• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
AKILIMALI: Anakula jasho lake kwa kilimo cha mkunde na mabenda

AKILIMALI: Anakula jasho lake kwa kilimo cha mkunde na mabenda

Na CHARLES ONGADI

KIPENDACHO roho ni dawa kama walivyosema wavyele ndivyo hali ilivyo kwa Alphonse Mwanyika, mkulima stadi wa mabenda na mboga za mkunde katika Kaunti ya Mombasa.

Baada ya kukamilisha masomo yake ya upili miaka kadhaa iliyopita, wazazi wake walimpeleka kwa mafunzo ya udereva.

Na baada ya miezi michache alikuwa amefuzu na kufaulu kuajiriwa katika kampuni moja ya uchukuzi bandarini, Mombasa.

Hata hivyo, moyoni mwake, Mwanyika alipenda sana kilimo kilichomvutia tangu utotoni alipokuwa na mazoea ya kuandamana na wazazi wake shambani wakiwa kwao katika Kaunti ya Taita Taveta.

“Nilijifunza udereva kutokana na ombi la wazazi wangu ila moyoni nilitaka kuwa mkulima stadi kutokana na faida niliyoanza kuona nikiwa mchanga,” asema Mwanyika katika mahojiano na Akilimali majuzi.

Lakini baada ya kufanya kazi ya udereva kwa kipindi cha zaidi ya miaka 30 akisafiri nchi mbali mbali kama Tanzania, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan Kusini miongoni mwa mataifa mengine, hatimaye Mwanyika aliamua kuwacha kwa hiari kazi hiyo na kujitosa katika kilimo biashara miaka miwili iliyopita.

Kulingana naye, kipindi akifanya kazi ya udereva alijiwekea hela ambazo baadaye alibadilisha kuwa mtaji wa kuanzisha kilimo chake.

Kwanza alihakikisha amenunua shamba lake la takribani ekari moja eneo la Zowerani, Bamburi Kaunti ya Mombasa na kuligawanya sehemu ya kuishi na kufanyia kilimo kisha kuchimba kisima cha maji.

“Sikutaka kufanya kilimo changu msimu wa mvua pekee ila wakati wowote ule ili kuweza kujiongezea mapato muda wote,” aeleza.

Hata hivyo, kabla ya kujitosa katika kilimo biashara, Mwanyika alifanya utafiti katika mazingara aliyokuwepo na kilimo ambacho kingemletea faida baada ya kipindi kifupi.

Alphonse Mwanyika akivuna mabenda shambani mwake katika kijiji cha Zoerani, Bamburi kaunti ndogo ya Kisauni, Mombasa. Picha/ Charles Ongadi

Ni hapo alipofikia uamuzi wa kuanzisha kilimo cha mabenda na mboga za mkunde zinazopendwa sana na wakazi wa Kisauni na Pwani kwa jumla.

“Unapata kwamba mboga za mkunde na mabenda zinaliwa sana na Wapwani wengi hasa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani,” anasema.

Anaeleza kuwa kwa mabenda kukomaa na kuwa tayari kuvunwa huchukua takribani mwezi mmoja pekee wakati mboga za mkunde zikichukua siku 18.

Katika shamba lake la nusu ekari, Mwanyika aliamua kuligawanya kwa sehemu mbili, moja akapanda mabenda na sehemu iliyosalia akiweka mboga za mkunde.

Hata hivyo, Mwanyika asema ili kupata mavuno mazuri mkulima anastahili kuandaa barabara shamba lake kwa kuondoa magugu na wadudu waharibifu kisha kuchanganya vyema mbolea shambani.

Anaongeza kwamba kamwe hatumii aina yoyote ya kemikali kuongezea rotuba shambani ila samadi ambayo haina madhara kwa mimea yake na hata kwa walaji wa mboga na mabenda yake.

Na kama wasemavyo wa zama kwamba kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza, wateja wa Mwanyika huja wenyewe shambani kununua mazao yake.

Huuza fungu moja la mabenda sita kwa Sh10 kwa wafanyabiashara na rejareja ni mabenda 10 kwa Sh10.

Wakati fungu moja la mboga zikienda kwa Sh30 ama Sh60 kwa wateja wa kawaida na wafanyibiashara mtawalia.

Mwanyika anafichulia Akilimali kwamba kwa siku ana uwezo wa kuvuna kiasi cha kati ya Sh1,500 hadi Sh2,000.

Anasema kwa mwezi mmoja ana uwezo kuweka faida ya kati ya Sh40,000 hadi Sh45,00 mara baada ya kuondoa matumizi mengineyo.

Na ili kuhakiksha wateja wake wanapata mboga na mabenda kila wanapohitaji, Mwanyika anahakikisha anapanda mimea yake kwa wakati tofauti.

Pia anasema kutokana na faida ambayo amekuwa akipata, ananuia kupanda aina ya mboga za mkunde zinazong’olewa kabisa ifikapo wakati wa mavuno ili kuwa na mboga freshi kila baada ya mavuno.

“Nanuia kuboresha zaidi mboga zangu kwa kupanda mkunde ambao ukishakomaa naung’oa kabisa na kupanda mwingine mpya ili kudumisha ubora wa mboga kila wakati badala ya kuzivuna kwa kipindi kirefu,” afafanua.

Mkulima huyu anaeleza kuwa hajutii uamuzi wake wa kuwacha kazi yake ya udereva na anacholenga kwa sasa ni kupanua zaidi kilimo chake kwa kuongeza mabenda na mboga za kienyeji kama mchunga na mnavu zinazopendwa na wenyeji eneo hili.

Anakiri kilimo kinalipa hasa maeneo ya mijini kutokana na kwamba ni wachache walio na uwezo wa kumiliki mashamba.

“Kilimo ni kazi nzuri wala haina presha kwa sababu mkulima anajipanga na kuelewa anachohitajika kufanya kila wakati na wala haina stori ya kufutwa kazi,” asema Mwanyika.

Anawashauri wenye mashamba jimbo la Pwani kutumia vyema nafasi walizo nazo kuzalisha chakula kwa faida yao badala ya kupoteza muda wakisaka kazi ya kuajiriwa ambazo kwa sasa ni haba.

You can share this post!

AKILIMALI: Ufugaji samaki kwa madema waleta kipato

AKILIMALI: Usanii wake wa kutumia penseli umemjengea jina