• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
WANDERI KAMAU: Tusimhukumu Trump, tujifunze kutoka kwa makosa yake

WANDERI KAMAU: Tusimhukumu Trump, tujifunze kutoka kwa makosa yake

Na WANDERI KAMAU

NI dhahiri kwamba huwa vigumu sana kwa marais wanaong’atuka uongozini baada ya kushindwa na wapinzani wao kwenye chaguzi kuu kuzoea tena maisha ya kawaida.

Hali hiyo huashiria mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yao. Ni mabadiliko magumu ya kimaisha; kutoka maisha ya hekima hadi yale ya kawaida.

Ikizingatiwa wao pia ni wanadamu, kuna ugumu kuyazoea maisha mapya ambayo hayana mbwembwe za kupigiwa saluti, kufanyiwa majukumu mengi na wasaidizi, kusafiri mtu atakako bila kugharimia malipo ya usafiri kati ya majukumu mengine.

Kando na hayo, marais wanaong’atuka uongozini pia hupigwa msasa sana kuhusu athari za sera zao katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kitamaduni kwa raia na nchi zao kwa jumla.

Ikiwa vitendo vyao havikuwaridhisha wengi, basi hilo huwa msingi wa kuekelezewa kila aina ya lawama.

Ikiwa sera zao ni za kuifaidi nchi, wao husifiwa kama mashujaa na wakombozi walioziongoza nchi zao kujitoa kutoka minyororo ya mahangaiko ya kisiasa na kiuchumi.

Ni hali ambayo amejipata aliyekuwa rais wa Amerika, Bw Donald Trump, baada ya Rais Mpya Joe Biden, kuapishwa rasmi mnamo Jumatano.

Kutokana na kutoamini kuwa Biden aliibuka mshindi kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 3 mwaka uliopita, Trump hakuhudhuria hafla ya kumwapisha kiongozi huyo mpya.

Ni kitendo kilichovunja kanuni na taratibu ambazo huzingatiwa na marais wa Amerika wanaowapokeza wenzao uongozi mpya.

Katika kipindi cha utawala wake kati ya 2016 na 2020, Trump aliwakasirisha sana watu na viongozi wengi duniani.

Ghadhabu na lawama dhidi yake zilitokana na sera alizoanza kutekeleza kwa lengo la “kurejesha hadhi ya Amerika.”

Zilikuwa sera za kibaguzi, ambazo ziliwaonea raia wa kigeni, hasa wahamiaji waliotafuta hifadhi Amerika.

Hata hivyo, Trump alisahau kuwa historia yake itaandikwa kulingana na vitendo alivyofanya. Lakini licha ya kukosolewa na watu ambao hawakuupenda uongozi wake, ama waliteseka kwa namna moja ama nyingine, si haki kumworodhesha Trump kama “kiongozi mbaya zaidi” katika historia ya Amerika.

Sababu kuu ni kuwa kando na Trump, kuna viongozi ambao wamefanya vitendo vibaya zaidi katika nchi zao. Barani Afrika, kuna marais ambao wanaokabiliwa na tuhuma za kuongoza harakati za mauaji dhidi ya watu wanaoachukulia kama “maadui wao.”

Kuna viongozi wengine kama Adolf Hitler ambao waliongoza mauaji ya mamilioni ya Wayahudi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Mbona tumlaumu Trump?

Badala ya lawama, tunapaswa kujifunza kutokana na makosa yake.

[email protected]

You can share this post!

Uingereza yapendekza wanaougua corona walipwe Sh65,000

DOUGLAS MUTUA: Kenya, Afrika zitafaidikaje kwa utawala wa...