• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Ukuzaji miche unahitaji mpanzi awe makini kufaulu

Ukuzaji miche unahitaji mpanzi awe makini kufaulu

NA MWANDISHI WETU

NICK Ontiso, 26, alisomea taaluma ya zaraa katika Chuo cha Kiufundi cha Eldoret.

Hata hivyo, kabla hajahafili, aliona mwanya katika shughuli ya uoteshaji wa mbegu, ambapo watu wengi walikuwa wakiinunua miche kutoka mbali.

“Nilianzisha Nikitech mwaka 2017, baada ya kumaliza masomo ya chuoni. Nilianza kwa kukuza pilipili mboga, na watu wengi walikuwa wakiniuliza jinsi ya kufanya ili mimea hiyo ikue vizuri. Hapo ndipo nilipoona kuwa, kulikuwa na mwanya katika uoteshaji wa mbegu. Kwa hivyo, nilikuwa nikiuza miche ya pilipili mboga sana,” asimulia Ontiso, ambaye alifuzu chuoni mwaka wa 2018.

Hata hivyo, alianza kuzitumia trei spesheli mwaka 2019, na habari kuhusu shughuli yake zikaenea.

“Kwanza haikufanya vizuri; nilijaribu mara tatu. Nikaanza kuingia kwa YouTube kupata mafunzo Nilianza na pilipili mboga ambazo huwa hazioti kwa urahisi. Nilifeli mara ya kwanza ambapo nilipoteza miche 4,000, nikafeli mara ya pili na ya tatu. Sikuwa nimejua kuwa kuna chembe za kumbi za nazi coco peats ambazo hutumika,” asema, akiongeza kuwa kumbi hizo huwa hazina magonjwa na husaidia mno uotaji wa mbegu.

“Kinachotufanya kuzitumia ni kwa sababu hazina magonjwa na haziathiriwi na wadudu. Halafu zina nafasi ya kuingiza hewa na ukimwaga maji, kuna nafasi ya maji kupenya. Pia, huruhusu miche kukua kwa usawa na zinafanya mizizi ishikilie kwa mchanga na miche iking’olewa, hung’oka na mchanga,” anaeleza.

“Niliachana na kumbi za nazi nikatumia peat moss zilizokuwa zikiuzwa na Amiran. Peat moss huwa ziko tayari kwa matumizi na zina madini kidogo si kama coco peats. Nikatumia kwa muda, lakini wakati wa corona, bei ikapanda kutoka Sh5,000 hadi Sh7,800 kwa kilo 50, ikawa changamoto. Nikaanza kutumia tena coco peats kwa sababu kampuni kubwa huzitumia.”

Kwa sasa, mkulima huyo huziotesha mbegu kwa kutumia vivungulio viwili, ambapo kandokando ameweka neti.“Kivungulio kimoja ni mita 6 kwa 10, na kingine ni mita 8 kwa 15 na tumejijengea kwa sababu shamba letu lina fundi,” afichua Ontiso.

“Huzinunua mbegu kutoka mjini Kisii. Hukuza miche ya pilipili mboga, spinachi, Ethiopian kales (kanzera), nyanya aina ya cherry na nyanya za kawaida, na mbegu zote tunazoziotesha ni za haibridi peke yake,” aongeza mkulima huyo, ambaye huendesha shughuli hiyo katika eneo la Kibirigo, Kaunti ya Nyamira.

Anasema kuwa, anaweza kuziotesha mbegu zake na kutangaza mitandaoni na wateja huenda kwake na kuinunua miche. Aidha, mteja anaweza kumpelekea mbegu zake aziotesha kwa niaba ya mteja mwenyewe, na kumtoza ada za huduma.

“Tunamwoteshea kwa muda wa siku 21 au 28, na siku zikipita, tunamtoza ada zaidi ya ile tulizoagana ya Sh300 kila siku kwa sababu kuna wafanyakazi wanaomwagia maji. Tukinunua mbegu zetu za nyanya Zara F1, huwa tunauza mche mmoja kwa Sh4, lakini kama mteja amezileta mbegu zake, huwa tunamtoza Sh1.50 kila mmoja,” asema Ontiso.

Mkulima huyo huuza miche ya sukumawiki kwa Sh2, kabichi Sh2, na kwa nyanya, huwa kuna aina tofauti. Miche inayokuzwa kwa vivungulio huuzwa kwa Sh12-Sh15, na miche mingine huwa ni Sh4, Sh7 au Sh8.

“Lakini mteja akizileta mbegu hutoza Sh1.50, iwe ni za kukuzwa kwa kivungulio au la. Sukumawiki huwa tunachukua Sh1,” aongeza.

“Kama mteja ameleta mbegu za ekari moja ambazo ni miche 12,000, huwa tunamtoza Sh1.50 kwa kila mche, ambapo hupata Sh18,000. Sukumawiki za ekari moja, ambazo ni miche 12,000 humtoza Sh1 ambapo hupata Sh12,000.”

Mbali na kuikuza miche, mkulima huyo pia, hukuza mboga wanazotumia kuwapa wakulima mafunzo shambani na hupeleka kuziuza kule Kisumu au Homabay.“Wale huwa wanakuja tuwafunze huwa tunawatoza ada ya Sh200 kila mmoja, lakini watu wakija kwa wingi kama kundi, huwa tunawatoza pesa kidogo,” asema.

Anaongeza, “Nina vijana ambao huwatuma kuwasaidia wateja wanaonunua miche. Wao huenda kupanda na kusimamia mradi huo. Mteja akiinunua miche ya shamba ekari moja, tunaenda na vijana na wanampandia na mkulima huyo huwalipa vijana hao. Nina vijana saba, na huwalipa wawili kila mwezi.”

Hata hivyo, anasema baadhi yachangamoto anazopitia ni mteja kuagiza miche na anapoipokea hukosa kuilipia.

“Huwa tunapeleka miche kwa kampuni ya kubeba mzigo, halafu tunalipia na tunamtumia mteja risiti aione. Mteja anaweza kukuambia uing’oe miche, halafu baadaye ukimpigia simu hapokei,” asema mkulima huyo, ambaye huyatumia maji ya kisima kuikuza miche yake.

Anadokeza kuwa wateja wake hutoka kote nchini Kenya. Kwa wakati mwingine, mteja akinunua miche kwa wingi, huwa wanamlipia gharama ya kuisafirisha.

Wao hung’oa na kuweka kwa maboksi. “Kwa hivyo, tunaweza kumlipia boksi moja alipie mawili,” aongeza mkulima huyo, aliyeutumia mtaji wa takriban Sh200,000 kuuanzisha mradi huo.

  • Tags

You can share this post!

Anapenda upishi, sasa ana kiwanda cha kupika pilipili

Samaki, mazao kusafirishwa kwa ndege kutoka Uwanja wa Kisumu

T L