• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Ustahimilivu umeimarisha ufugaji ng’ombe wa maziwa

Ustahimilivu umeimarisha ufugaji ng’ombe wa maziwa

NA SAMMY WAWERU

LICHA ya wafugaji nchini kuendelea kulemewa na gharama ya juu ya malisho ya mifugo, Samuel Kinyua na babake, Joseph Karimi wamefanikiwa kuendeleza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Chini ya kipindi cha muda wa mwaka mmoja, chakula cha mifugo cha madukani kimeshuhudia mfumko wa bei mara dufu.

Mradi wa ng’ombe wa wawili hao ukiwa katika Kijiji cha Mukonyo, Kagumo, Kaunti ya Kirinyaga, ni wa kibiashara.

Mzee Karimi aliuanza 1998, ili kuondolea familia yake changamoto za kununua maziwa.

Hatimaye, oda alizopata zilimchochea kuugeuza kuwa mradi wa biashara.

Aliuzindua wakati ambapo si wakazi wengi walikuwa wanafuga ng’ombe wa maziwa. Eneo la Kagumo, ni tajika katika ukuzaji wa kahawa, majanichai na matunda. Anafichua, alianza na ng’ombe wawili pekee, mori na dume.

“Wakati huo, bei ya ng’ombe haikuwa imepanda. Ilinigharimu karibu Sh10, 000,” adokeza.

“Sikuwa na zizi, utangulizi ulikuwa ule wa kuwafungilia kwenye mti au kikingi kwa kamba.

Baadaye, aliwajengea boma analosema lilimgharimu Sh30,000.

Ni kutokana na kuimarika kwa mradi wake, alijumuisha mwanawe kuwa mshirika. Wakiwa na jumla ya ng’ombe wanne, kwa sasa wanakama watatu.

Kuling’ana na Kinyua ambaye humpiga jeki kifedha na kushughulikia malisho, kuna anayezalisha kati ya lita 18 – 20 za maziwa kwa siku. Mwingine, anawatuza lita 10 – 15.

“Anayezalisha kiwango cha chini ni kati ya lita 7 – 10,” Kinyua ambaye pia hufanya biashara ya fanicha aelezea.

Kinachochochea ng’ombe wa wafugaji hao kuwa na uzalishaji bora wa maziwa, kwa mujibu wa maelezo yake ni kuwa makini kwa chakula.

Soko la bidhaa za mifugo likiendelea kukumbwa na matatizo makubwa, Mzee Karimi anasisitiza huzingatia ubora wa chakula. Wametafuta mbinu mbadala kuafikia azma yao katika uzalishaji wa maziwa.

Mzee Joseph Karimi, akikama mmoja wa ng’ombe wake maziwa, katika mradi wake anaoshirikiana na mwanawe Samuel Kinyua, Kagumo, Kaunti ya Kirinyaga. PICHA | SAMMY WAWERU

Kwa kiwango kikubwa, wanategemea nyasi zinazomea shambani, za mabingobingo (napier grass) na majani na matawi ya mahindi.

“Hujikuzia, na pia kununua ili kuepuka gharama ya juu ya chakula cha madukani,” Kinyua asema.

“Tunaposaga majani, humwagilia Pollard na madini faafu kwa ng’ombe wa maziwa,” adokeza.

Hali kadhalika, huwapa chumvi maalum ya mifugo. Kiwango cha maziwa pia kinategemea madini kama; Calcium, Phosphorus, Magnesium, Selenium na Vitamin A, D na E, kwenye chakula.

“Msimu wa mvua, majani huwa tele. Wakulima wajifunze kuyahifadhi kama silage,” ashauri Michael Ngaruiya, mtaalamu wa mifugo.

Chakula cha madukani kikiendelea kuwa ghali, Mzee Karimi analalamikia baadhi ya watengenezaji kushusha ubora wa bidhaa.

“Kuna wakati ng’ombe wawili walikuwa wanatoa jumla ya lita 46. Kwa sababu ya mlo duni na ambao haujaafikia ubora wa bidhaa, kiwango hicho kimeshuka hadi 30,” ateta.

“Huwa makini na kampuni za kutengeneza malisho ya mifugo. Huhakikisha tunachonunua kimeafikia ubora wa bidhaa,” Karimi asisitiza.

Kinyua na babake hufuga bridi aina ya Friesian. Mbegu wanayotumia kujamiisha ni ya Artificial Insemination (AI), Uhamilishaji, njia bora kuimarisha ng’ombe.Safari ya kuimarisha mradi wao hata hivyo haijakuwa mteremko.

Karimi anakumbuka kisa ambapo kampuni moja ilimtapeli lita 600 za maziwa.

“Nilifunguka macho. Kwa sasa soko langu ni wateja rejareja – wanaonunua maziwa kutumia na familia yao,” aelezea.

Huku lita moja akiiuza Sh50, anasema hatua hiyo imemuondolea kero ya mabroka ambao wamevamia soko la mazao ya kilimo na ufugaji.

Changamoto nyingine, ni AI kuwa ghali, Kinyua akisema kwa sasa inagharimu 3,000 kutoka Sh1,000.

You can share this post!

Kikao cha Urusi, Ukraine chakosa kuzaa matunda

Sonko, familia yake wapigwa marufuku ya kuingia Amerika

T L