• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mna siku 7 kumshtaki Mwendwa, korti yaagiza

Mna siku 7 kumshtaki Mwendwa, korti yaagiza

RICHARD MUNGUTI na JOHN ASHIHUNDU

MAHAKAMA imempa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji siku saba amfungulie mashtaka ya ubadhirifu wa pesa za umma Rais wa Shirikisho la Kandanda Nchini (FKK) Nick Mwendwa.

Na wakati huo huo, DPP alipata pigo kubwa mahakama ilipokataa kumzuilia Bw Mwendwa kwa siku 14 ikisema “ombi hilo halina mashiko kisheria kwa vile wachunguzi hawakueleza namba ya mahojiano wanayotaka kufanya.”

Akitoa uamuzi kuhusu ombi la kuruhusu polisi wamzuilie Bw Mwendwa kwa siku 14 kukamilisha uchunguzi wa ubadhirifu wa Sh38 milioni, hakimu mkuu Wandia Nyamu alisema DPP hakuwasilisha sababu tosha za kumzuilia kinara huyo wa kandanda nchini.

Hakimu alisema endapo DPP hatawasilisha mashtaka dhidi ya Mwendwa, faili ya kumchunguza yapasa kufungwa na kumruhusu aendelee na kazi yake.

Bi Nyamu alisema DPP hakuwasilisha cheti chochote cha mashtaka kuonyesha kiasi cha pesa anachodaiwa kutumia vibaya.

Mahakama ilisema polisi walitangaza Mwendwa amefuja zaidi ya Sh513 milioni lakini kortini walisema ni Sh38 milioni zilizotolewa na watu wasioidhinishwa kuendeleza masuala ya kifedha ya FKF.

Bi Nyamu alisema polisi walimharibia jina na sifa Mwendwa kwa madai hayo yasiyo na msingi.

Mahakama ilisema ilikuwa makosa kwa polisi kumtia nguvuni Mwendwa bila kufanya uchunguzi wa kutosha.

“Polisi walikosea kumzuilia Mwendwa kabla ya kufanya uchunguzi wa kutosha,” alisema Bi Nyamu.

Hakimu alisema ni bayana polisi walimshika Mwendwa ndopo watafute ushahidi.Mahakama iliamuru uchunguzi uendelee Mwendwa akiwa nje kwa dhamana ya pesa tasilimu ya Sh4 milioni.

Mahakama iliamuru Mwendwa aendelee kuwa nje kwa dhamana na iwapo polisi wanataka kumhoji wako huru kuwasiliana naye.

Aliagizwa asiwavuruge mashahidi ili ajiepushe na bughudha zaidi.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 25, 2021 kwa maagizo zaidi.

“Hutatembelea afisi za FKF ama kuongea na wafanyakazi wako hadi Polisi watakapokamilisha uchunguzi,” akaambiwa Mwendwa.

You can share this post!

‘Sekta za kilimo, ufugaji ziimarishwe vijana wapate...

Vituo vya pombe vyaongeza uzembe Juja

T L