• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Kenya kunufaika na ufadhili wa Sh42b wa CIF wa kupiga jeki uhifadhi wa mazingira

Kenya kunufaika na ufadhili wa Sh42b wa CIF wa kupiga jeki uhifadhi wa mazingira

NA PAULINE ONGAJI akiwa SHARM EL-SHEIKH, MISRI

KENYA imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zitakazonufaika na ufadhili wa zaidi ya Sh42 bilioni kutokana na hazina mpya ya uhifadhi wa mazingira, iliyozinduliwa na mashirika ya Nature People na Climate Investment Program (NPC), iliyozinduliwa hivi majuzi na hazina Climate Investment Fund (CIF).

Habari hii ilitangazwa na afisa mkuu mtendaji wa CIF Mafalda Duarte, katika kongamano la mabadiliko ya tabianchi la Umoja wa Mataifa 2022, al-maarufu Kongamano la wanachama wa UNFCCC, au COP27 linaloendelea katika jiji la Sharm el-Sheikh nchini Misri.

Kenya ni miongoni mwa nchi nyingine zikiwemo Zambia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Tanzania, Misri, Fiji na Dominican Republic, ambazo kupitia ufadhili huu zinatarajiwa kupokea pesa hizi zilizochangwa na nchi za Italia, Uingereza na Uswidi.

Mpango huu utaangazia kuimarisha na kuhifadhi mazingira asili katika masuala ya kilimo na mfumo endelevu wa vyakula, kuhifadhi misitu na mifumo ya pwani na kusaidia jamii za kiasili.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mafalda Duarte, Afisa mkuu mtendaji wa CIF alisema kwamba ufadhili huu utahusisha kusaidia nchi zilizochaguliwa baada ya mataifa haya kuwasilisha mipango yao ya ufadhili katika kukabiliana na baadhi ya changamoto kuu za kimazingira zinazozikumba.

Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, nchi 55 zilituma maombi ili kuhusishwa kwenye mpango huu.

Bodi ya usimamizi ilifikia uamuzi wa mwisho uliotangazwa katika kongamano hili kufuatia shughuli kali za mchujo zilizofanywa na wataalam huru.

Hatua ifuatayo ni kwa nchi zilizochaguliwa kuandaa mipango ya uwekezaji kwa ushirikiano na benki za kimataifa za maendeleo.

Kulingana na Chris Armitage, Afisa mkuu mtendaji wa Global EverGreening Alliance, kwa sasa Kenya inatarajiwa kupokea zaidi ya Sh3.6 bilioni kutokana na mpango huu.

“Mwaka uliopita katika kongamano la kimataifa la mabadiliko ya tabianchi COP26, jijini Glasgow, Scotland, tulitangaza uwekezaji wa zaidi ya Sh18 bilioni kuhusisha nchi sita katika eneo la Afrika Mashariki na Kusini, miongoni mwao Kenya, Ethiopia, Uganda, Tanzania, Malawi and Zambia. Mpango huo ulianza kutekelezwa takriban miezi mijnne iliyopita.

“Jana tulikuwa tumetangaza kutolewa kwa zaidi ya Sh40 bilioni za ziada ambapo takriban Sh22 bilioni za kwanza zitaelekezwa kusimamia uwekezaji wa rasilmali. Kwa hizo, takriban zaidi ya Sh18 bilioni zimetengewa Kenya.”

Irene Ojuok, mtafiti na mtaalam anayefanya kazi na jamii za humu nchini, asema, mpango huu unanuiwa kuhimiza jamii mbali mbali kupanda miti na hivyo kunufaika na hati zinazoruhusu kuzalisha kiwango fulani cha gesi ya dioksidi ya kaboni au gesi nyingine zinazosababisha joto ulimwenguni (carbon credits).

“Kwa sasa Kenya inakumbwa na ukame kiwango cha kwamba hata wanyamapori wameanza kuangamia. Kuna jamii ambazo zimepoteza mifugo yao na huenda zikalazimika kuingilia misitu na Wanyamapori, na hivyo pesa hizi zinanuiwa kujaza hilo pengo hili,” alisema

Shirika la NPC nchini Kenya linatarajiwa kusimamia uhifadhi wa misitu na vyanzo vikuu vya maji katika maeneo ya Mlima Elgon na Cherangany.

Kwa upande mwingine, Kenya iliahidi kusaidia jamii za Rendile, Turkana, Samburu na Borana ambazo zimeathirika pakubwa na mabadiliko ya tabianchi, kukabiliana na shida hii.

Habari hii ilichapishwa kama sehemu ya Ushirikiano wa Vyombo vya Habari kuangazia Mabadiliko ya Tabianchi 2022 unaoongozwa na Mtandao wa Internews wa Kuangazia Habari kuhusu sayari ya Dunia na Kituo cha Stanley cha Amani na Usalama

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro awatafutia wafanyabiashara mikopo

Makatibu wapya 52 wa Ruto wapingwa kortini

T L