• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Marais 10 kuhudhuria ibada ya kumuaga Magufuli Dodoma leo

Marais 10 kuhudhuria ibada ya kumuaga Magufuli Dodoma leo

Na LEONARD ONYANGO

MARAIS zaidi ya kumi wanatarajiwa kuhudhuria ibada ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli itakayofanyika leo Jumatatu katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Msemaji wa Serikali Dkt Hassan Abbas alisema Jumapili kuwa wakuu wa nchi 10 tayari wamethibitisha kuhudhuria ibada ya leo.

Asubuhi, mwili wa Magufuli unapelekwa katika majengo ya Bunge jijini Dodoma kabla ya kupelekwa katika Uwanja wa Jamhuri.

Wakazi wa Dar es Salaam walikamilisha shughuli ya kuaga mwili wa Magufuli jana Jumapili. Wakazi wa Kisiwani Zanzibar watapata fursa ya kuaga mwili wa kiongozi wao kesho Jumanne na baadaye utasafirishwa hadi jijini Mwanza. Wakazi wa Mwanza wataaga mwili wa Magufuli.

Marais zaidi ya 10 watashiriki ibada ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Tangu kupata uhuru wake, Tanzania imepoteza marais watatu; rais wa kwanza Julius Kambarage Nyerere (1999), rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa (2020) na sasa Magufuli (2021).

Hata hivyo, Magufuli ni wa kwanza kufariki akiwa afisini.

Viongozi wa nchi waliofariki wakiwa afisini barani Afrika

Viongozi wa nchi zaidi ya 15 wameaga dunia wakiwa afisini tangu miaka ya 1990.

Aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza alifariki mwaka jana huku akiwa amesalia na chini ya wiki mbili kabla ya kung’atuka mamlakani. Nkurunziza alifariki baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ambapo Evariste Ndayishimiye alichaguliwa kuongoza taifa hilo.

Pierre Nkurunziza

Rais Nkurunziza alifariki akiwa na umri wa miaka 55. Kulingana na serikali ya Burundi, Nkurunziza alifariki kutokana na mshtuko wa moyo kinyume na madai yaliyokuwa yakienezwa mitandaoni kuwa aliuawa na corona.

Michael Sata

Rais wa tano wa Zambia – aliaga dunia mnamo 2014 akiwa na umri wa miaka 77 baada ya kuongoza nchi hiyo wa kipindi cha miaka mitatu kutoka 2011. Serikali haikufichua maradhi yaliyosababisha kifo cha Sata.

Meles Zenawi

Aliyekuwa waziri mkuu wa Ethiopia kwa muda mrefu Meles Zenawi alifariki mnamo 2012 akiwa na umri wa miaka 57. Aliongoza nchi yake tangu mwaka 1991.

Meles alikuwa hajaonekana hadharani kwa wiki kadhaa na kulikuwa na uvumi kuhusu afya yake wakati aliposhindwa kuhudhuria baadhi ya mkutano mjini Addis Ababa.

Atta Mills

Alichaguliwa kuwa rais wa Ghana mnamo 2009 na alifariki kutokana na maradhi ya saratani ya koo na kiharusi akiwa na umri wa miaka 68.

Bingu Mutharika

Alifariki akiwa na umri wa miaka 78 kutokana na mshtuko wa moyo. Makamu wa rais wa Malawi Joyce Banda aliapishwa kuwa rais wa nchi hiyo kufuatia kifo cha Mutharika. Awali, kulikuwa na tetesi kuwa watu wa karibu wa Mutharika walijaribu kubadili katiba ya nchi ili kuzuia Bi Banda kuchukua madaraka na badala yake wampe ndugu yake, Peter Mutharika ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje wakati huo.

Malam Sanha alifariki kutokana na maradhi ya kisukari akiwa na umri wa miaka 64. Taarifa za kifo cha kiongozi huyo zilitolewa na serikali ya Ufaransa ambapo alikuwa akitibiwa.

Serikali ya Sanha nusra ipinduliwe na kundi la wanajeshi waasi alipokuwa akitibiwa nchini Ufaransa.

Muammar Gaddafi

Mnamo 2011, bara la Afrika lilitikisika baada ya kundi la waasi walioungwa na Amerika, kuvamia na kuua aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi katika eneo la Sirte.

Aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama alipongeza wanajeshi waliotekeleza mauji hayo huku akionya kuwa viongozi madikteta katika eneo la Mashariki ya Kati watakabiliwa.

Lakini mnamo 2016, Obama alikiri kuwa alifanya makosa kwa kuua Gaddafi bila kuweka mipango kuhusu jinsi Libya ingeendeshwa baadaye. Libya imekuwa ikiendeshwa na serikali mbili tangu kuuawa kwa Gaddafi.

Umaru Yar’Adua

Mnamo 2010, kiongozi wa Nigeria Umaru Yar’Adua alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alifariki kutokana na matatizo ya moyo.

Alipokuwa akitibiwa ughaibuni bunge la Nigeria lilimpa makamu wake Goodluck Jonathan madaraka ya kuwa Kaimu Rais. Baada ya kifo cha Yar Adua, Jonathan alipenya na kuwa kiongozi wa Nigeria kati ya 2010 na 2015.

Mnamo 2009, Rais Joao Bernardo Vieira (69) wa Guinea Bissau aliuawa na kundi la wanajeshi waasi ambao inaaminika walikuwa wakilipiza kisasi kufuatia mauaji ya mkuu wao wa jeshi.

Msemaji wa jeshi Zamora Induta aliwaambia waandishi wa habari, “Rais Vieira aliuawa na jeshi wakati alikuwa akijaribu kutoroka nyumbani kwake kufuatia mashambulizi ya kundi la wanajeshi.”

Zamora alimshutumu Rais Vieira kwa kuwajibu juu ya mauaji ya mkuu wa jeshi kufuatia sintofahamu kati yao.

Mwaka huo huo, nchi ya Gabon ilipata pigo baada ya kiongozi wake Omar Bongo kuaga dunia kutokana na saratani ya utumbo akiwa na umri wa miaka 72.

Omar Bongo aliongoza Gabon kati ya 1967 na 2009 kabla ya kufariki na kurithiwa na mwanawe Ali Bongo ambaye ni rais wa sasa wa taifa hilo.

Mnamo 2008, Afrika ilipoteza marais wa nchi mbili; Lansana Conte (rais wa pili wa Guinea) na Levy Mwanawasa (Zambia).

Conte alifariki kutokana na maradhi ya kisukari huku Mwanawasa aliuawa na ugonjwa wa kiharusi.

Viongozi wengine waliokufa afisini ni rais wa Togo Gnassingbé Eyadéma (2005) na Laurent-Desire Kabila, kiongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) aliyeuawa kwa risasi na mlinzi wake mnamo 2001.

Mwaka wa 1999, Afrika ilipatwa na pigo baada ya kupoteza viongozi wa mataifa mawili; Mfalme Hassan II wa Morocco na aliyekuwa kiongozi wa Niger Ibrahim Bare Mainassara.

Mainassara aliuawa kwa kumiminiwa risasi katika uwanja wa ndege mjini Niamey.

You can share this post!

Akasha: Shirika lahitaji miezi 6 kwa uchunguzi

TAHARIRI: Serikali ilinde wote mitihani inapoanza