• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Mihemuko kuhusu video ya utani Pakistan

Mihemuko kuhusu video ya utani Pakistan

NA MARY WANGARI

KHYBER PAKHTUNKHWA, PAKISTAN

MWANAFUNZI wa Pakistan mwenye umri wa miaka 19 aliyejitwalia umaarufu kufuatia video yake ya dakika tano, kwenye mitandao ya kijamii kote eneo hilo, ameeleza matumaini yake.

Anatumai kuwa tafsiri tele za mazungumzo yake zitasababisha mjadala zaidi kati ya mataifa jirani hasimu ya India na Pakistan.

Video hiyo fupi, ilirekodiwa na Dananeer Mobeen katika Milima ya Nathaigali, kaskazini mwa Pakistan, na kuchapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram.

Inaonyesha kundi la vijana wakijivinjari kandokando mwa barabara.

Akigeuza kifaa anachotumia kurekodi kumtazama, Mobeen anaashiria nyuma yake na kusema kwa lugha ya Urdu, “Hili ni gari letu, hawa ni sisi, na hii ni burudani yetu inayofanyika.”

Yamkini bila kukusudia chochote, alitaja kimaksudi jina la Kiingereza  “party” kama “pawri” kuwafanyia utani raia wa Asia Kusini wanaoiga lafudhi za kimagharibi.

Kitendo hicho kilivutia ghafla pande zote mbili za mpaka na kuzua heshitegi zilizovuma mno kwenye mitandao ya kijamii, zilizotazamwa na milioni na kuenezwa mara kadhaa Pakistan na India.

“Ilikuwa video ya kawaida mno. Mwanzoni sikuwa na nia ya kuichapisha,” alisimulia Mobeen, akieleza mshangao kwamba ilisambaa mno mitandaoni na kueleza kuwa ilionyesha nguvu na upeo wa mitandao ya kijamii.

Tafsiri za “Pawri” tangu hapo zimetumiwa na polisi nchini India na Tume ya Delhi kuhusu Wanawake katika kampeni zao kwenye mitandao ya kijamii.

Katika video mojawapo, wanajeshi wawili wa India waliotumwa katika milima yenye barafu wanaitafsiri kivyao.

“Hawa ni sisi, hii ni bunduki yetu na tunapiga doria hapa,” wanasema.

Waigizaji nyota wa Bollywood Ranveer Singh na Deepika Padukone walifanya tafsiri zao kila mmoja ambazo vilevile zilisambazwa mno mitandaoni.

Kampuni ya maziwa India inayofahamika kwa kujumuisha mikondo inayovuma kuhusu masuala ibuka katika matangazo yake ilisema “hii ni pav-chai yetu” kuhusiana na kitafunio maarufu kinacholiwa kwa chai wakati wa mapumziko.

Wanasiasa pia walijiunga na msafara huo huku rais wa chama cha Bharatiya Janata, India, akitumia kauli hiyo ya kunata katika mkutano wa hadhara wa uchaguzi.

You can share this post!

Salman taabani kuhusu mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi

Makamu wa Rais Zimbabwe ajiuzulu kuhusu video ya ngono