• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 11:13 AM
TUJIFUNZE UKULIMA: Wakulima wahamasishwe jinsi ya kukabili mabadiliko ya tabianchi

TUJIFUNZE UKULIMA: Wakulima wahamasishwe jinsi ya kukabili mabadiliko ya tabianchi

Na SAMMY WAWERU

ATHARI za mabadiliko ya tabia nchi zinapotajwa, wakulima Simon Mungai na dadake Wairimu Mungai wanazielewa bayana.

Wakiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika ukuzaji wa matunda aina ya plamu, wanakiri kiwango cha mazao kimeendelea kupungua kwa kiwango kikubwa.

Wanaendeleza kilimo cha matunda hayo katika Kaunti ya Nyandarua.

“Mambo yalianza kuenda kombo 1997, baada ya Kenya kushuhudia mvua kubwa ya mafuriko,” Simon asema.

Walirithi miplamu 100, na athari za mabadiliko ya tabianchi zimewachochea kuipunguza hadi 40.

Uamuzi huo unatokana na kupungua kwa kiwango cha mvua, na pia ratiba kubadilika, mabadiliko yaliyosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ni upungufu wa maji ambao umechangia kiwango cha mazao kushuka, kutoka wastani wa kilo 70 kila mplamu hadi chini ya kilo 35.

Licha ya athari za mabadiliko ya hali ya anga, Simon na Wairimu wanasisitiza hawataasi kilimo cha plamu.

“Upanzi wa miti unasaidia kukabiliana na athari tunazopitia,” Simon asema.

Ni hatua ya busara anayohoji ikiigwa na wakulima wenza kote nchini, uwezekano upo kurejesha hadhi ya mazingira ya zamani.

Tafiti za muungano wa Alliance for A Green Revolution in Africa (Agra), zinaonyesha shughuli za kilimo zimechangia asilimia 30 ya mabadiliko ya tabianchi.

Ukataji wa miti na uharibifu wa misitu ndio unaoongoza.

Athari zake zimebadilisha misimu ya upanzi na mavuno.

“Tuhakikishe tunachofanya kama wakulima hakitachangia kuendeleza mabadiliko ya tabianchi,” ashauri Dkt Agnes Kalibata, Rais wa Agra.

“Ukuaji wa Bara letu la Afrika unaegemea wakulima.”

Kulingana na Shirikisho la Kitaifa la Wakulima (KNFF), athari za mabadiliko ya hali ya anga zitaangaziwa endapo wakulima wataungana.

“Ikiwa una ekari 10 kuza idadi ya miti 10, 000…Isitoshe, tupande miti kwa kuambatana na umri wetu. Mfano, iwapo una miaka 20 panda idadi sawa na umri huo,” ahimiza Ruth Maraba, kutoka KNFF.

Machi 2019, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kwamba serikali inafanya kila iwezalo kuafikia kigezo cha asilimia 10 ya misitu nchini kufikia mwaka huu, 2022.

You can share this post!

Mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri kilimo cha plamu...

Mfugaji stadi wa majibwa wenye pato la kuridhisha

T L