• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Watekaji nyara wamnyaka mzee aliyewapelekea Sh7m

Watekaji nyara wamnyaka mzee aliyewapelekea Sh7m

Na MASHIRIKA

ABUJA, NIGERIA

WATEKAJI nyara Jumapili walimkamata mtu ambaye alikuwa ametumwa kuwasilisha ngawira – malipo kwa mtekaji – kabla ya kuwaachilia watoto 136 wa shule waliokuwa wakizuiliwa Kaskazini mwa Nigeria.

Mwanamume huyo ambaye ni mkongwe alitumwa na wazazi wa watoto hao ambao walikuwa wamechangisha Sh7 milioni wakitumai wangewaachilia huru ili waungane nao tena.

Hata hivyo, wazazi wa watoto hao sasa wametamauka zaidi, wakishangazwa na tukio hilo. Baadhi yao walikuwa wameyauza mashamba yao na mali nyingine ili kupata pesa hizo za juu zilizokuwa zikitakikana.

Taifa hilo limekuwa likikumbwa na visa vingi vya utekaji nyara hasa watoto wa shule huku wahalifu na watekaji nyara wakiitisha pesa za juu la sivyo wawaue watoto hao.

Ingawa watekaji nyara wamekuwa wakipokea pesa na kuwaachilia watoto, kisa cha jana kinashangaza kwa kuwa anayepeleka pesa hizo huwa hazuiliwi.

Jumapili, watekaji nyara hao walipiga simu na kuwaeleza walimu wakuu wa shule hiyo kuwa pesa zilizowasilishwa si zile walizoagana wangepokezwa.

Watoto hao wanatoka katika majimbo ya Tegina na Niger walitekwa mwezi Mei.

Wakati huo, watu waliojifunika nyuso wakiwa kwenye pikipiki walifika katika mji huo kisha kuwapiga risasi watu wote waliokuwepo kisha kumuua mmoja wao na kuwajeruhi wengine.

Watu walipokuwa wakitoweka, wavamizi hao walielekea shuleni kisha kuwanyaka watoto hao na kuenda nao.

Baadaye wazazi na wasimamizi wa shule walikubaliana na watekaji nyara hao na wakakubali kulipa pesa zilizokuwa zikihitajika. Waliuza kipande cha shamba la shule na mali nyingine ili kupata pesa zilizohitajika.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Malam Abubakar Alhassan alifichua kuwa watu sita walitumwa ili wakutane na watekaji nyara hao karibu na msitu ambao watoto hao walikuwa wakizuiliwa kisha walipe pesa hizo ndipo watoto hao waachiliwe.

Walipowasili, watekaji nyara hao waliamrisha kuwa mzee mmoja aliyekuwa katika kundi hilo aandamane nao hadi ndani ya msitu ndipo wahesabu pesa hizo.

Hata hivyo, walipiga simu baadaye kusema pesa hizo hazikutosha kiwango kinachohitajika ndipo wakamzuilia mzee huyo pia.

“Wazazi sasa wameacha hatima ya watoto hao mikononi mwa Mungu. Sasa wanasema kuwa hawawezi kuchangisha fedha zaidi wala hawatashiriki mchango wowote,” akasema Alhassan.

Zaidi ya wanafunzi 1,000 wametekwa nyara kutoka shule mbalimbali Kaskazini mwa Nigeria tangu Disemba mwaka jana.

Wengi wao bado wanaendelea kuzuiliwa huku wananchi wakikosoa serikali kwa kutofanya lolote kuzuia visa vya utekaji nyara vilivyokithiri.

You can share this post!

Mulembe wapigania minofu ya Uhuru

Kenya Shujaa yasalimu amri ya Amerika raga ya wachezaji...