• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Mwanavoliboli Mkenya Chemos anyakuliwa na Mouloudia nchini Tunisia

Mwanavoliboli Mkenya Chemos anyakuliwa na Mouloudia nchini Tunisia

Na AGNES MAKHANDIA

MSHAMBULIAJI wa klabu ya voliboli ya Kenya Prisons, Michael Chemos amesajiliwa na klabu ya Mouloudia nchini Tunisia kwa kandarasi ya miezi sita.

Chemos ameratibiwa kuabiri ndege ya kuelekea Tunisia mnamo Oktoba 1 kabla ya msimu mpya wa ligi nchini humo kuanza mwezi huo huo.

Katika mahojiano mnamo Septemba 25 wakati wa dhifa ya mchana ya timu ya taifa ya wanaume ya Kenya maarufu Wafalme Spikers, iliyoandaliwa na Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF) kwa ushirikiano na Shirika la Kenya la Wanyamapori (KWS) mtaani Lang’ata jijini Nairobi, Chemos alisalia mwingi wa matumaini atafanya vyema katika klabu yake mpya.

“Sijawahi kushiriki ligi yoyote kaskazini mwa Afrika, lakini nina ari kuhusu safari hiyo mpya. Nafahamu klabu hiyo ilikamata nafasi ya nne ligini msimu uliopita na niko tayari kuisaidia kuimarisha matokeo yake msimu huu,” alisema.

“Njia ya pekee timu ya taifa inaweza kukuwa ni kuruhusu wachezaji zaidi kucheza voliboli ya malipo. Natoa changamoto kwa shirikisho letu pia liruhusu wachezaji kushiriki ligi kokote duniani kwa sababu mwishowe itakuwa na manufaa kwa timu yetu hapa nyumbani kupata matokeo mema. Natumai kupata mafunzo mengi niwezavyo nchini Tunisia na ninatumai ukuaji wangu utaonekana kupitia kazi yangu uwanjani,” aliongeza.

Chemos hapo awali alichezea Al Arabi nchini Qatar, Raiso Lomu na Joensu (Finland), Karamaras (Uturuki), Oita Miyoshi (Japan) na Hapoel Kfar Saba (Israel).

Yeye ni mchezaji wa pili kutoka Kenya kupata klabu ya kigeni mwaka 2021 baada ya mshambuliaji wa pembeni kulia wa GSU, Abiud Chirchir kunyakuliwa na Grand Nancy nchini Ufaransa mwezi Mei.

Dhifa hiyo ilikuwa ya kusherehekea Wafalme Spikers kukamilisha Kombe la Afrika katika nafasi ya tisa kati ya timu 16 zilizoshiriki nchini Rwanda majuma machache yaliyopita ambapo vijana wa kocha Gideon Tarus waliduwaza miamba Misri kwa seti 3-2 katika mojawapo ya mechi za makundi.

Naibu mwenyekiti wa KVF, Charles Nyaberi, ambaye aliandamana na maafisa wengine kutoka shirikisho hilo Mududa Waweru, Kenneth Tonui na Moses Mbuthia katika dhifa hiyo, alisema kuwa shirikisho hilo limejitolea kuendelea kusaidia timu hiyo.

“Matokeo ya Kombe la Afrika yanaonyesha kuwa tunaendelea kuwa wazuri katika mchezo huu. Tutaanzisha mpango utakaosaidia kikosi hiki kiwe pamoja kwa muda mrefu. Kimethibitisha kuwa kikipata usaidizi mzuri kinaweza kuwa tishio na hatuna budi ila kukisaidia,” alisema Nyaberi.

Kocha David Lung’aho, ambaye pamoja na Elisha Aliwa walisaidia Tarus nchini Rwanda, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kikosi hicho cha taifa wakati huu.

Nahodha Enock Mogeni alitaka wachezaji wenzake watie bidii mazoezini wanapojiunga na klabu zao kwa msimu mpya nchini Kenya unaotarajiwa kung’oa nanga mwezi Novemba.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Alaves wakomesha rekodi nzuri ya Atletico Madrid kwenye La...

Watu 7 wauawa katika shambulio la kigaidi Mogadishu