• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
‘Sekta za kilimo, ufugaji ziimarishwe vijana wapate kazi’

‘Sekta za kilimo, ufugaji ziimarishwe vijana wapate kazi’

Na SAMMY WAWERU

JOYCE Gichana na dadake pacha mzawa Ruth Wakonyo, wenye umri wa miaka 24 wamekuwa wakisaidia wazazi wao kutafutia soko mazao wanayozalisha eneo la Ruai, Kaunti ya Nairobi.

Wazazi wao ni wakulima hodari wa nyanya, pilipili mboga za rangi tofauti, vitunguu, matango na celery-kiungo kinachofanana na dhania.

Aidha, huendeleza kilimo-biashara katika shamba lenye ukubwa wa ekari 30.

“Tumekuwa katika kitengo cha mauzo,” Joyce adokeza.

Duka lao, Forujo Fresh Veggies likiwa miongoni mwa maduka yaliyofunguliwa yakiwa ya kwanza, wanadada hao wanaridhia mikakati ya Nairobi Farmers Market (NFM), soko lililoko Kiambu Road, Runda, kiungani mwa jiji, katika kusaidia wakulima kufikia wateja.

Wateja nao, wanapata mwanya wa kipekee kutangamana na wakulima wazalishaji, ana kwa ana, kwa sababu NFM inamilikiwa na wakulima.

Kabla soko hilo kufunguliwa mwishoni mwa mwaka uliopita, na kuzinduliwa rasmi mapema 2021, wanasema mazao yao yote walikuwa wakiyaelekeza katika masoko mbalimbali Nairobi, Kiambu na viunga vyake.

“Haikuwa rahisi kuwahi bei bora, ikizingatiwa kuwa mengi ya masoko yametekwa nyara na mawakala,” Ruth asema.

Kwa sasa, idadi kubwa ya mazao shambani mwao yanafikia walaji kupitia duka lao.

“Yanayosalia baada ya kuhakikisha tuna stoki ya kutosha, tunayasambaza katika masoko mengine,” Joyce aelezea.

Wafanyabiashara hao wachanga ni wasomi. Joyce ana Shahada ya Digrii katika Masuala ya Uhusiano mwema wa Umma (Public Relations) na Saikolokia, naye Ruth amesomea Digrii ya Uhusiano wa Kimataifa na kuipiga jeki kwa Uhusiano mwema wa Umma.

Kwa mujibu wa masimulizi, baada ya kuhitimu chuoni ilikuwa mithili ya kupanda mchongoma kupata ajira.

“Tulituma maombi chungu nzima kuomba kazi katika kampuni na mashirika tofauti, ila hatujawahi kupata mwaliko wa ajira,” Ruth asema.

Hata ingawa hatma ya jitihada zao masomoni ni Mungu tu anayejua, mabinti hao wanasema wanaridhia kuwa katika sekta na mtandao wa uzalishaji na usambazaji vyakula.

Uzoefu na tajiriba waliyozoa, Joyce na Ruth wanahisi sekta ya kilimo ndiyo suluhu kwa mahangaiko ya vijana nchini, hasa ikiwa serikali na wadauhusika wataipiga jeki kikamilifu.

Mamia na maelefu ya vijana wanaendelea kufuzu vyuoni kwa kozi na taaluma mbalimbali, wakijiunga na wenzao, wengi wakisaga meno kwa kukosa ajira.

Safari ya kuboresha Forujo Fresh Veggies hata hivyo haijakuwa rahisi.

“Nyakati zingine, hususan mazao mbichi yanayokosa wanunuzi huishia kuharibika. Isitoshe, mengine huongezea wateja,” wanasema.

Jeff Mundia, meneja wa soko hilo pia ni mmoja wa wanaomiliki duka.

The Farm Outlet, huuza mazao ya shambani ya familia yake, yanayokuzwa katika Kaunti ya Tharaka Nithi.

Aidha, hulima matunda aina ya mapapai, karakara, ndizi, avokado na matikitimaji. Hali kadhalika, hukuza malenge, nyanya, vitunguu na miwa.

“Ili kukwepa kero ya mazao kuharibika na kuoza, huyaongeza thamani kwa kuunda sharubati ya matunda na viungo vinginevyo,” Jeff afichua.

Wana mashine za shughuli hiyo, ikiwemo ya kukama juisi kutoka kwenye miwa.

Fairtrade Africa (FTA), shirika linalounganisha wakulima na kampuni wanachama wake kwa soko la mazao katika nchi za kigeni, linasema bidhaa zilizoongezwa thamani zina ushindani mkubwa.

Aidha, linahoji chini ya asilimia 10 ya mazao linalouza ndiyo huongezwa thamani.

“Mazao yaliyoungezwa thamani, mapato yanakuwa hadi mara tatu,”anasema Kate Nkatha, Mkurugenzi Mkuu wa Mauzo FTA, akihimiza wakulima kukumbatia mfumo wa uongezaji thamani.

Muungano huo una zaidi ya wakulima milioni 1.8 kote ulimwenguni, 450, 000 wakitoka Kenya.

Nkatha anasema FTA ina soko tayari Ujerumani, Uholanzi, Canada, Finland, Ufaransa, Ubelgiji, Luxembourg, Italia, Australia, Norway, Uswidi, Uswisi na Uingereza, kati ya mataifa mengine.

Kwa sasa, inasaka mianya kuingia Korea, China na Japan.

Kenya huuza majanichai, kahawa na maua kwa wingi katika masoko ya kigeni.

“Hata hivyo, tumeona mazao mabichi ya shambani yasiyochukua muda mrefu kuzalisha, mazao ya kuku na ng’ombe na pia bidhaa zilizoongezwa thamani, yana mianya bora ya soko,” Kate anasema.

Huku Nairobi Farmers Market ikijikakamua kuhakikisha wateja wanapata mazao bora, uongozi wa soko hilo unasema uko tayari kushirikiana na wadauhusika wengine katika sekta pana ya kilimo.

Julai 2021, soko hilo liliandaa hafla, Kiambu County Harvest Festival ambapo wakulima kutoka kaunti hiyo walipata jukwaa kutangamana na wateja na kuuza mazao.

Ilifadhiliwa na Kenya Climate Innovation Centre (KCIC), kupitia muungano wa Bara Uropa (EU) na Wizara ya Masuala ya Kigeni Denmark.

Gavana wa Kiambu, James Nyoro ndiye alizindua tamasha hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa mishikaki ya maini

Mna siku 7 kumshtaki Mwendwa, korti yaagiza

T L