• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Kenya Shujaa yasalimu amri ya Amerika raga ya wachezaji saba kila upande Olimpiki

Kenya Shujaa yasalimu amri ya Amerika raga ya wachezaji saba kila upande Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya Shujaa imeanza kampeni yake ya Olimpiki 2020 kwa kupoteza kwa alama 19-14 dhidi ya Amerika jijini Tokyo, Japan mapema Jumatatu.

Vijana wa kocha Innocent “Namcos” Simiyu pia watapepetana na Afrika Kusini saa saba mchana leo Jumatatu halafu wakamilishe mechi za Kundi C dhidi ya Ireland hapo Julai 27.

Afrika Kusini, ambayo ilizoa medali ya shaba kwenye Olimpiki 2016 jijini Rio de Janeiro nchini Brazil, imepepeta Ireland 33-14.

Collins Injera na Jeff Oluoch walifunga miguso ya Kenya naye Eden Agero akapachika mikwaju ya miguso hiyo.

Amerika, ambayo inanolewa na kocha wa zamani wa Kenya Mike Friday, ilizima Shujaa kupitia miguso ya Martin Iosefo, nahodha Madison Hughes, na Carlin Isles. Steve Tomasin na Hughes pia walichangia mkwaju mmoja kila mmoja. Amerika iliongoza 12-0 kupitia kwa miguso ya Isles na Iosefo na mkwaju kutoka kwa Hughes kabla ya Kenya kusawazisha 14-14 ilipopata miguso kutoka kwa Injera na Oluoch na mikwaju ya miguso hiyo kutoka kwa Agero. Hata hivyo, Hughes alifunga mguso wa ushindi dakika ya mwisho ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Tomasin.

Kabla ya Olimpiki, Shujaa na Amerika zilikutana mara mbili jijini Madrid nchini Uhispania. Mnamo Februari 21, Shujaa ilichapa Amerika 38-7 kupitia miguso ya William Ambaka, Jacob Ojee, Johnstone Olindi, Herman Humwa na Billy Odhiambo na mikwaju ya Tony Omondi. Perry Baker alifungia Amerika mguso wa pekee.

Shujaa na Amerika zilikutana tena katika mashindano ya pili ya Madrid mnamo Februari 27. Vijana wa Simiyu pia waliibuka na ushindi katika mchuano huo 29-12. Ambaka, Onyala, Taabu na Alvin Otieno walifunga miguso ya Shujaa.

Kabla ya kupiga Amerika mara mbili jijini Madrid, Shujaa ilikuwa imepoteza mechi nne mfululizo dhidi ya Waamerika hao 41-0 (Februari 2), 26-10 (Machi 3), 17-14 (Aprili 13) na 26-14 (Juni 2) mwaka 2019 kwenye Raga za Dunia.

Afrika Kusini imelemea Kenya mara 15 na kupoteza mchuano mmoja kati ya 16 zilizopita kwa hivyo Shujaa ina kibarua kigumu.

Kikosi cha Shujaa jijini Tokyo: William Ambaka, Vincent Onyala, Herman Humwa, Collins Injera, Eden Agero, Billy Odhiambo, Nelson Oyoo, Andrew Amonde (nahodha), Alvin Otieno, Daniel Taabu, Johnstone Olindi, Jeff Oluoch na Jacob Ojee.

You can share this post!

Watekaji nyara wamnyaka mzee aliyewapelekea Sh7m

Andy Murray ajiondoa kwenye tenisi ya mchezaji mmoja kila...