• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
WHO yatoa majina mapya kurejelea virusi vya corona

WHO yatoa majina mapya kurejelea virusi vya corona

Na MASHIRIKA

GENEVA, Uswisi

AINA za virusi vya Covid-19 zitakuwa zikitajwa kwa kutumia alfabeti za Kigiriki ili kuzuia unyanyapaa dhidi ya mataifa ambako virusi hivyo vilizuka kwa mara ya kwanza.

Hii ni kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumatatu.

Mfumo huo mpya vilevile unajumuisha virusi vipya hatari hasa aina nne kuu za virusi vinavyosambaa kwa sasa pamoja na virusi vilivyoibuka kutokana na wimbi la pili la mkurupuko, ambavyo vinachunguzwa.

“Majina hayo hayatachukua nafasi ya majina yaliyopo kwa sasa ya kisayansi lakini yananuiwa kusaidia katika mazungumzo ya umma,” alisema kiongozi wa idara ya kiufundi WHO, Maria Van Kerkhove.

Katika mfumo huo mpya, aina kuu za virusi vya corona zitakuwa zikitambulishwa kwa namna ifuatayo, virusi vya kwanza kuzuka Uingereza B.1.1.7 vitaitwa Alpha, virusi aina ya B.1.351 vilivyogunduliwa kwa mara ya kwanza Afrika Kusini, vitaitwa Beta, huku aina ya virusi vilivyozuka kwa mara ya kwanza Brazil P.1 vikiitwa Gamma.

Virusi vinavyohangaisha taifa la India vinavyojulikana kama B.1.617 vitagawanywa katika vitengo vidogo vidogo ambapo kitengo kikuu B.1.617.2 kitafahamika kama Delta.

Aina ya virusi vinavyofahamika kama B.1.617.1 vitaitwa Kappa.

“Leo hii WHO imetangaza mfumo mpya wa kutaja virusi vikuu vya Covid-19. Majina hayo yanatokana na alfabeti za Kigiriki ambavyo ni Alpha, Beta, Gamma, na kadhalika, hivyo kuyafanya rahisi kukumbukwa,” ilisema WHO kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Aidha, majina mengine mawili ya kisayansi yatatumiwa kwa kila aina ya virusi vinavyobadilikabadilika, huku majina mbalimbali ya kijiografia yakitumiwa kufafanua aina moja ya virusi. Kwa mfano, nchini Uingereza, virusi ambavyo mataifa mengine yamekuwa yakitaja kama Virusi vya Uingereza, aghalabu huitwa Virusi vya Kent.

Kent ni kaunti inayopatikana Kusini Mashariki mwa Uingereza, ambapo virusi hivyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza.

Majina yanayofuata orodha kama vile B.1.1.7.2 yataendelea kutumiwa katika nyanja za kisayansi kwa sababu yanasheheni maelezo muhimu kuhusu mabadiliko ya virusi.

“Japo yana faida zake, majina ya kisayansi yanaweza kuwa magumu kuyataja na kuyakumbuka na kuna hatari ya kuripotiwa kimakosa,”

“Kutokana na hilo, aghalabu watu hugeukia kutaja aina mbalimbali za virusi kutokana na mahali vilipozuka kwa mara ya kwanza, jambo ambalo ni la kinyanyapaa na kibaguzi,” ikaeleza WHO.

You can share this post!

Mbunge aitaka serikali ijenge shule zilizozama

Nani mkali? Kevin De Bruyne, Harry Kane na Ruben Dias kati...