• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Wanajeshi wa Uganda walia kuzidiwa ujanja

Wanajeshi wa Uganda walia kuzidiwa ujanja

THE EASTAFRICAN

WANAJESHI wa Uganda waliotumwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupambana na makundi ya waasi, wamezidiwa maarifa na wanamgambo hao.

Majeshi ya Uganda (UPDF) yalipelekwa nchini DRC mnamo Novemba 30, mwaka jana kupambana na wanamgambo wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) ambalo limetangaza kuwa mshirika wa mtandao wa kigaidi wa Islamic State (IS).

Kundi la ADF limehusika na mashambulio kadhaa nchini Uganda huku shambulio la hivi majuzi likiwa lile la Oktoba 2021, ambapo watu watatu waliuawa baada ya mabomu mawili kulipuka jijini Kampala.

Wanajeshi wa UPDF wamekuwa wakishirikiana na wenzao wa Congo (FARDC) kuendesha operesheni hiyo dhidi ya ADF.

Lakini waasi wa ADF wamekuwa wakivalia sare za wanajeshi wa UPDF na FARDC na kuvamia vijiji kaskazini wma DRC.

Wakuu wa majeshi wa nchi hizo mbili sasa wanasema kwamba waasi wanalenga kukasirisha raia wa DRC ili waanzishe maandamano ya kupinga operesheni inayoendeshwa na wanajeshi wa UPDF na FARDC.

Taarifa ya pamoja ya wanajeshi hao Jumatano ilisema kuwa wapiganaji wa ADF wanapanga kutekeleza shambulio jingine dhidi ya raia huku wakijifanya wanajeshi wa Uganda na DRC.

Wasemaji wa UPDF na FARDC Brigedia-Jenerali Flavia Byekwaso na Meja Jenerali Leon Richard Kasonga mtawalia, walisema: “Taarifa za kijasusi tulizo nazo zinaonyesha kwamba wanamgambo sasa wanavalia sare za wanajeshi wetu na kwenda kuvamia raia. Lengo lao ni kutatiza operesheni inayoendelea dhidi ya ADF.”

Wasemaji hao wa vikosi vya Uganda na DRC walisema kuwa waasi hao wanapanga kuua watu ili ionekane kwamba wanauawa na wanajeshi wa UPDF na FARDC.

“Lengo lao kuu ni kuharibu sifa ya majeshi ya Uganda na DRC ambayo yamekuwa yakiendesha operesheni kali dhidi ya ADF. Wanajeshi wetu wanaheshimu haki za kibinadamu,” ikasema taarifa hiyo.

Wanajeshi wa Uganda mapema mwezi huu, walisema kuwa walifanikiwa kuzidi nguvu waasi wa ADF. Wanajeshi hao walidai kuwa walifanikiwa kuharibu kambi sita za mwisho za ADF mashariki wa DRC.

Byekwaso alisema kuwa walifanikiwa kuharibu Kambi ya Yua ambayo ni kambi kuu ya mafunzo ya ADF.

Kambi nyingine zilizoharibiwa ni Belu I, Belu II, Mombasa naKambi Erumu zilizoko katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Ripoti ya waataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa 2013, ilisema kuwa kundi la ADF lina kati ya wapiganaji 1,200 na 1,500 mkoani Kivu Kaskazini karibu na mpaka wa Uganda.

Upinzani nchini Uganda umeshutumu Rais Yoweri Museveni kwa kupeleka wanajeshi nchini DRC bila idhini ya bunge la nchi hiyo.

Mnamo Desemba 2021, raia 12 na wanamgambo 38 wa ADF waliuawa kaskazini mashariki mwa DRC kufuatia mapigano makali baina ya wanamgambo hao na wanajeshi.

  • Tags

You can share this post!

COVID-19: Burkina Faso kukosa nahodha wao dhidi ya Cape...

SGR: Jinsi Wachina walivyozima Uhuru

T L