• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Zuma alazwa hospitalini baada ya kuugua gerezani

Zuma alazwa hospitalini baada ya kuugua gerezani

Na MASHIRIKA

Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma anayetumikia hukumu jela kwa kudharau mahakama, amelazwa hospitalini nje ya gereza.

Kulingana na Idara ya Magereza ya Afrika Kusini, Zuma alilazwa kufanyiwa uchunguzi wa matibabu Ijumaa.

Zuma pia anakabiliwa na mashtaka 16 ya ufisadi alipokuwa makamu wa rais wa Afrika Kusini na kesi yake ilitarajiwa kuendelea wiki ijayo.

Mahakama ilimtaka afike kortini binafsi wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.Zuma anatumikia kifungo cha miezi 15 katika gereza la Estcourt Correctional Centre, jimbo la KwaZulu-Natal kwa kudharau mahakama.

Alihukumiwa kufungwa jela baada ya kukosa kufika kortini wakati wa kusikilizwa kwa kesi.Msemaji wa idara ya magereza Singabakho Nxumalo alisema kwamba rais huyo wa zamani anahitaji huduma za afya zinazohitaji kuhusika kwa idara ya afya ya jeshi.

“Hali imekuwa hivi tangu alipofikishwa katika gereza la Estcourt Correctional Centre,’ Nxumalo alisema.Alisema iliamuliwa alazwe hospitalini baada ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake gerezani.

“Baada ya uchunguzi wa kawaida wa afya iliamuliwa kwamba Zuma alazwe hospitalini,” alisema.

Idara hiyo ilisema kwamba afya ya wafungwa imehakikishwa chini ya sehemu 35(2) ya katiba.

Sehemu hii inapatia idara hiyo mamlaka ya kuhakikisha kwamba kila anayezuiliwa jela, akiwemo kila mfungwa aliyehukumiwa ana haki ya kuwa na mazingira ambayo ni ya utu ikiwemo mazoezi, lishe, vifaa vya kusoma, matibabu na malazi bora kwa gharama ya serikali.

Kulazwa hospitali kwa Zuma kulijiri saa chache baada ya Rais Ceril Ramaphosa kuondoa wizara ya ulinzi iliyokashifiwa kufuatia ghasia zilizozuka katika nchi hiyo kwa wiki tatu baada ya mtangulizi wake kufungwa jela.

Ramaphosa alifuta wizara hiyo kwenye mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ambayo pia alilenga kusafisha serikali yake kufuatia madai ya wizi wa mabilioni ya pesa zilizotengewa vita dhidi ya corona na ukosefu wa usalama.

Aliyekuwa waziri wa afya, Zweli Mkhize, alijiuzulu saa chache kabla ya Rais Ramaphosa kutangaza mabadiliko katika baraza la mawaziri ambapo alimteua Joe Phaahla kusimamia wizara hiyo.

Duru zilisema kwamba Zweli alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa angefutwa baada ya kuhusishwa na ufisadi kuhusiana na mabilioni ya corona.

Joe Phaahla aliyeteuliwa waziri mpya wa afya alikuwa naibu waziri katika wizara hiyo.Enoch Gondongwana aliteuliwa waziri wa fedha kuchukua nafasi ya Tito Mboweni ambaye aliomba aondolewe kutoka wadhifa huo.

Mboweni, aliyeteuliwa waziri wa fedha mwaka wa 2018, amesaidia kufufua uchumi wa Afrika Kusini ulioathiriwa vibaya na janga la Covid-19.

Kufuatia ghasia zilizokumba nchi hiyo kwa wiki tatu ambapo watu zaidi ya 200 waliuawa na mali ya mabilioni ya pesa kuharibiwa, uwezo wa maafisa wa usalama na ujasusi ulipigwa darubini.

Ramaphosa alitangaza kuwa atateua jopo la wataalamu kuchunguza maandalizi ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo kukabiliana na changamoto zikizuka.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Tubuni makavazi ya uanahabari kukuza...

Maandalizi ya kura ya maamuzi yashika kasi