• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Watu 7 wauawa katika shambulio la kigaidi Mogadishu

Watu 7 wauawa katika shambulio la kigaidi Mogadishu

Na MASHIRIKA

MOGADISHU, Somalia

WATU saba wamefariki jijini Mogadishu Jumamosi, Septemba 25, 2021 kutokana na shambulio la kigaidi lililotekelezwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga.

Shambulio hilo lilitokea katika makutano ya barabara karibu na makazi ya Rais, kulingana na taarifa fupi iliyotolewa na afisa mmoja wa ngazi ya juu katika serikali ya Somalia.

Alisema mshambuliaji huyo alikuwa ameteka bomu hilo ndani ya gari aliloliegesha eneo hilo.

“Mshambuliaji wa kujitoa mhanga alilipua bomu lililotegwa ndani ya gari katika makutano ya barabara ya Ceelgaab na kuwaua watu saba. Watu wengine wanane pia wamejeruhiwa katika kisa hicho, Muawiye Mudeey, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Hamarjajab, Mogadishu,” aliwaambia wanahabari.

Haikujulikana mara moja aliyehusika na shambulio hilo.

Hata hivyo, kundi la wapiganaji wa al-Shabaab ambalo linapania kuipindua serikali ya Somalia na kuanzisha utawala mpya, hutekeleza mashambulio aina hiyo.

Mwanamume aliyeshuhudia tukio hilo alisema magari saba na mikokoteni kadha iliharibiwa katika mlipuko huo.

“Damu ilitapakaa katika eneo lote la makutano ya barabara,” akasema mwanamume huyo ambaye aliomba jina lake libanwe.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Mwanavoliboli Mkenya Chemos anyakuliwa na Mouloudia nchini...

MUTUA: Wakenya walio ng’ambo wana haki ya kupiga kura