• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Sonko, familia yake wapigwa marufuku ya kuingia Amerika

Sonko, familia yake wapigwa marufuku ya kuingia Amerika

NA JOSEPH WANGUI

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko pamoja na familia yake wamepigwa marufuku kusafiri Amerika.

Hii ni kuhusiana na madai ya ufisadi ikiwemo matumizi mabaya ya ofisi na kutoa hongo.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana na Mshauri kuhusu Masuala ya Umma katika Ubalozi wa Amerika nchini, Eric Watnik, marufuku dhidi ya Bw Sonko kutoka Amerika inatokana na “kuhusika kwake katika ufisadi uliokithiri” katika hatamu yake fupi kwenye serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Bw Watnik alisema Ubalozi huo umemtangaza Bw Sonko, mkewe Primrose Mbuvi, binti zake Saumu na Salma pamoja na mwanawe ambaye hajahitimu umri, kama watu wasioruhusiwa kuingia Amerika.

Tangazo hilo linamaanisha kuwa vilevile wamepigwa marufuku kufanya biashara yoyote na Amerika.

“Ufisadi wake (Sonko) umeripotiwa mno kwenye vyombo vya habari nchini na kimataifa. Kutokana na haya, Ubalozi huu unasisitiza haja ya kuwepo uwajibikaji, uwazi na heshima kwa sheria kwenye taasisi za kidemokrasia, michakato ya serikali na vitendo vya maafisa wa umma,” alisema Bw Watnik.

“Amerika itaendelea kutumia mbinu zote zinazopatikana kupigana na ufisadi na kupigia debe haki za kibinadamu kote duniani,” alisema hayo kwa niaba ya Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika, Antony Blinken.

Alifichua kuwa idara yake ina habari zilizothibitishwa kwamba Bw Sonko alipokea rushwa kutoka kwa washirikawake ili awapatie zabuni za mabilioni ya pesa.

Mwanasiasa alipanda ngazi kutoka biashara ya matatu hadi akawa gavana wa jiji kuu la Kenya.

Kwa sasa kesi mbili dhidi yake zinaendelea mahakamani kuhusiana na ufisadi, kukiuka kanuni za ununuzi na ulaghai.

Waendesha mashtaka wanasema Bw Sonko alipokea mamilioni ya pesa kupitia mtandao wa ufisadi uliohusisha kampuni zilizopewa kandarasi na serikali ya Nairobi.

Marufuku hiyo imefanyika siku mbili tu baada ya korti kutupa kesi yake ya kupinga kutimuliwa.

You can share this post!

Ustahimilivu umeimarisha ufugaji ng’ombe wa maziwa

Putin asababishia Wakenya kero kuu

T L