• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
SHINA LA UHAI: Kansa ya matiti: Wanaume msiipuze!

SHINA LA UHAI: Kansa ya matiti: Wanaume msiipuze!

Na PAULINE ONGAJI

ALIPOGUNDUA kwamba alikuwa na maradhi ya kansa ya matiti mwaka wa 2010, David Thuo Mwanyura, 61, kutoka eneo la Ndeiya, Kaunti ya Kiambu, alipigwa na butwaa kwani hakudhania mwanamume anaweza kuugua ugonjwa huu.

Ni suala ambalo pia liliwashangaza madaktari kiasi kwamba iliwachukua muda kutambua kwa kweli ilikuwa kansa ya matiti.

“Mwanzoni walidhani kwamba ulikuwa tu uvimbe ambapo hawakuuchukulia kwa umakini. Mwaka wa 2013 – miaka mitatu baadaye – ndipo waligundua kwamba kwa kweli nilikuwa na awamu ya pili ya kansa na titi langu la kushoto lilikuwa limeathirika,” aeleza.

Ni suala lililomsababisha kufanyiwa upasuaji, ambapo titi lake la kushoto lililondolewa mwaka huo huo, na papo kwa papo akaanza matibabu.

“Matibabu pia yalihusisha kufanyiwa awamu nane za tibakemia na tisa za tibaredio,” anasema.

Kwa bahati nzuri kufikia 2014, Bw Mwanyura alikuwa amekamilisha matibabu na hata madaktari kuthibitisha kwamba ugonjwa huo ulikuwa umetoweka.

David Thuo Mwanyura, manusura wa kansa ya matiti wakati wa mahojiano nyumbani kwake Ndeiya, Kaunti ya Kiambu mnamo Oktoba 14, 2021. Picha/ Evans Habil

Lakini safari yake haikuwa rahisi huku akikumbwa na changamoto za kifedha, zilizomzuia hata kuwapeleka wanawe katika shule ya upili.

“Mimi ni mkulima mdogo na sikuwa na mbinu nyingine ya mapato. Wakati huo, nusura niuze shamba na ng’ombe wangu, lakini kwa bahati nzuri rafiki yangu alinitambulisha kwa mdhamini katika hospitali moja jijini Nairobi aliyenisaidia kugharimia matibabu,” aeleza.

Ni takriban mwongo mmoja sasa tangu agundulike kuugua maradhi haya, na chunguzi kadhaa za kimatibabu zimethibitisha kwamba kansa hiyo ilishatoweka, ila anaendelea kutumia dawa.

Japo anashukuru kuwa miongoni mwa baadhi ya wanaobahatika kushinda vita dhidi ya maradhi haya, anakumbuka alipokuwa mgonjwa jinsi alivyokumbwa na woga wa kujitokeza waziwazi.

“Nilikumbwa na wasiwasi wa kuieleza jamii kuhusu hali yangu kwani nilihofia kwamba ningetengwa. Aidha, niliona kana kwamba ningepoteza fahari yangu kama mwanamume kwani nilikuwa naugua maradhi ambayo wengi wanayatambua kama ugonjwa wa wanawake,” asimulia.

Shirika la Afya Duniani – WHO – linaonyesha kwamba kansa ya matiti ni nadra mno miongoni mwa wanaume ikilinganishwa na wanawake.

Lakini licha ya hayo, wataalamu wa kiafya wanahoji kwamba kamwe haipaswi kupuuzwa.

“Kwa wanaume, kuna uwezekano wa kansa hii kuenea kwa kasi katika sehemu zingine mwilini kwani tishu za matiti yao ni ndogo zikilinganishwa na wanawake, miongoni mwao huja kwa mshindo na ni rahisi sana kusambaa mapema,” aeleza Dkt Miriam Mutebi, daktari wa upasuaji wa kansa ya matiti katika hospitali ya Aga Khan, jijini Nairobi.

Kulingana na WHO, nchini Amerika ambapo uwezo wa utambuzi, viwango vya elimu na ufahamu kuhusu maradhi haya miongoni mwa wanaume viko juu, mmoja kati ya wagonjwa 100 wa kansa ya matiti, ni wanaume.

Aidha, mwaka 2020, ilikadiriwa kwamba takriban wanaume 2,620 watagundulika na maradhi ya kansa ya matiti nchini humo, huku kati yao takriban 520 wakiaga dunia.

Hapa Kenya hakuna takwimu kamili zinazoonyesha idadi ya wanaume wanaougua kansa ya matiti.

Dkt Mutebi anasema, mojawapo ya sababu kuu ni kwamba wengi hawajitokezi na kutangaza hali zao, huku wakihofia kunyanyapaliwa.

“Tatizo ni kwamba watu wanapohofia kujitokeza na kutafuta usaidizi, kuna uwezekano wa maradhi haya kusambaa na hivyo kuwa changamoto kutibu,” anasema.

Anaongeza kwamba, sawa na kwa wanawake, ishara za kansa ya matiti kwa wanaume huonyesha dalili zilezile.

“Hii ni pamoja na uvimbe usio na uchungu kwenye tishu ya matiti, mabadiliko ya rangi kwenye ngozi inayozingira titi lililoathirika, sehemu hiyo kubadilika rangi na kuwa nyekundu na ngozi kuonekana kana kwamba ina magamba. Pia, kuna mabadiliko ya chuchu kuwa nyekundu au kuingia ndani ya ngozi,” aeleza.

Shirika la WHO lasema kwamba ili kuongeza uwezekano wa mgonjwa kupona na hivyo kuzuia vifo, utambuzi wa mapema ni muhimu.

“Kuna mikakati miwili ya utambuzi mapema wa kansa ya matiti. Moja yazo ni utambuzi wa mapema na hivyo kuanzisha tiba haraka iwezekanavyo. Kisha kuna uchunguzi ili kutambua kansa kabla ya ishara kujitokeza (screening), ambapo ala za utaratibu huu zinahusisha kukaguliwa titi na mhudumu wa afya (mammography), vile vile mhusika kujikagua mwenyewe,” afafanua Dkt Mutebi.

Kadhalika anasema mbinu hizi zimesaidia wanawake wengi kutambua mapema maradhi haya na hivyo kuyadhibiti.

“Lakini kwa upande wa wanaume, huenda ikawa vigumu kwani sio wengi walio tayari kukubali kufanyiwa taratibu hizi,” aeleza.

Kulingana na Jane Frances Angalia, mwanaharakati dhidi ya maradhi ya kansa ya matiti, changamoto kuu imekuwa kuwarai wanaume kufanyiwa uchunguzi wa matiti, ili kutambua mapema, na hivyo kuanza matibabu kabla ya kuenea katika sehemu zingine mwilini.

“Wanaume wengi wanaogopa kujitokeza kwani wanachukulia maradhi kuwa ugonjwa wa wanawake,” aeleza Bi Angalia.

Kulingana na Dkt Mutebi, kuna mambo yanayoongeza hatari ya kukumbwa na kansa ya matiti.

“Miongoni mwa wanaume mambo yanayoongeza hatari ya maradhi haya ni umri, ambapo waathiriwa wa kansa ya matiti huwa katika miaka ya sitini,” asema.

Pia historia ya maradhi haya katika familia huchangia uwezekano wa kuugua.

“Hii inamaanisha kwamba ikiwa una jamaa wa karibu ambaye amewahi kuugua kansa ya matiti, basi una uwezekano mkubwa wa kukumbwa na maradhi haya,” anaeleza.

“Katika mataifa ya magharibi, imekadiriwa kwamba 10% ya wanaume wanaougua kansa ya matiti wana historia ya kifamilia ya kansa ya matiti au ya ovari. Pia, hali kama vile BRCA2 mutation and Klinefelter’s syndrome (XXY) zinaongeza hatari, japo changio la masuala haya ya kijenetiki barani Afrika, hayatambuliki,” aeleza Dkt Mutebi.

Anasema pia kwamba kuna sababu zingine zinazosababisha mabadiliko ya matiti kwa wanaume kama vile gynaecomastia (ambapo matiti yanakuwa makubwa kutokana na sababu kadha wa kadha), kumaanisha kwamba ili kuwa salama mabadiliko haya yanapaswa kukaguliwa na daktari.

Kulingana naye, kuna masuala yanayoweza badilishwa na mengine haiwezekani.

“Kwa mfano haiwezekani kwa mtu kubadili historia ya familia yake, au aepuke uzee – baadhi ya masuala yanayochangia pakubwa hatari ya aina hii ya kansa – lakini kuna mambo ambayo waweza badilisha kupunguza hatari hii,” afafanua.

Mbinu mwafaka asema ni kubadili mtindo wa maisha, kula chakula cha kudumisha afya na kufanya mazoezi.

“Tiba huhusisha upasuaji wa kuondoa tishu za titi lilioathirika, lakini pia kuna matibabu mengine kama vile tibakemia na tibaredio kuambatana na hali ya mwathiriwa,” aongeza.

Mtaalamu huyu anasema kwamba waathiriwa wa kiume wa kansa ya matiti huenda wakahitajika kupokea matibabu yanayolenga homoni za kike mwilini mwao, suala ambalo huwatia wengi aibu.

“Hii inamaanisha kwamba wanahitaji usaidizi hata zaidi katika safari hii ya matibabu,” asisitiza.

Kulingana na Dkt. Martin Ajujo, daktari wa upasuaji wa kurekebisha sehemu za mwili zilizoharibika, katika huduma ya Nairobi Metropolitan Services (NMS), hili ni dhihirisho tosha la umuhimu wa ushauri nasaha kwenye matibabu ya kansa.

“Kwa waathiriwa wengi matibabu haya huwa makali sana, na pia wazo la kupoteza sehemu ya mwili huwasumbua sana,” aeleza.

Kwa upande wake, Bi Angalia asema, shughuli za uhamasishaji kuhusu maradhi haya miongoni mwa wanaume zinapaswa kushika kasi. Ni kauli anayokubaliana nayo Dkt Mutebi.

“Wanaume wanahitaji kuhamasishwa kuhusu jinsi ya kukagua sehemu hii ya mwili, ili iwe kawaida kwao kufanya hivyo bila aibu. Hii itachangia pakubwa utambuzi wa mapema wa maradhi haya, na hivyo kuokoa maisha,” asisitiza.

You can share this post!

Kocha Unai Emery aongoza Villarreal kupiga Young Boys...

Lewandowski aongoza Bayern kuzamisha Benfica na kufuzu kwa...

T L