• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mvua kubwa yaua 357 na kujeruhi 400 Pakistan

Mvua kubwa yaua 357 na kujeruhi 400 Pakistan

NA XINHUA

ISLAMABAD, Pakistan

WATU 357 waliuawa na wengine zaidi ya 400 wakajeruhiwa baada mvua kubwa kushuhudiwa nchini Pakistan kwa zaidi ya wiki tano mfululizo, Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Majanga (NDMA) nchini humo ilisema Alhamisi.

Kando na kusababisha maafa, mvua iliyosababisha mafuriko kote Pakistani tangu Juni 14, pia imeharibu miundomsingi, barabara, nyumba na maduka, duru za NDMA zilisema.

Jumla ya nyumba 23, 792 ziliharibiwa na kuwaacha maelfu ya watu bila makazi, mamlaka hiyo ikaongeza.

Mvua hiyo pia iliharibu madaraja na hivyo kukatiza usafiri wa magari ya abiria na yale ya mizigo kati ya sehemu kadha nchini humo.

Waziri Mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif Alhamisi alisema mvua kubwa inayoshuhudiwa nchini humo inasababishwa na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Mabadiliko ya tabia nchini iko nasi na inasababisha madhara mengi kwa nchini zinazoendelea kama vile Pakistan. Serikali imezingatia mahitaji ya mabadiliko ya tabia katika mipango yake ya maendeleo,” akasema.

Mkoa wa Balochistan ulioko kusini mwa Pakistan ndio umeathirika zaidi baada ya kurekodi jumla ya vifo vya watu 106 kutokana na matukio yanayohusiana na mvua pamoja na mafuriko.

Mkoa wa pili kuathirika zaidi ni Sindh ambako jumla ya watu 90 walikufa na wengine wengi kujeruhiwa.

Watu 76 wameripotiwa kufa katika mkoa wa Punjab mashariki, watu 70 katika kaskazini mwa mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa huku watu 15 wakiuawa katika maeneo mengine ya Pakistan, NDMA ilisema.

Wakati huo huo, wahudumu wa usimamizi wa miji mbalimbali wakisaidiana na wanajeshi wa Pakistan wanaendesha shughuli za uokoaji na usambazaji wa misaada katika maeneo yaliyoathirika na mvua hiyo.

Watawala wanawahamisha watu walioachwa bila makao na kuwapeleka sehemu salama ambako wanapewa chakula, maji na huduma za kimatibabu.

Waziri Mkuu Sharif amebuni kamati maalum ya kukagua kiwango cha uharibifu uliosabishwa na mkasa huo.

Aidha, ametangaza kuwa raia walioathirika watalipwa fidia ya fedha ili kuwawezesha kurejelea maisha yao ya kawaida.

Farzana Bibi, 48, ambaye ni mkazi wa mji wa Karachi, alisema watu wa familia yake hawawezi kuondoka nyumbani kwa sababu barabara katika mtaa wanakoishi zimeloa maji yenye matope.

“Maji ya mafuriko wameingia ndani ya nyumba yangu na kuharibu fanicha na vyombo vingine vya nyumba nilivyonunua juzi. Nimekasirishwa zaidi. Mvua huchukuliwa kama baraka kutoka kwa Mungu lakini imetusababishia usumbufu mkubwa zaidi katika siku za hivi karibuni,” Bibi akaambia Xinhua.

Shirika la kutabiri hali ya anga nchini Pakistan jana Ijumaa lilisema kuwa mvua, inayoandamana na upepo, itaendelea kusambaa katika maeneo ya kaskazini na kati mwa Pakistan kuanzia wiki ijayo.

  • Tags

You can share this post!

Ushirikiano wa kibiashara waimarika baada ya DRC kujiunga...

Utata kuhusu Fomu 34A waondolewa

T L