• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Kikao cha Urusi, Ukraine chakosa kuzaa matunda

Kikao cha Urusi, Ukraine chakosa kuzaa matunda

NA XINHUA

KIEV, Ukraine

MAZUNGUMZO ya awamu ya tatu na yanayolenga kusitisha operesheni ya kijeshi inayofanywa na Urusi nchini Ukraine yaliyofanyika Belarus, Jumatatu, yalifeli kuzaa matunda.

Hata hivyo, mjumbe mmoja katika mazungumzo hayo, alisema awamu ya nne ya mazungumzo itafanyika “siku chache zijazo”.

“Majadiliano yaligusia masuala ya kisiasa na kijeshi. Hata hivyo, bado hali ni ngumu. Ni mapema kusema tumepiga hatua nzuri,” msaidizi wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, Vladimir Medinsky, alisema.

Afisa huyo pia alikuwa kiongozi wa wajumbe wa Urusi katika mazungumzo hayo.

Wawakilishi wa Urusi waliwasilisha hati zenye makubaliano fulani katika mazungumzo hayo lakini wenzao wa Ukraine walikataa kuzitia saini. Waliomba kupeleka stakabadhi hizo nyumbani ili ziweze kukaguliwa kwa kina zaidi.

“Kwa ukweli matarajio yetu katika mazungumzo hayo hayakufikiwa. Hata hivyo, tunatumai kuwa wakati mwingine tutaweza kupiga hatua muhimu,” Medinsky akawaambia wanahabari baada ya mkutano huo ambao ulidumu kwa karibu saa tatu katika mji wa Belovezhskaya Pushcha.

Mji huo uko katika mpaka wa Belarus na Poland.

Pande zote mbili zilizungumzia suala la kuondolewa kwa raia.

Wajumbe wa Ukraine waliwahakikishia wenzao wa Urusi kwamba raia wote wataondolewa kutoka maeneo yenye vita.

Mkuu wa Kamati ya Bunge la Urusi kuhusu Masuala ya Kimataifa, Leon Slutsky, pia aliongeza kuwa awamu ya nne ya mazungumzo inatarajiwa siku zijazo.

“Awamu nyingine ya mazungumzo yatafanyika nchini Belarus siku chache zijazo. Hata hivyo, siwezi kutaja siku kamili,” Slutsky akawaambia wanahabari.

Mazungumzo hayo yalipeperushwa moja kwa moja kupitia shirika la habari la Urusi Rossiya 24.

Siku hiyo hiyo, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa China, Wang Yi alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mjumbe wa Muungano wa Ulaya (EU) kuhusu masuala ya kigeni na usalama, Joseph Borrell.

Wakati wa mazungumzo hayo, Borrell alimfahamisha Wang kuhusu msimamo wa EU kuhusiana na mzozo wa Ukraine.

Alisema jambo muhimu wakati huu ni kusitishwa kwa vita ili kuzuia maafa zaidi.

EU inapendekeza kuwa mzozo huo usuluhishwe kupitia mazungumzo, Borrell akasema.

Kwa upande wake, Wang alisema suala ambalo linafaa kupewa kipaumbele wakati huu ni utoaji misaada ya kibinadamu kwa watu walioathiriwa na vita hivyo nchini Ukraine.

Aidha, alisema China imewasilisha mapendekezo sita makuu yanayolenga kupunguza madhara ya vita hivyo kwa raia na wageni ambao wanaishi nchini humo, haswa wanafunzi wa asili ya kigeni.

Wang alisema jamii ya kimataifa inafaa kuhimiza Urusi na Ukraine kuendelea na mazungumzo yanayolenga kusitishwa kwa vita na uharibifu wa mali.

You can share this post!

Aliyetoweka kwake 1973 apatikana Lamu

Ustahimilivu umeimarisha ufugaji ng’ombe wa maziwa

T L