• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Nani mkali? Kevin De Bruyne, Harry Kane na Ruben Dias kati ya wawaniaji wa taji la Mchezaji Bora wa Msimu wa 2020-21

Nani mkali? Kevin De Bruyne, Harry Kane na Ruben Dias kati ya wawaniaji wa taji la Mchezaji Bora wa Msimu wa 2020-21

Na MASHIRIKA

MASOGORA Kevin De Bruyne na Ruben Dias wa Manchester City ni miongoni mwa wanasoka ambao wameteuliwa kuwania taji la Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika msimu wa 2020-21.

Fowadi na nahodha wa Tottenham Hotspur, Harry Kane aliyeibuka mfungaji bora msimu huu, pia yuko katika orodha hiyo ya wawaniaji kwa pamoja na kiungo Bruno Fernandes wa Manchester United na fowadi Mohamed Salah wa Liverpool.

Mason Mount wa Chelsea, Tomas Soucek wa West Ham United na Jack Grealish wa Aston Villa wanakamilisha orodha hiyo ya wawaniaji.

Mkufunzi Pep Guardiola ameteuliwa kuwania taji la Kocha Bora wa Msimu wa 2020-21 na anapigiwa upatu wa kuibuka mshindi kutokana na matokeo bora yaliyosajiliwa na waajiri wake Man-City.

Guardiola aliyeongoza Man-City kutia kapuni taji la tatu la EPL katika kipindi cha misimu minne, atashindana na mkufunzi Marcelo Bielsa wa Leeds United, David Moyes wa West Ham United, Brendan Rodgers wa Leicester City na Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United.

Dias ambaye ni beki matata raia wa Ureno alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2020-21 na Chama cha Wanahabari wa Soka (FWA) mnamo Mei.

De Bruyne alitawazwa Mchezaji Bora wa Msimu wa 2019-20 huku Jurgen Klopp wa Liverpool akiibuka mshindi wa taji la Kocha Bora muhula huo.

Kane ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza, alijishindia ‘kiatu cha dhahabu’ msimu huu wa 2020-21 baada ya kufunga jumla ya mabao 23, moja nyuma ya Salah na matano zaidi kuliko Fernandes.

Kwa upande wake, Mount alisaidia Chelsea kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kutinga ndani ya orodha ya nne-bora kwenye msimamo wa jedwali la EPL. Soucek alichangia mafanikio ya West Ham kufuzu kwa soka ya Europa League huku Grealish akiongoza waajiri wake Villa kuambulia nafasi ya 11 katika msimu wao wa pili tangu warejee kunogesha soka ya EPL.

Mshindi wa kila kategoria anaamuliwa kupitia kura za umma kwenye tovuti ya EA Sports pamoja na kura 20 zitakazopigwa na manahodha wote wa vikosi vya EPL na wataalamu teule wa soka kutoka Uingereza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

WHO yatoa majina mapya kurejelea virusi vya corona

NGILA: Nchi za Afrika ziungane kujiendeleza kiteknolojia