• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
COVID-19: Burkina Faso kukosa nahodha wao dhidi ya Cape Verde huku Senegal wakiathiriwa zaidi

COVID-19: Burkina Faso kukosa nahodha wao dhidi ya Cape Verde huku Senegal wakiathiriwa zaidi

Na MASHIRIKA

NAHODHA wa Burkina Faso, Bertrand Traore hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachovaana na Cape Verde katika mchuano wa pili wa Kundi A kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon usiku wa Januari 13, 2022 baada ya kupatikana na virusi vya corona.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 anayechezea Aston Villa ya Uingereza alivalia utepe wa unahodha wakati wa mechi ya ufunguzi dhidi ya wenyeji Cameroon mnamo Januari 9, 2022. Kikosi chao kilipigwa 2-1 katika mchuano huo.

Mbali na mechi dhidi ya Cape Verde, Traore atakosa pia mchuano wa mwisho wa Kundi A utakaokutanisha Burkina Faso na Ethiopia mnamo Januari 17, 2022. Sasa Issoufou Dayo atakuwa kapteni mpya wa Burkina Faso kwenye michuano hiyo.

Kwa upande wao, Cape Verde watakaribisha idadi kubwa ya wachezaji wao waliokosa gozi dhidi ya Ethiopia baada ya kupona Covid-19. Licha ya Cape Verde almaarufu The Blue Sharks kukosa wanasoka 11 dhidi ya Ethiopia, walishinda 1-0.

Kwingineko, wanafainali wa 2002 na 2019, Senegal watakuwa bila wachezaji Fode Ballo-Toure, Idrissa Gana Gueye, Edouard Mendy na Kalidou Koulibaly katika mchuano wa Kundi B dhidi ya Guinea kutokana na virusi vya corona.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Korea Kaskazini yatishia kuunda nyuklia kali zaidi

Wanajeshi wa Uganda walia kuzidiwa ujanja

T L