• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Joho aapa kuzima Sonko Mombasa

Joho aapa kuzima Sonko Mombasa

NA ANTHONY KITIMO

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, amepuuzilia mbali ujio wa aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kwa siasa za Mombasa.

Bw Sonko alijitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania ugavana Mombasa wiki chache zilizopita, kupitia chama cha Wiper kinachoongozwa na Bw Kalonzo Musyoka.

Huku akipiga mbiu ya siasa zilizokuwa zimetulia Pwani msimu wa Ramadhan jana Jumatatu, Bw Joho ambaye ni naibu kiongozi wa ODM, alikosoa Wiper kwa kumruhusu Bw Sonko kuwania ugavana kaunti hiyo.

Kulingana naye, hatua hiyo ni kinyume na ushirikiano wa vyama chini ya Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, ndiye mgombeaji ugavana wa Mombasa kupitia kwa ODM.

“Tunaona rafiki zetu wengine wameamua kuleta ushindani katika ngome yetu lakini tutatumia rasilimali zetu zote kwa njia ya amani kuhakikisha wakazi wa Mombasa wanapata gavana anayefahamu shida zao,” akasema.

Bw Joho alieleza kuwa mipango yake ya kukabidhi mamlaka kwa kiongozi anayeamini ndiye bora, ilianza zamani na hayuko radhi kuzima azimio lake.

“Tangu nilipoingia mamlakani 2017 nilichukua muda kuhakikisha nitakabidhi mamlaka kwa mtu anayefaa ambaye ni Bw Nassir. Yeyote anayedhani anaweza kuja hapa dakika za mwisho kubadili mawazo ya watu wetu kupitia kwa propaganda na pesa, ajue hatuko tayari kukubali watu ambao walikataliwa kwingine,” akasema.

Alikuwa akizungumza baada ya sala ya Eid ya kukamilisha Ramadhan iliyohudhuriwa na mamia ya waumini wa Kiislamu.

Bw Joho alisema ingawa atajishughulisha sana na siasa za kitaifa kuelekea kwa uchaguzi wa Agosti 9, atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa Bw Nassir ndiye ameibuka mshindi wa ugavana Mombasa.

“Nitalaumiwa ikiwa nitaacha kiti hiki kwa mtu asiyefaa. Kwa kuwa wameamua kuvamia ngome yetu, sasa tutapiga kampeni ya kushawishi wafuasi wetu wa Mombasa kupigia kura wagombeaji wote wa ODM kuanzia kwa urais ambapo Bw Raila Odinga ndiye mgombeaji wetu, hadi chini katika kaunti,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Nassir alidai kuwa Bw Musyoka alimwidhinisha Bw Sonko kuwania ugavana katika jiji hilo ili kumpiga vita Bw Odinga.

Alimtaka kiongozi huyo wa Wiper akome kuingilia siasa za Mombasa kwa kumshinikiza Bw Sonko kuwania ugavana.

Wakati uo huo, aliwashauri wapigakura pia wasikubali kumchagua aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, ambaye atapeperusha bendera ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi huo wa ugavana.

Wanasiasa wengine wanaomezea mate kiti hicho ni Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi wa Chama cha Pamoja African Alliance (PAA), na aliyekuwa Mbunge wa Nyali, Bw Hezron Awiti wa Chama cha Vibrant Democratic Party.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge wa Uingereza ajiuzulu kwa kosa la kutazama video...

Wafanyikazi wahimiza vita Ukraine vimalizwe

T L