• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Zelensky aashiria nia ya kutaka mazungumzo na Urusi

Zelensky aashiria nia ya kutaka mazungumzo na Urusi

KYIV, UKRAINE

RAIS wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameongeza juhudi za kidiplomasia za kuikabili Urusi kufuatia uvamizi wake dhidi ya taifa hilo.

Kiongozi huyo amekuwa akifanya mazungumzo na viongozi wa mataifa yenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiuchumi kama Amerika, Uturuki na Ufaransa, licha ya mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea katika eneo la mashariki.

Ijapokuwa Zelensky amekuwa akifanya mazungumzo na Rais Joe Biden wa Amerika, Emmanuel Macron wa Ufaransa na Recep Erdogan wa Uturuki tangu Urusi kuivamia Ukraine mnamo Februari, ni nadra kwake kufanya mazungumzo kama hayo kwa siku moja.

“Tunashirikiana pakubwa na washirika wetu,” akasema Zelensky, kwenye hotuba aliyotoa Jumapili usiku.

Aliongeza kuwa katika wiki kadhaa zijazo, anatarajia “matokeo muhimu” kutokana na vikao kadhaa vya kimataifa ambavyo vitaangazia hali ilivyo Ukraine.

Hapo jana Jumanne, Chansela wa Ujerumani, Olaf Scholz alifanya kikao cha mtandaoni na viongozi wa mataifa wanachama wa kundi la G7 na mawaziri wa mashauri ya kigeni kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU).

Kikao hicho kiliangazia vikwazo zaidi vitakavyowekwa kwa Urusi, utoaji zaidi wa silaha za vita kwa Ukraine kati ya masuala mengine.

Mashambulio ya Urusi dhidi ya taifa hilo yameharibu miundomsingi muhimu ya kuzalisha na kusambaza umeme, hali ambayo imewaacha mamilioni ya watu gizani, hasa msimu huu wa baridi.

Urusi imekuwa ikitumia droni na roketi kutekeleza mashambulio hayo.

Zelensky alisema amemshukuru sana Biden kwa msaada wake wa “kifedha na kijeshi” ambao Amerika imetoa kwake kufikia sasa.

Alisema pia waliangazia haja ya Ukraine kuwa na mfumo thabiti wa kulinda anga yake kwa usalama wa raia.

“Tunaishukuru Amerika pia kwa usaidizi ambao imekuwa ikitupa katika kurejesha huduma za umeme,” akasema.

Alisema Ukraine itashiriki kwenye mikutano itakayofuata ya kundi la G7.

Kwenye taarifa jana Jumanne, Ikulu ya White House ilisema kuwa Biden alisisitiza Amerika inafanya kila iwezalo kuisaidia Ukraine kulinda anga yake.

Zelensky alijadili masuala yayo hayo na marais Macron na Erdogan wa Ufaransa na Uturuki mtawalia.

Zelensky alitaja kikao chake na Macron kuwa “chenye manufaa sana” kwani kiliangazia “ulinzi, kawi, uchumi na diplomasia”.

Wakati huo huo, pia aliishukuru Uturuki kwa kuwapa makao maelfu ya watoto kutoka Ukraine na misaada ya mamia ya jenereta kufuatia mashambulio ya Urusi dhidi ya vituo vyake vya kuzalisha na kusambaza umeme.

Kiongozi huyo pia alisema walijadili uwezekano wa kupanua mpango wa kusafirisha nafaka, kufuatia kufunguliwa kwa bandari za Ukraine mnamo Julai.

Bandari hizo zilikuwa zimefungwa na Urusi kwa karibu miezi sita.

Uturuki ndiyo ilikuwa mpatanishi mkuu kwenye mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi, kwa usaidizi wa Umoja wa Mataifa (UN).

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaanzisha operesheni dhidi ya pombe haramu na dawa...

Kisima cha maji ya chumvi chageuka baraka kwa jamii

T L