• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Wafanyikazi wahimiza vita Ukraine vimalizwe

Wafanyikazi wahimiza vita Ukraine vimalizwe

NA MASHIRIKA

MAMILIONI ya raia na makundi ya wafanyakazi, Jumapili yaliungana katika sehemu mbalimbali duniani kuadhimisha Leba Dei yakilalamikia athari za kiuchumi zinazotokana na vita vinavyoendelea kati ya Ukraine na Urusi.

Viongozi wa makundi hayo waliionya Urusi kuwa huenda vita hivyo vikaenea katika maeneo mengine barani Ulaya.

Nchini Uturuki, polisi waliwakabili vikali waandamanaji waliofika katika eneo la Taksim Square, jijini Instanbul. Eneo hilo ndiko kulikotokea maandamano makubwa nchini humo mnamo 1977, ambako watu 34 waliuawa.

Afisi ya gavana wa jiji hilo ilisema kuwa jumla ya watu 164 walikamatwa na polisi.

Nchini Sri Lanka, maelfu ya watu waliandamana katika jiji kuu la taifa hilo, Colombo, wakimshinikiza Rais Gotabaya Rajapaska kujiuzulu pamoja na serikali yake. Walimlaumu kutokana na ongezeko la gharama ya maisha. Wengi pia waliutaka Umoja wa Mataifa (UN) kuingilia kati kwenye vita vinavyoendelea Ukraine, wakivitaja kuwa mojawapo ya sababu ambazo zimechangia mzozo wa kiuchumi unaoikumba nchi hiyo.

Nchini China, siku hiyo iliadhimishwa kwa utulivu jijini Beijing na maeneo mengine, kutokana na masharti yaliyowekwa na serikali kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Ijapokuwa China imekuwa ikiepuka kujiingiza kwenye mzozo wa Urusi na Ukraine, raia wake waliandika jumbe kwenye mitandao ya kijamii kushinikiza amani duniani.

Nchini Italia, washiriki wa maandamano walitoa wito vita hivyo kukamilika.

Waandalizi wa sherehe hizo waliandaa tamasha kubwa jijini Roma, ambalo liliyaleta pamoja makundi matatu makuu ya wafanyakazi nchini humo.

“Tunataka hali ya amani kuwepo duniani,” akasema mwandalizi mmoja.

Nchini Ugiriki, zaidi ya watu 10,000 walifanya maandamano katika jiji kuu, Athens, wakilalamikia gharama ya juu ya maisha.

Walilalamikia bei ghali ya gesi na umeme kutokana na vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimewekewa Urusi.

“Hali ni ngumu sana. Inaendelea kuwa ngumu kwa wafanyakazi kutokana na gharama ya juu ya bidhaa. Tutaikabili kwani hatuwezi kuishi hivi,” akasema Katerina Dekaristoou, ambaye ni mwalimu.

Nchini Bulgaria, Rais Rumen Radev wa taifa hilo alionya kuwa kuna uwezekano vita hivyo vikasambaa kote barani Ulaya na duniani kote kwa jumla.Alisema kuwa mataifa ya Ulaya yanapaswa kuwa katika hali ya tahadhari.

“Makazi yetu, watoto wetu na nchi yetu kwa jumla iko kwenye hatari ya kuathiriwa na mapigano hayo,” akaonya.

Kiongozi huyo alisema kuwa hawatajihusisha kwa vyovyote kwenye vita hivyo.

Nchi hiyo imekuwa kwenye njiapanda kuhusu ikiwa inafaa kupeleka wanajeshi na silaha za kivita nchini Ukraine au la.

  • Tags

You can share this post!

Joho aapa kuzima Sonko Mombasa

Ndoto za nyota wa KCPE zafifia kwa kukosa karo

T L