• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
AKILIMALI: Ufugaji samaki kwa madema waleta kipato

AKILIMALI: Ufugaji samaki kwa madema waleta kipato

Na RICHARD MAOSI

TANGU mwaka wa 2010, kumekuwa na ongezeko la hitaji la samaki aina ya tilapia kwenye soko la kitaifa na lile la kimataifa.

Hata hivyo, changamoto kubwa inayowakumba wafugaji ni ukosefu wa sera za kudhibiti shughuli za uvuvi kwenye maziwa makuu kama vile Ziwa Victoria na Baringo ambayo yanaamika kuwa kitovu cha samaki wengi nchini.

Ni kwa sababu hiyo baadhi ya wavuvi na wafugaji samaki, katika ufuo wa Ziwa Victoria eneo la Mbita Kaunti ya Homabay wameunda madema maalum ya kufugia samaki (fish cages)kulinda tilapia, ambao huenda wakaangamia siku za mbeleni.

Akizungumza na Akilimali, Exodus Nyabuku ambaye anaendesha biashara ya kufuga samaki kwa madema, anasema madema hayo yamekuwa yakimsaidia kufuga samaki ambao, huwavuna kila baada ya miezi minane, na kusafirishwa katika masoko ya nje ambayo ni kaunti za Nairobi, Mombasa, Kisumu Nakuru na Uasin-Gishu.

Nyabuku anasema alianzisha mradi huu mnamo 2015 baada ya kuhitimu stashahada ya uhandisi, lakini alipokosa ajira akaamua kujiajiri.

Alipochoka kusaka vibarua aliamua kufanya biashara ya kufuga samaki ambapo alikuwa akifuga samaki kwenye vidimbwi ila kipato chake kilichukua muda mrefu kuimarika.

“Mnamo 2016, nilitembelea eneo la Mbita, Kaunti ya Homabay ambapo nilijifunza kutoka kundi moja la vijana, namna ya kufuga samaki kwenye madema,” anaeleza.

Baada ya hapo, aliamua kutafuta mkopo wa Sh50,000 na kununua vyuma, chandarua na kuajiri vibarua ambapo anaungama kuwa ufugaji samaki kwa madema ni bora kuliko kwenye vidimbwi.

Vile vile, anasema kuwa ili mfugaji wa samaki aweze kufikia samaki wake ndani ya dema atahitaji kununua mashua au kukodi wakati wa kuzivua na kusafirisha windo lake.

Kulingana naye wanunuzi wengi wanapenda kula samaki wa kienyeji badala ya wale wa kigeni kwa gharama ya kadri ambayo si ghali mno.

“Mara ya kwanza nilinunua vidagaa 5,000 na kutumbukiza ndani ya maji na kulisha kwa kipindi cha miezi mitano hivi kabla ya kuzaana ambapo idadi ilifikia zaidi ya 9,000,” anaeleza.

Kwanza gharama ya kulisha tilapia huwa ni ndogo na ubora wake huwa ni wa hali ya juu, ikizingatiwa kuwa wanakulia kwenye mazingira yao ya asilia, anasema.

“Ingawa dema la samaki mara nyingi huwa pembezoni mwa ziwa mkulima hulazimika kuchimba kima cha mita 10 hivi ili kufikia oksijeni ambayo ni kiungo muhimu katika ukuaji wa samaki na lishe,” anaeleza.

Pili, kwa kutumia vyuma samaki huzungushiwa uzio kwa kutumia chandarua chenye vishimo vidogo ili kulinda vidagaa vsisombwe na maji wala kuhepa kutoka kwa madema.

Wavuvi katika eneo la Mbita, Kaunti ya Homa Bay wakiendelea kuvua samaki kutoka kwenye aina spesheli ya nyumba ya samaki inayofahamika kama madema yaani fish cages. Picha/ Richard Maosi

Mfugaji huyo anaeleza kuwa lishe ndani ya ziwa hazitoshelezi mahitaji ya samaki wanaofugwa na yeye wakati mwingi huchanganya lishe za viwandani, zenye madini ya vitamini na protini ili kutoa muda kwa samaki wake kukomaa haraka.

Kulingana na Nyabuku madema huzalisha hadi tani 40,000 ya samaki kila mwaka katika Ziwa Victoria, huku tani nyingine 99,000 zikizalishwa ndani ya ziwa

Anasema kuwa ufugaji wa samaki ndani ya madema pembezoni mwa Ziwa Victoria ni bora kuliko ufugaji kwa vidimbwi kwani sehemu nyingi nchini zimekuwa zikiathirika na ukame wa mara kwa mara. Hali hiyo ni tofauti na mazingira ya ziwani ambapo si rahisi kiwango cha maji kushuka.

Isitoshe anasema ndani ya madema kuna mzunguko mzuri wa hewa safi ya oksijeni, lishe asilia ambapo samaki huwa wanakulia kwenye mazingira ya kawaida.

Anawashauri wafanyibiashara ambao wanalenga kuingilia ufugaji wa samaki, kukumbatia mfumo huu wa madema, ili kuvuna samaki ambao wanakubalika sokoni.

“Mara nyingi ninawashauri wafugaji wenzangu kuhakikisha wanaelewa madini ambayo hupatikana ndani ya lishe ya samaki, endapo wanalenga kufikia soko la kimataifa,” anasema.

Katika biashara hii anasema yeye huweza kutengeneza faida ya hadi Sh18,000 kwa wiki. Hitaji la soko kila wiki huwa angalau samaki 6,000, akiuza kwa kati ya Sh350 hadi Sh600 ingawaje wale wadogo huuzwa hata Sh200.

Hata hivyo, anasema kuwa bei ya samaki hubadilika kulingana na msimu, na wanunuzi wake wengi ni maduka ya jumla katika Kaunti za Nairobi na Kisumu.

Mfugaji huyu pia anaeleza kuwa si kila wakati ambapo huwa ana kiasi cha samaki kinachohitajika sokoni, na hivyo hulazimika kununua kutoka kwa wafugaji wenzake.

Mbali na biashara hiyo ya ufugaji samali, Nyabuku pia hufunza vijana mbinu hii ili waweze kujiajiri na kukabili soko la samaki wenye ubora duni.

“Kuna nafasi kubwa ya ajira katika sekta hii, kwani sio wengi ambao wamepata ufahamu wa mbinu hii mpya hususan mijini ambapo hakuna maziwa,” anafichua.

“Hii ni njia mojawapo ya kuinua kipato kwa akina mama na vijana kutoka mashinani ambao wanategemea uvuvi kukidhi mahitaji yao ya kila siku.”

Hata hivyo, Nyabuku anasema kuwa soko la kimataifa limekuwa likiharibu soko la samaki aina ya tilapia humu nchini, ambapo samaki ghushi wamekuwa wakiuzwa sokoni kwa bei nafuu.

Anasema kuwa jambo hili litamkandamiza mfanyibiashara wa humu nchini ambaye amekuwa akitumia jasho lake kuzalisha samaki ambao wana ubora kiafya.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Ubaguzi na ukabila umekithiri...

AKILIMALI: Anakula jasho lake kwa kilimo cha mkunde na...