wakisema kuwa serikali haijafuata taratibu zifaazo za kisheria na kikatiba.

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa na Jaji Mkuu Mstaafu Willy Mutunga wametaja uamuzi huo kuwa “hatari”.

Dkt Mutunga alisema kuwa kando na hatua hiyo kuwa ukiukaji wa Katiba, inaendeleza mtindo ambapo maafisa wa ngazi za juu serikalini wamekuwa wakivunja Katiba bila kujali.

“Hili linaeleza sababu ambapo mikataba ya kibiashara baina ya Kenya na Haiti imekuwa ikifanywa gizani,” akasema Dkt Mutunga, kwenye makala aliyoandika kwenye gazeti moja.

  • Tags

You can share this post!

Siko vizuri kabisa, Akothee alilia mashabiki wamuombee

Jalang’o auguza mguu baada ya kufanyiwa upasuaji

T L