• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Anapenda upishi, sasa ana kiwanda cha kupika pilipili

Anapenda upishi, sasa ana kiwanda cha kupika pilipili

NA SAMMY WAWERU

KENYA ilipokumbwa na virusi vya corona, ambavyo kwa sasa ni janga la kimataifa, Njoki Muriuki ni miongoni mwa mamia, maelfu na mamilioni ya Wakenya waliopoteza ajira.

Amesomea taaluma ya masuala ya usafiri (travel specialist), ambapo alikuwa akitafutia abiria wa ndege vyeti vya kuabiri, ndani na nje ya nchi.

“Biashara ziliposambaratika, singekaa bila kufanya kazi hivyo basi sikuwa na budi ila kutafuta njia mbadala kujiendeleza kimaisha na kukithi familia yangu,” asema mama huyu mkwasi wa ucheshi.

Njoki anapenda mapishi, na wazo likamjia kugeuza kipaji hicho kuwa chanzo cha mapato.Ni wazo analoridhia kuwa msingi na nguzo ya Kijo’s Garden, kampuni inayoongeza thamani mazao mabichi ya shambani.Husindika (process) pilipili hoho – zile kali, kwa kutumia viungo kama ndimu, tangawizi, vitunguu saumu, asali na mafuta ya canola.

“Mimi hutengeneza chilli paste kwa kutumia viungo asilia, haina viungio (additives) wala vihifadhi vyovyote vyenye kemikali,” mjasirimali huyu aelezea.

Anaiambia Akilimali kwamba, kabla kuingilia biashara anayoendeleza kwanza alipata mafunzo kupitia Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Nchini (KIRDI).

Huosha na kuchambua viungo anavyotumia, baadhi anavikamua juisi, kuvipondaponda-kusaga, anavichanganya na kuvipika kwa pamoja.“Natumia maabara ya KIRDI kwa sababu sijamudu kununua vifaa vinavyohitajika,” adokeza.

Mbali na vifaa vya taasisi hiyo, vingine anavyotumia ni grainda ya jikoni, chombo cha kuchanganya kwa kutumia nguvu za umeme (blender) na kipimajoto.Baada ya kusindika, huchoma (pasteurize) kuondoa vijidudu kwenye chilli paste, anapakia na kuhakikisha vipakio havina mwanya kuruhusu hewa kuingia, kisha anahifadhi kwenye jokofu.

“Jokofuni, bila kufungua bidhaa ninazounda zinadumu hadi miezi minane mfululizo. Zinapofunguliwa, na kuhifadhiwa kwenye friji zinadumu majuma manane,” akafafanua wakati wa mahojiano.

Kipimo cha gramu 250 anauza Sh550, bei ya rejareja.Chilli paste ya mfanyabiashara huyu imegawanywa kwa makundi matatu; yenye utamu japo chachu (sweet chilli), uchachu wa kadri (mild chilli) na moto – chachu zaidi (hot chilli).

Aidha, bidhaa zake zimeidhinishwa na Kebs. “Kijo’s Garden ina nembo ya Kenya na chini ya miaka 10 ijayo, itavuma Bara Afrika na ulimwengu kwa jumla,” asisitiza.

Ana karibu wakulima 800 wanaomsambazia viungo anavyotumia, hasa kutoka maeneo ya Pwani, Kajiado na Ukambani.

“Licha ya kunifaa kimapato, ni mradi unaolenga kuinua wakulima,” Njoki na ambaye ni afisa mkuu mtendaji asema.

“Kwa muda mrefu, wakulima hususan wa mazao mabichi yanayodumu muda mfupi wamekuwa wakihangaishwa na mawakala,” anaelezea, akihoji shabaha yake ni kuwanasua kutoka kwa kero ya minyororo hiyo.

Wakulima wakiendelea kulalamikia kukandamizwa na mabroka, Katibu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki – Kenya, Dkt Kevit Desai anasema huku asilimia 50 ya viwanda ikitegemea sekta ya kilimo, mikakati kabambe inapaswa kuwekwa kuiimarisha.

“Soko la mazao na bidhaa za kilimo litanogeshwa kwa kupiga jeki wakulima na kutathmini kwa kina suala la viwanda – kuongeza thamani, ili pia kuwahi masoko ya nje ya nchi,” Dkt Desai ahimiza.

Kwa upande wake Njoki, hatua ya kushirikisha wakulima moja kwa moja, mbali na kuwaondolea mahangaiko yanayochangiwa na mawakala, anasema inampa fursa ya kipekee kupata mazao bora.

“Hutembelea mashamba yao na kukagua wanavyoyazalisha ili kuhakikisha bidhaa ninazotengeneza zinafika mezani zikiwa salama,” afafanua, akisisitiza huwa makini sana na pembejeo na mifumo ya zaraa waliyokumbatia.

Ana maduka na matawi kusambaza chilli paste katika maeneo kama Karen, ABC-Nairobi, Lenana Road, kati ya mengineyo.Licha ya mafanikio yake chini ya kipindi cha miaka miwili, mwasisi huyu wa Kijo’s Gardens anasema haijakuwa mteremko, ikizingatiwa kuwa anategemea maabara ya KIRDI ambapo hutozwa ada.

“Changamoto nyingine ni kupata wakulima wa kutosha kunisambazia viungo mfululizo,” asema.

Kauli hiyo inaashiria ana upungufu wa mazao anayohitaji, hivyo basi ni jukumu la wakulima wanaoyazalisha kumakinika na kujituma shambani kuzalisha kwa wingi.Hutumia tovuti ya Ongoza, mitandao ya Facebook na Instagram kutafutia bidhaa zake soko.

  • Tags

You can share this post!

Michenza kitega uchumi tosha kwa mwalimu mstaafu

Ukuzaji miche unahitaji mpanzi awe makini kufaulu

T L