• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Maandalizi ya kura ya maamuzi yashika kasi

Maandalizi ya kura ya maamuzi yashika kasi

Na BENSON MATHEKA

MAANDALIZI ya kura ya maamuzi ya marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), yanaendelea kushika kasi, huku waandalizi wa mchakato huo wakisubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa katika kesi wanayotaka ibatilishe uamuzi wa Mahakama ya Juu uliozima referenda kufanyika.

Majaji watano wa Mahakama Kuu walizima Mswada wa Kura ya Maamuzi wa BBI wakisema haukuwa wa kikatiba na wakaharamisha mchakato mzima ikiwemo kupiga marufuku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuushughulikia kwa vyovyote.

Wakiweka breki safari ya kubadilisha katiba ambayo ilianza na handisheki ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, majaji hao walisema kwamba Rais alikiuka katiba kwa kuanzisha mchakato wa kubadilisha katiba akiwa mamlakani.

Viongozi hao wawili wamekuwa wakisisitiza nia yao ya kukamilisha marekebisho ya katiba kupitia BBI kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Majaji saba wa Mahakama ya Rufaa wanatarajiwa kutoa uamuzi wao wakati wowote kuanzia Agosti 20, hatua ambayo ingezuia kura ya maamuzi kufanya iwapo watakubaliana na waliokata rufaa na kubatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu kwa sababu ya muda.

Ili kuhakikisha muda hautakuwa kizingiti kwa BBI ikizingatiwa umebaki mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, washirika wa Rais Kenyatta na Bw Odinga katika Bunge, wameanza mikakati ya kurekebisha sheria kufupisha muda wa hatua zinnazohitajika kufanikisha kura ya maamuzi.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuondoa hitaji, wabunge wajadili mswada huo na kuidhinisha swali litakaloshirikishwa kwenye referenda.

Washirika wa vinara hao, kupitia kamati ya bunge kuhusu sheria, wanataka muda wa kuamua kesi ya kupinga matokeo ya kura ya maamuzi upunguzwe kutoka miezi sita hadi siku 21.

Kwenye mswada huo, washirika wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wanataka muda wa IEBC kuandaa referenda usizidi siku 36 badala ya 90 inayoruhusiwa kuchukua kikatiba.

Hatua ya wabunge hao inajiri mwezi mmoja baada ya IEBC kutangaza tenda za kununua karatasi za kura ya maamuzi na uchaguzi mkuu hatua iliyochukuliwa na wengi kama ya kujiandaa kwa referenda.

Kulingana na mwenyekiti wa IEBC, tume ilitangaza tenda hizo kwa kuwa mojawapo ya majukumu yake ni kuandaa kura ya maamuzi.

Mswada huo wa kupunguza muda wa hatua za kuandaa referenda ulianza kushughulikiwa bungeni Alhamisi siku ambayo Rais Uhuru Kenyatta alijaza nafasi nne za makamishna wa IEBC zilizokuwa wazi.

Miongoni mwa sababu za Mahakama Kuu kuzima IEBC kushughulikia Mswada wa IEBC ilikuwa kwamba tume hiyo haikuwa imeundwa kikamilifu ilipokagua saini za kuunga mswada wa marekebisho ya katiba wa BBI.

Ili kuepuka kucheleweshwa kwa matangazo ya mwisho ya kura ya maamuzi, wabunge wanapendekeza kuwa tume iyachapishe ndani ya siku moja baada ya referenda kufanyika.

Ikiwa mapendekezo ya wabunge yatapitishwa, marekebisho ya katiba kupitia BBI yatakuwa tayari Desemba mwaka huu. Mswada huo unapendekeza muda wa kuwasilisha rufaa kuhusu kesi za kupinga matokeo ya kura ya maamuzi hadi siku saba kutoka siku 30.

Rufaa ikiwasilishwa, iwe ikisikilizwa na kuamuliwa ndani ya siku 21 badala ya siku 30.Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakisisitiza kwamba marekebisho ya katiba yaliyopendekezwa katika BBI ni muhimu kwa kuunganisha nchi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Odinga amekuwa akisema kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu ulioharamisha marekebisho ulipumzisha BBI lakini haukuiua.

“Mahakama ilipeleka BBI kwenye mapumziko. Reggae itarudi kwa kishindo kwa kuwa tunataka kuunganisha nchi hii,” Bw Odinga amekuwa akisema.

Naibu Rais William Ruto na washirika wake ambao wanajitambulisha na chama cha United Democratic Alliance (UDA) wamekuwa wakidai BBI ilikufa ilipozimwa na Mahakama kwa kuwa katiba hairuhusu referenda ifanyike mwaka moja. kabla ya uchaguzi.

  • Tags

You can share this post!

Zuma alazwa hospitalini baada ya kuugua gerezani

Hatari wakazi ‘wakisusia’ madaraja ya barabara kuu