• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Njaa: Watu 8 milioni hatarini Sudan Kusini

Njaa: Watu 8 milioni hatarini Sudan Kusini

NA AFP

JUBA, SUDAN KUSINI

WATU milioni nane nchini Sudan Kusini, au thuluthi mbili ya idadi ya jumla ya watu katika nchi hiyo inayozongwa na vita, wanakabiliwa na hatari ya kufa njaa, ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) imeonya.

Nchi hiyo, ambayo ni mojawapo ya mataifa maskini zaidi ulimwenguni, imezongwa na vita tangu ilipopata uhuru 2011.

Karibu watu 400,000 wamekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyodumu kwa miaka mitano, vilivyomalizika mnamo 2018.

“Visa vya njaa na utapiamlo vimeongezeka katika maeneo kadhaa ambayo yamekumbwa na mafuriko, ukame na mapigano nchini Sudan Kusini. Baadhi ya familia zinakabiliwa na hatari ya kukumbwa na njaa ikiwa shughuli za utoaji misaada ya kibinadamu hazitadumishwa na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga haitaimarishwa,” ripoti hiyo inasema.

Ripoti hiyo iliyotayarishwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Hazina ya Watoto (UNICEF) na Mpango wa Chakula Ulimwenguni (WFP), inasema kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa na utapiamlo “ni juu zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Sudan Kusini”.

“Idadi ya watu wanaokumbwa na baa la njaa na utapiaji mlo imezidi idadi iliyoshuhudiwa katika miaka ya mapigano kati ya 2013 na 2017,” ripoti hiyo ikaeleza.

Inasema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa jumla ya watu milioni 7.76 kudhuriwa na makali ya uhaba wa chakula hadi mwezi wa Julai 2023.

Aidha, jumla ya watoto milioni 1.4 wanakumbwa na tatizo la utapiamlo.Ripoti hiyo inasema changamoto hiyo imesababishwa na mapigano, hali mbaya ya kiuchumi, majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia-nchi, na ongezeko la bei ya chakula na mafuta.

Mbali na hayo, tatizo hilo limesababishwa na kupunguzwa kwa ufadhili wa mipango ya utoaji misaada ya kibinadamu.

“Tumekuwa tukiendeleza mipango ya kukabiliana na njaa mwaka huu wote na tumezuia madhara mabaya zaidi, lakini hii haitoshi,” Makena Walker, mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini akasema kwenye taarifa.

“Sudan Kusini inaathiriwa zaidi na shida ya mabadiliko ya tabianchi kila siku, familia zinapoteza makazi yao, ng’ombe, mashamba na matumaini kutokana na shida hii,” Walker akasema.

“Bila misaada ya chakula, mamilioni ya watu watajipata katika hali mbaya kiasi kwamba hawataweza kupata mahitaji ya kimsingi ya familia zao,” akaongeza.

Sudan Kusini imekumbwa na mapigano makali, majanga ya kiasili, changamoto za kiuchumi na misukosuko ya kisiasa tangu ilipopata uhuru mnamo 2011.

  • Tags

You can share this post!

Gredi 6: Serikali kutoa mwelekeo wake Desemba

TUSIJE TUKASAHAU: Yusuf Hassan aishinikize serikali...

T L