• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Amos Rono sasa atangaza kuvunjilia mbali harusi na Nelly shutuma zikikolea

Amos Rono sasa atangaza kuvunjilia mbali harusi na Nelly shutuma zikikolea

FRIDAH OKACHI, VITALIS KIMTAI NA CHARLES WASONGA

HARUSI iliyokumbwa na utata katika Kaunti ya Bomet kati ya Amos Rono na Nelly Chepkoech sasa haitafanyika tena.

Hii ni baada ya Bw Rono kutangaza kuwa harusi hiyo, iliyokuwa imekatizwa kwa njia ya kutatanisha, haitafanyika na kwamba amekatiza uhusiano na Bi Chepkoech.

Alisema amechukua hatua hiyo kutokana na presha kutoka “sehemu mbalimbali” na sababu zingine ambazo hatuwezi kutaja hapa kwani sheria hairuhusu.

Hata hivyo, imeibuka kuwa tofauti kati ya Bw Rono na Bi Chepkoech ilichochewa zaidi na madai yaliyotolewa kupitia mitandao ya kijamii ndani ya siku mbili zilizopita na hatua ya jamaa na marafiki kuingilia mipango ya harusi yao.

“Nimemwachilia. Namtakia mema katika maisha yake ya baadaye na sina kisasi naye au watu wa familia yake. Baada ya kutafakari kwa kina na kufanya mashauriano, nimeamua kusalia bila mke kwa wakati huu,” Bw Rono akasema Jumapili jioni, akiandamana na watu wachache wa familia yake.

Harusi kati ya Rono na Chepkoech ilifutiliwa Alhamisi ilhali ilipangiwa kufanyika Jumamosi iliyopita.

Hatua hiyo imeibua joto kufuatia kuibuka kwa madai yasiyothibitishwa kuhusu sababu zilizochangia kuchukuliwa kwa hatua hiyo.

Baadhi ya madai yamewekwa kama siri na pande husika na hutolewa tu faraghani, hali ambayo imeendeleza uvumi potovu kuhusu harusi hiyo.

“Nimelia na kutokwa na machozi mengi kabla ya kufikia uamuzi wa kukatiza uhusiano wangu na Bi Chepkoech kabisa. Uhusiano huo haungenisaidia kama kiongozi wa vijana kanisani. Nimevunjwa moyo zaidi,” Bw Rono akaambia Taifa Leo, kwenye mahojiano Jumapili jioni.

Kauli yake ilikinzana kabisa na ile iliyotolewa na Bi Chepkoech saa chache kabla. Alikana madai ya kukatiza harusi hiyo,  ilivyodaiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Bi Chepkeoch alielezea matumaini kuwa angefunga ndoa na Bw Rono na kuanzisha familia.

“Tulishauriwa na Kanisa tuahirishe tarehe ya harusi kwani muda wa matumizi ya leseni ya ndoa unadumu hadi Februari mwaka ujao,” Bi Chepkoech akasema.

Alishikilia kuwa madai yaliyokuwa yakienezwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba yeye ndiye alikatiza harusi hiyo ni uwongo.

Aidha, imebainika kuwa Rono na Chepkoech wamekuwa wakichumbiana kwa muda wa mwaka mmoja na wamekuwa wakipanga harusi hiyo kwa pamoja kwa muda wa miezi miwili iliyopita.

Walikuwa wamepitia hatua zote hitajika kisheria na Kanisani.

Tangazo la Bw Rono kukatiza uhusiano na Bi Chepkoech lilijiri wakati ambapo Pasta Clement Chalulot alisema kuwa familia ya Bwana Harusi na Bi Harusi zinafanya mazungumzo kwa lengo la kuweka tarehe nyingine ya harusi.

“Familia yangu sasa haimtaki Chepkoech. Kulingana na yale ambayo yamefanyika ndoa hiyo imetibuka na hatuna kinyongo na familia yake,” Bi Sarah Nyige, mamake Bw Rono, akasema.

“Tulikuwa tumejiandaa kwa harusi. Tulikuwa tumetayarisha kila kitu. Lakini tangazo la kuahirishwa kwa harusi lilijiri kuchelewa. Tango hilo lilituathiri kisaikolojia,” Bi Nyige akasema.

Lakini Bi Chepkoech alishikilia kuwa sio yeye aliyesababisha kuahirishwa kwa harusi hiyo.

“Nimeshangazwa na madai kwamba nimefutilia mbali harusi na kutoweka ilhali niko hapa nyumbani na wazazi wangu. Nimekuwa nikisubiri kwa hamu harusi hiyo,” Bi Chepkoech, 23, akasema.

Alikuwa ameandamana na babake ambaye ni Kasisi Charles Koskei wa Kanisa la AGC, katika kijiji cha Chebirbelek, Sotik kaunti ya Bomet.

Bi Chepkoech alidai kuwa aliitwa na viongozi wa kanisa pamoja na Bw Rono na wakaarifiwa kuwa harusi hiyo ingeahirishwa kutokana na “sababu za kiufundi.”

“Tulipopashwa habari kuhusu kuahirishwa kwa harusi hiyo, sote (Chepkoech na Rono) tulibubujikwa na machozi lakini hatungefanya lolote kuhusu suala hilo. Niko tayari kwa siku hiyo kubwa tarehe nyingine ikiwekwa,” Bi Chepkoech akasema.

Hakuwa na na habari kuhusu tangazo, la kuvunja moyo, ambalo mpenzi wake alikuwa akipanga kutoa saa chache baadaye.

Inadaiwa kuwa tangazo kuhusu kuahirishwa kwa harusi lilitolewa na viongozi wa kanisa katika afisi za kanisa la African Gospel (AGC) eneo la Tenwek katika uwepo wa jamaa na marafiki wa familia hizo mbili.

“Harusi ingeendelea Jumamosi. Lakini niliitwa na mkurugenzi wa kanisa letu eneo hilo na akaniambia kwa maharusi hao walifaa kufanyiwa ushauri nasaha kwa sababu wamechumbiana kwa muda usiozidi miezi sita,” akasema Kasisi Koskei, akithibitisha kuwa alihudhuria mkutano ambapo tangazo hilo lilitolewa.

“Nimelipwa ng’ombe watano kama mahari pamoja na pesa kulingana na desturi. Mungu akipenda harusi hiyo itafanyika Februari au Aprili mwaka ujao,” Kasisi Koskei akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Kasisi huyo alipuuzilia mbali madai yaliyokuwa yakienezwa mitandaoni kwamba bintiye alikatiza harusi hiyo na kutoroka nyumbani.

“Watu wengine wamekuwa wakitoa madai katika mitandao ya kijamii kwamba binti yangu ametoweka. Hii ni licha ya kwamba tuko naye hapa na sote tunashangazwa na madai hayo ya kuvunja moyo,” akaeleza.

Lakini Bw Rono ana mipango gani siku za usoni baada ya nafasi yake ya kupata mke kutumbukia nyongo?

Je, ataanzisha juhudi za kumtafuta msichana mwingine wa kufanya naye pingu za maisha?

“Nimeamua kutulia kabla ya kupiga hatua nyingine. Bila shaka uamuzi huoa hautajiri hivi karibuni. Sharti nipate uponyaji, lazima niwe katika hali ambapo ninaweza kufanya maamuzi yenye busara ili nisijipate katika hali sawa na hii au hata mbaya zaidi,” Rono akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano.

Lakini aliongeza haraka kwamba: “Ningependa kuthibitisha kuwa nilimpenda zaidi Chepkoech na nilimwamini. Lakini pia nafahamu kuwa kile ambacho hakijapangiwa kutimia, hakitafanyika.”

“Tangazo la kuahirishwa kwa harusi lilipotolewa nilikuwa nimenunua mavazi maalum kwa ajili ya sherehe hiyo. Nilikuwa nimelipa pesa katika saluni moja mjini Bomet ambako Chepkoech angetengenezwa nywele na kucha, kati ya matayarisho mengine mengi yaliyogharimu pesa,” Bw Rono akasema.

Hema kadha zilikuwa zimetundikwa nyumbani kwao katika kijiji cha Kapsoiyo, wadi ya Silibwet, eneo bunge la Bomet ya Kati.

“Ng’ombe angechinjwa siku hiyo ili wageni wetu wafurahie,” akasema huku akizingirwa na watu wa familia ambao hawakutaka wanahabari wamuulize maswali mengine.

Wao ndio waliamua maswali ambayo Rono angejibu, ishara kwamba kulikuwa na mengi kuhusiana na harusi hiyo ambayo umma haukuhitajika kujua.

Ilidaiwa kuwa Sh300,000 zilikusanywa kugharamia harusi hiyo lakini ni Sh50,000 zilikuwa zimetumika wakati harusi hiyo ilisitishwa Alhamisi.

Aidha, iliibuka kuwa familia hizo mbili (ya Rono na ile ya Chepkoech) hazijakutana tangu stori hiyo ilipolipuka kwenye mitandao ya kijamii Ijumaa jioni.

  • Tags

You can share this post!

Siasa: Ukambani na Meru nao pia wasuka muungano mpya

Barobaro aliyemfuata shugamami kwake nyumbani atumiwa...

T L