• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Majonzi Afrika baada ya shujaa wa ukombozi Kenneth Kaunda kufariki

Majonzi Afrika baada ya shujaa wa ukombozi Kenneth Kaunda kufariki

Na MASHIRIKA

Viongozi Afrika wamemwomboleza rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda “KK” aliyefariki Alhamisi akiwa na umri wa miaka 97 wakimsifu kwa wajibu wake katika ukombozi wa Afrika kutoka utawala wa ukoloni.

Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi alimtaja marehemu Kaunda kama kiongozi shujaa aliyehitimu na aliyejitolea kwa maslahi ya nchi yake, ya majirani na binadamu kwa jumla.

Rais Masisi alisema, Kaunda alikuwa rafiki mkubwa wa Botswana wakati ilipokuwa katika hali mbaya zaidi kwenye vita vya kupigania uhuru wake.

Alitangaza kuwa Botswana itaadhimisha siku saba za kumuomboleza marehemu Kaunda.

Katika rambi rambi zake, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alisema nchi hiyo “inamuombeleza baba mpendwa wa ukombozi na umoja wa Afrika – Rais Kenneth ‘KK’ Kaunda”.

Chama tawala Afrika Kusini, African National Congress (ANC), kilimtaja Kaunda kama simba wa ukombozi wa nchi hiyo na wa bara zima la Afrika.

“Dkt Kaunda anashikilia nafasi spesheli katika mioyo ya mapambano yetu, nchi yetu na watu wa Afrika Kusini. Alitufungulia Zambia na kuifanya makao makuu ya ANC kwa miaka zaidi ya 30,” chama hicho kilisema kwenye taarifa.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alisema Afrika imempoteza mpiganiaji uhuru, mzalendo na mtetezi shupavu wa Afrika.

Aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo alimkumbuka Kaunda kama mmoja wa mashujaa wa mwisho wa kupigania uhuru aliyejitolea mhanga kwa njia nyingi.

“Ombi langu ni kuwa kifo cha mwana huyu shujaa wa Afrika na kiongozi kitatukumbusha kuhusu kujitolea kwake na wenzake waliopigania uhuru wa Afrika,” alisema.

Kaunda alifariki akitibiwa Niumonia katika hospitali ya kijeshi katika jiji kuu la Zambia, Lusaka na wasaidizi wake walisema hakuwa na Covid-19.

Mnamo miaka ya 50, Kaunda alikuwa miongoni mwa wapiganiaji wakuu wa ukombozi wa Zambia, iliyofahamika kama Northern Rhodesia.

Alikuwa rais wa kwanza nchi hiyo ilipopata uhuru 1964. Aliondoka mamlakani 1991 aliposhindwa kwenye uchaguzi mfumo wa vyama vingi ulipobisha hodi.

Rais wa Zambia Edgar Lungu alisema kwamba nchi hiyo inamuomboleza shujaa halisi wa Afrika.

“Nimepokea habari za kufariki kwake kwa huzuni mwingi,” alisema.

“Kwa niaba ya nchi yote na kwa niaba yangu binafsi ninaombea faraja familia yote ya Kaunda tunapomuomboleza rais wetu wa kwanza na shujaa halisi wa Afrika.”

Alitangaza kuwa Zambia itamuomboleza Kaunda kwa wiki tatu muda ambao shughuli zote za burundani zitasimamishwa.

Wakfu wa Nelson Mandela Foundation, ulisema kwamba mchango wa Kaunda katika vita dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi hauwezi kusahaulika.

You can share this post!

Wanaokabiliwa na njaa wasajiliwa ili wasaidiwe

NMG yashirikiana na serikali ya Machakos kupanda miche...