• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
AKILIMALI: Hivi viazi vitamu ni spesheli kwa njia moja muhimu: havina sukari!

AKILIMALI: Hivi viazi vitamu ni spesheli kwa njia moja muhimu: havina sukari!

Na CHARLES ONGADI

NI katika kijiji cha Majengo, Kanamai, Kaunti ya Kilifi ambako Tina Anderson, 28, anafanya kilimo cha aina tofauti ya viazi ambavyo ni nadra kupatikana Pwani.

Viazi hivi havina ladha ya sukari na ndani ni rangi ya manjano na wala si mviringo, umbo lake ni mfano wa muhogo vile. “Mbegu yake nilipatiwa na rafiki yangu aliyetoka nchini India ili nifanyie majaribio kama inaweza kufanya vyema nchini na matokeo yake nimeyaona baada ya kipindi kifupi,” asema Bi Tina Anderson wakati wa mahojiano na Akilimali majuzi.

Bila kusita, Tina anasema aliamua kuifanyia majaribio aina hii ya viazi na baada ya kipindi cha miezi mitano aligundua kwamba vinafanya vyema hasa katika udongo mweusi na ulio mwororo.

Kulingana na Tina, kabla ya kujitosa mzimamzima katika kilimo cha aina hii ya viazi aliamua kufanya utafiti wa kina na kugundua kwamba viazi hivi vinapendwa sana na watu walio na mahitaji spesheli ya mlo.

Tina anafichua kwamba mwanzoni baadhi ya wateja wake walisusia viazi hivi wakidai havina ladha ya utamu kwa walaji.Lakini baadaye alianza kuwapata aina spesheli ya wateja wakiwa ni wanaogua ugonjwa wa kisukari ambao mara nyingi hushauriwa kutotumia vyakula vilivyo na sukari.

Ni baada ya hapo ndipo mkulima huyu aliamua kuvalia njuga kilimo cha aina hii ya viazi ambavyo vimeanza kuvutia wateja wengi ndani na nje ya Kilifi.

Kwa mujibu wa Tina, wateja wake wengi ni wa jamii ya Kieshia (Wahindi) wanaonunua kwa wingi na kuwauzia wafanyibiashara wenzao katika maduka makubwa (supermarkets) yaliyo mijini.

Mbali na hao, wafanyabiashara wa kawaida eneo la Majengo Kanamai wameanza kugundua umuhimu wa viazi hivi wakinunua kwa wingi kuchuuza kwa wateja wao hasa wasiopendelea kula vyakula vilivyo na sukari.

Denis Ngumbao, mkazi wa Kanamai, Kilifi, anasema amekuwa mteja sugu wa Tina mara baada ya kugundua umuhimu wa viazi hivi.

“Nilishauriwa na daktari kutotumia vyakula vilivyo na sukari na viazi hivi vimekuwa ndilo kimbilio langu kila siku kwa sababu navitumia kila asubuhi badala ya mkate,” asema Ngumbao aliyefika shambani kununua bidhaa hii.

Tina anasema kwamba ili kuvuna kwa wingi aina hii ya viazi shambani, mkulima anahitajika kufuata kwa uangalifu sheria na masharti.

Tina anasema kilimo cha aina hii ya viazi hufanya vyema kipindi cha mvua kutokana na kwamba wadudu hatari hawapati nafasi kuvamia mizizi wala matawi kutokana na hali ya unyevu unyevu.

Aidha, anaongeza kwamba amefaulu kila msimu katika kilimo hiki kutokana na kuwa na kisima cha maji anachokitumia kipindi cha kiangazi.

Tina anasema kwa mkulima wa viazi hivi kupata mavuno mazuri na yenye faida, mkulima anastahili kuandaa vyema shamba lake kwa kulainisha mchanga kisha baadaye kunyunyizia mbolea ya samadi kabla ya kufanya upanzi wake.

Huchukua kipindi cha miezi mitano kuwa tayari kwa mavuno na kulingana na Tina ana uwezo wa kuvuna takribani kilo 25 kwa siku katika shamba lake la robo ekari.

Tina Anderson akivuna viazi spesheli katika shamba lake eneo la Majengo Kanamai kaunti ya Kilifi. wakulima wengi Pwani wameifumbia macho kilimo hiki pengine kwa kutojua faida yake. Picha/Charles Ongadi

Kilo moja anawauzia wateja wake kwa kati ya Sh150 hadi Sh160 kulingana na hali ya biashara katika soko kuu la Kongowea, Mombasa.

Anasema changamoto hutokea kipindi cha kiangazi wakati wadudu waharibifu huwa wengi na hivyo kulazimika kutumia kiasi kikubwa cha hela kununua dawa za kuwaangamiza.

“Mkulima anapokosa kuwa makini kipindi cha kiangazi wadudu hawa huweza kuvamia mizizi ama kuvamia viazi na kutoboatoboa ndani na kumletea mkulima hasara kubwa,” ashauri Tina.

Ni miaka miwili tangu Tina ajitose katika kilimo hiki na tayari ameona faida yake kubwa ikiwa kwa sasa analenga kupanua zaidi kilimo hiki.

“Msimu ujao nitaongeza nusu ekari nikilenga kuimarisha zaidi mapato yangu,” asema mama huyu aliyevutiwa na shughuli za kilimo akiwa angali mchanga.

Anawashauri akina mama Pwani kukumbatia zaidi kilimo kwa kuwa ndio uti wa mgongo wa taifa letu hasa baada ya kudorora kwa shughuli za utalii Pwani.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Hongera Uhuru na Raila kukubali...

Polo 2 wakabana demu akijifungua