• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Ulimwengu kumuaga Malkia kishujaa leo

Ulimwengu kumuaga Malkia kishujaa leo

NA MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

ZAIDI ya viongozi 200 kutoka sehemu tofauti duniani wataungana na Uingereza kumuaga Malkia Elizabeth II, aliyefariki wiki mbili zilizopita akiwa na umri wa miaka 96.

Hafla hiyo itafanyika katika kanisa la Westminister Abbey.

Inatarajiwa kutazamwa na mamilioni ya watu katika sehemu tofauti duniani.

Mfalme Charles III ndiye anayetarajiwa kuwakaribisha viongozi hao kwa niaba ya familia ya kifalme na serikali ya Uingereza.

Rais Joe Biden wa Amerika aliwasili jijini London Jumamosi.

Hafla hiyo inatajwa kuwa kubwa zaidi tangu mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa waziri mkuu wa taifa hilo, Winston Churchill mnamo 1965.

Malkia Elizabeth alifariki mnamo Septemba 8 baada ya kuliongoza taifa hilo kwa miaka 70.

Maelfu ya watu wamekuwa wakipanga foleni kuutazama mwili wake katika majengo ya Bunge la Uingereza.

Picha ya Malkia Elizabeth II ikiwa katikati ya maua pamoja na risala za rambirambi kushoro katika bustani ya Green Park jijini London, Uingereza jana. Malkia huyo aliyeaga dunia Septemba 8 atazikwa leo huku Mfalme Charles III akitarajiwa kuwapokea wageni mbalimbali kutoka pembe nyingi za dunia. PICHA | AFP

Kulingana na taratibu zilizowekwa, wale wanaolenga kuutazama mwili huo wana hadi leo, Jumatatu, alfajiri kuutazama katika jumba la Westminister Hall.

Waombolezaji wamekuwa wakingoja hadi saa 25 kwenye foleni kuutazama mwili huo.

Hapo jana Jumapili, iliwalazimu maafisa wa serikali kuwazuia watu zaidi kupanga foleni.

Shaun Mauyo, 27, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya teknolojia, ni miongoni mwa watu wachache waliofaulu kuutazama mwili wa Malkia, baada ya kukaa kwenye foleni kwa muda wa saa 14.

“Nilishikwa na hisia nyingi. Alikuwa kama nyanya wa taifa,” akasema, kwenye mahojiano na wahahabari.

“Tutamkosa sana,” akaongeza.

Kutokana na muda mrefu ambao watu walikuwa wakingoja ili kuutazama mwili huo, baadhi yao walikata tamaa.

Mnamo Jumamosi, polisi walimkamata mwanamume mmoja aliyeruka foleni karibu na jeneza la Malkia.

Mwanamume huyo, aliyetambuliwa kama Muhammad Khan, 28, alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya “kuusumbua umma”. Anatoka mashariki mwa jiji la London.

Siku iyo hiyo, Mwanamfalme William na nduguye, Mwanamfalme Harry, waliwaongoza wajukuu wanane wa Malkia kwa hafla fupi ya dakika 12, kukumbuka maisha yake.

Harry alikuwa amevalia mavazi maalum ya kijeshi.

Baadhi ya viongozi ambao tayari washatoa heshima zao za mwisho kwa Malkia ni mawaziri wakuu Jacinda Arden (New Zealand), Anthony Albanese (Australia), Justin Trudeau (Canada) miongoni mwa wengine.

“Katika wakati huu mgumu wa maombolezo, tunatoa heshima zetu za mwisho kwa Malkia Elizabeth kutokana na kujitolea kwake kutekeleza majukumu yote aliyohitajika kuyatimiza,” akasema Albanese kupitia mtandao wa Twitter.

Trudeau alisema kuwa “Malkia Elizabeth aliwaongoza na kuwahudumia raia wa Uingereza kwa uungwana”.

Hafla ya leo Jumatatu inafikisha kikomo maombolezo ambayo yamekuwa yakiendelea kwa jumla ya siku 11 zilizopita.

Rais William Ruto ni miongoni mwa viongozi ambao washasafiri jijini London kuhudhuria mazishi hayo.

Uingereza imekuwa ikishinikizwa na baadhi ya mataifa yaliyokuwa koloni zake kuomba msamaha kwa ukatili uliotekelezwa na polisi wake dhidi ya Waafrika.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wabunge watumikie raia kwa uaminifu

WANTO WARUI: Hekima yahitajika kufanya uamuzi kuhusu...

T L