• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Talaka ya Uhuru na Ruto baraka kwa Tanzania

Talaka ya Uhuru na Ruto baraka kwa Tanzania

Na WANDISHI WETU

NAIROBI, KENYA

MVUTANO wa kisiasa baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuhusu siasa za urithi 2022 umegeuka kuwa baraka kwa kiongozi wa Tanzania Samia Suluhu.

Mataifa jirani kama vile Uganda, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Burundi ambayo yamekuwa yakipitisha bidhaa katika bandari ya Mombasa, yameanza kutafuta njia mbadala kwa kuhofia joto la kisiasa nchini Kenya.

Mataifa hayo yamekuwa yakiagiza mafuta kutoka ughaibuni kupitia Bandari ya Mombasa.

Uganda imeanza kupitisha mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam na Ziwa Victoria.

Uganda wiki iliyopita, ilisafirisha lita 500,000 za mafuta kutoka Dar es Salaam kwa njia ya reli hadi Mwanza na kisha kuyapeleka Uganda kupitia Ziwa Victoria.

Iwapo Uganda itaanza kupitisha bidhaa zake katika Bandari ya Dar es Salaam, Kenya itapoteza mapato kwa kiwango kikubwa.

Kenya imetumia Sh40 bilioni kukarabati mtandao wake wa mabomba ya mafuta kutoka Mombasa hadi mjini Eldoret. Kadhalika, Kenya ilitumia Sh17 bilioni kujenga kituo cha mafuta ambayo yanasafirishwa nchini Uganda na mataifa mengineyo kupitia Ziwa Victoria.

Kampuni za kusafirisha bidhaa zinahofia kuwa joto la kisiasa linaloendelea kutanda nchini huku Kenya ikijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 9, 2022, huenda likasababisha machafuko sawa na yaliyoshuhudiwa baada ya uchaguzi 2007.

Kampuni za kusafirisha bidhaa za Uganda na Rwanda zililipwa fidia ya Sh12.3 bilioni kutokana na hasara zilizopata kutokana na vurugu za baada ya uchaguzi za 2007. Fidia hiyo ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Masagha Mbogholi.

Lakini Mkurugenzi wa Shirika la Kusafirisha Mafuta (KPC) Macharia Irungu, anasema kuwa hatua hiyo itasababisha Kenya kupoteza asilimia tatu pekee ya bidhaa ambazo hupitishwa katika Bandari ya Mombasa.

Kulingana na Bw Irungu, Tanzania haina bomba la kusafirishia mafuta kutoka Bandari za Dar es Salaam na Tanga hadi Mwanza. Tanzania inategemea matrela kusafirisha mafuta – usafiri anaoutaja kuwa ghali.

Kenya husafirisha lita milioni 900 kila mwezi katika mataifa jirani.

“Ni nafuu kupitisha bidhaa Kenya kuliko Tanzania. Kenya ina mpangilio mzuri wa kusafirisha mafuta na kutoza ushuru. Lakini Tanzania hawana mpangilio wowote. Kenya ina uwezo wa kusafirisha lita milioni 1 kutoka Bandari ya Mombasa hadi Nairobi kwa saa. Itachukua miaka mingi Tanzania kupokonya Kenya soko la Uganda,” akasema.

Kaimu wa Shirika la Reli la Uganda (URC) Stephen Wakasenza wiki iliyopita alisema kuwa nchi hiyo imeanza mikakati ya kutafuta njia mbadala ya kupitisha bidhaa zake.

“Sasa tunalenga kutumia njia mbili; Bandari ya Kisumu na Bandari ya Mwanza, kupeleka lita milioni 20 za mafuta kila mwezi,” akasema Bw Wakasenza.

Kenya, Uganda na Rwanda tayari zimeachana na mradi wa pamoja wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Eldoret-Kampala hadi Kigali. Mradi huo ungegharimu Sh150 bilioni.

Tangu Rais Suluhu alipotwaa hatamu za uongozi wa Tanzania kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli mnamo Machi 17, 2021, amekuwa akilenga ushirikiano wa kibiashara kutoka kwa mataifa jirani.

Rais Suluhu amekuwa akiwakikishia viongozi wenzake wa ukanda huu kuwa Tanzania ni thabiti na ina mazingira bora ya kufanyia biashara.

Iwapo mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo utakamilika, Bandari ya Mombasa huenda ikapata pigo kubwa.

You can share this post!

Chipukizi Oduor afungia Barnsley goli ikizima Sheffield...

Mswada bungeni kubuni ‘mwakilishi-wazee’