• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Tukataeni ushoga, Museveni arai Waafrika

Tukataeni ushoga, Museveni arai Waafrika

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amezirai serikali za Afrika kuongoza juhudi za kuongoza mpango wa kukataa ushoga, akiutaja kuwa “tishio kwa ubinadamu”.

Museveni alitaja ushoga kama tishio na hatari kubwa kwa mchakato wa uzao kwa binadamu. Alitoa kauli hiyo Jumapili.

“Afrika inafaa kuongoza juhudi za kuiokoa dunia kutoka kwa mporomoko huu wa kimaadili, ambao ni hatari sana kwa ubinadamu,” akasema Museveni.

Museveni alisema hayo baada ya kukutana na ujumbe wa wabunge kutoka nchi 22 za Afrika na Uingereza.

Kundi hilo lilikuwa limekongamana kwa Kikao cha Kwanza cha Mabunge kuhusu Maadili ya Kifamilia na Uhuru chini ya kaulimbiu “Kulinda Utamaduni wa Kiafrika na Maadili ya Kifamilia” jijini Entebbe, ulio umbali wa kilomita 40 kutoka jiji kuu, Kampala.

Kauli yake pia ilijiri mwezi mmoja baada ya Bunge la taifa hilo kukubali hoja yenye utata inayopiga marufuku ndoa za jinsia moja. Kwa sasa, mswada huo unangoja kutiwa saini na kiongozi huyo ili kuwa sheria.

Mswada huo unapendekeza kupigwa marufuku kwa vitendo vyote vinavyohusiana na ushoga. Pia, unapendekeza kulipwa ridhaa kwa waathiriwa wa vitendo vinavyohusiana na ushoga.

Bunge la taifa hilo lilipitisha sheria hiyo mara ya kwanza mnamo Desemba 20, 2013, lakini ilifutiliwa mbalo mnamo 2014 na mahakama ya kikatiba, ikisema hakukuwepo na wabunge wa kutosha ilipopitishwa kuwa sheria.

Wakati huo huo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) leo Jumatatu waliwataja maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Sudan Kusini waliosema wanafaa kukamatwa na kuchunguzwa kwa ukatili ambao wamewafanyia raia.

Kwenye ripoti hiyo ambayo ilitolewa na Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu (UNCHR) nchini humo, maafisa wa ngazi za juu wa serikali na jeshi walitajwa kuwa wahusika wakuu kwenye ukatili ambao umekuwa ukiendeshwa dhidi ya raia.

Baadhi ya vitendo vya ukatili huo ni mauaji, ubakaji na utumwa wa kingono.
Ripoti hiyo inafuatia uchunguzi uliofanywa na tume hiyo kwa muda wa mwaka mmoja katika majimbo sita nchini himo.

“Kwa miaka mingi, chunguzi zetu zimekuwa zikibainisha kuwa ukatili dhidi ya raia umekuwa ukiendeshwa na kufadhiliwa na maafisa wakuu wa serikali na jeshi,” akasema Kamishna Mkuu wa tume hiyo, Yasmin Sooka.

“Tumechukua hatua ya kuwataja watu wenye ushawishi ambao wamekuwa wakihusika katika maovu hayo yanayokiuka haki za binadamu,” akasema.

Baadhi ya watu waliotajwa ni Gavana wa Jimbo la Unity Joseph Monytuil na Lutemi Jenerali Thoi Channy Reat wa kundi la South Sudan People’s Defence Forces. Wanadaiwa kuongoza mauaji katika Kaunti ya Mayom mnamo Agosti mwaka 2022.

Wengine waliotajwa ni Gordon Koang, anayehusishwa na kuongoza mauaji ya raia katika Kaunti ya Leer kati ya Februari na Aprili 2022.

  • Tags

You can share this post!

Nitabeba msalaba wa wenzangu, mchungaji aambia mahakama

‘Ghost’ Mulee ndiye kocha mpya wa Gaspo Women

T L