• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Mfugaji stadi wa majibwa wenye pato la kuridhisha

Mfugaji stadi wa majibwa wenye pato la kuridhisha

NA SAMMY WAWERU

KATIKA kijiji cha Rukubi, Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu na kilomita chache kutoka soko maarufu la Wangige ndiko Oscar Ragui Ngime huendeleza ufugaji wa majibwa.

Ikiwa ni biashara iliyokumbatiwa na watu wachache nchini, mfugaji huyu hujamiisha kupata vilebu (wana wa mbwa).

Ana uzoefu wa zaidi ya miaka saba, hususan majibwa ya ulinzi.

Kulingana naye, alilelewa katika mazingira yenye majibwa jambo ambalo lilimchochea kuwaenzi.

“Baba anapenda mbwa, na tangu nikiwa mdogo kiumri alikuwa akiwafuga. Nadhani jeni za mapenzi ya dhati kwa wanyama hawa wa nyumbani zilihamia kwangu,” aelezea.

Alianza na mbwa mmoja wa kike aina ya German shepherd, anayefichua alimgharimu mtaji wa Sh40, 000.

Licha ya ari yake, Ragui anasema hakuwa amefanya utafiti wa kutosha kuhusu ufugaji wa mbwa.

“Alipohitaji dume kwa bahati mbaya akajamiiana na mbwa wa kawaida. Matokeo hayakuwa ya kuridhisha, nilipata watoto chotara,” adokeza.

Chotara, ni mnyama au binadamu anayezaliwa baada ya spishi zenye rangi au hulka tofauti kujamiiana.

Mbwa huzaa kati ya siku 58 – 68, baada ya kujamiiana.

“Wengi hawapendi mbwa waliopatikana kwa kujamiisha mbwa wa spishi tofauti. Hata baada ya kugharamika malisho na chanjo, niliamua kupeana watoto waliozaliwa,” asema.

Alianza upya safari, kufuatia utafiti wa kina aliofanya. Ragui sasa ni mfugaji hodari wa mbwa, wa kupigiwa upatu.

Mbali na German shepherd, hufuga spishi aina ya Havanese na Japanese Spitz, shabaha yake ikiwa ni kupata wana kuuzia wanaofuga mbwa kwa minajili ya ulinzi.

Ana makazi matatu ya wanyama hao wa nyumbani, kila moja ikiwa na ukubwa wa futi tisa urefu na upana futi nne na nusu.

Kila makazi yamegawanywa mara mbili, wanakolala – kizimba ambacho kimeezekwa kwa mabati na kimeinuliwa juu kiasi kuzuia maji ya mvua kuingia.

Pili, cha mapumziko na kujiburudisha, ambacho hakijaezekwa.

Kimeundwa kwa mbao na nyaya. “Mara nyingi utawapata wakijituliza kupunga hewa mwanana na miale ya jua,” Ragui asema.

Yalimgharimu Sh100, 000 kuyatengeneza.

Wanapotazama sura geni, mazingira huhinikiza mbweko, maumbile na ukubwa wao ukiogofya, hulka za ujasiri ambazo anasema wateja wake huridhia kwa sababu ya ulinzi mkali.

Kiwango cha usafi katika makazi ya majibwa yake, ni cha hadhi ya juu.

Wakati wa mahojiano, aliambia Akilimali kwamba huyang’arisha kila siku na pia kuyapulizia majibwa dawa aghalabu mara tatu kwa wiki ili kuua kupe, viroboto na vijidudu.

“Huwaosha mara mbili kila juma na kuchana manyoya yao,” asema.

Aidha, mbwa huzaa mwaka mmoja na nusu baada ya kuzaliwa.

“Ni muhimu mfugaji afanye utafiti wa kina na wa kutosha kujua dume bora. Asitumie aliyezaliwa kupitia anaofuga, ili kuepusha mjamiiano wa familia moja,” ashauri Simon Wagura, mtaalamu wa masuala ya mifugo.

Kulingana na mdau huyu, mifugo wa ‘mama’ na ‘baba’ mmoja wanapotungana ujauzito, bridi inayozaliwa huwa hafifu, inayokodolewa macho na changamoto nyingi za ukuaji.

“Endapo unataka bridi bora na ya hadhi ya juu, tumia madume ya wafugaji wengine,” ahimiza.

Ragui hujamiisha kila baada ya miezi mitatu. Kwa sasa ana jumla ya majibwa 7, mmoja akiwa mjamzito.

Ingawa amefanikiwa kuboresha mradi wake, analalamikia gharama ya juu ya malisho, hasa chakula cha madukani.

Huwalisha mara moja kwa siku. “Huwapa mchele wa mbwa, Omena na miguu na vichwa vya kuku. Wanahitaji vyakula vyenye virutubisho vya kutosha, na kiwango cha juu cha Protini,” Ragui aelezea.

“Aliyezaa, hulishwa mara mbili kwa siku. Pia, anapaswa kupewa chakula maalum aina ya pellets, kuongeza kiwango cha maziwa.”

Anasema si ajabu mbwa mmoja atumie gharama ya Sh500 kila juma katika chakula, mjamzito na aliyezaa bei yake ikiwa mara dufu.

Ragui ni makini sana katika kufuatilia hali ya mbwa wake, hususan matibabu na chanjo.

Anasema kulea mwana hadi afikishe umri wa kuingia sokoni, gharama ya chanjo haipungui Sh3, 500.

Anataja kero ya maradhi kama vile Parvo virus, kuwa mojawapo ya changamoto kuu katika ufugaji wa mbwa.

Yote tisa, kumi wanapofikisha umri kuwageuza kuwa pesa Ragui hutabasamu akielekea benkini.

Huku akiwa amesajili ufugaji wake kupitia asasi husika, anafichua kilebu mwenye umri wa miezi mitatu hapungui Sh70,000.

“Kuna bridi za zaidi ya Sh250,000.”

Ni mwasisi wa apu inayotafutia wafugaji na mavetinari wateja. Maarufu kama Bobbi, Ragui anakiri hahangaiki kupata soko.

Apu hiyo ya kidijitali, yenye zaidi ya wateja 1,000 waliojiandikisha kufikia sasa pia huunganisha wafugaji na wauzaji wa chakula.

  • Tags

You can share this post!

TUJIFUNZE UKULIMA: Wakulima wahamasishwe jinsi ya kukabili...

Wakulima wahimizwa wasivune makadamia kabla hayajakomaa

T L