• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
KIKOLEZO: Maisha na makeke ya General Defao

KIKOLEZO: Maisha na makeke ya General Defao

Na THOMAS MATIKO

JUMANNE wiki hii, nyota mkongwe wa muziki wa rhumba na lingala Lulendo Matumona almaarufu General Defao, alimaliza mwendo.

Defao alikata pumzi katika hospitali ya Laquintinie mjini Doula, Cameroon alikokuwa amelezwa baada ya kuugua ghafla.

Runinga ya kitaifa ya Congo RTNC iliripoti kuwa mkali huyo wa ‘Papa Sango’ na ‘Sala Noki’ alifariki kutokana na Covid-19 ikiwa ni siku tatu kabla ya kutimiza umri wa miaka 63.

Kabla ya kifo chake, Defao alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya Kisukari.

Defao aliyezaliwa jijini Kinsasha, Congo Disemba 31, 1958, alianza kuimba 1978 akiwa mwanachama wa bendi ya Orchestre Suka Movema. Alifanya kazi na bendi mbalimbali kabla ya kuanzisha yake Big Stars 1990.

Lengo lake lilikuwa ni kuiteka tasnia ya muziki wa rhumba kutoka kwa mikono ya mibabe Koffi Olomide na Bozi Boziana waliokuwa wakiwika sana miaka hiyo. Defao hakutoboa ila aliendelea kufanya muziki kadri ya uwezo wake.

MAISHA YA MSOTO

Ukiweka pembeni muziki wake, Defao aliishi maisha ya ustaa, utata, utashi na uzushi. Kuna vipindi sanaa yake iliyumba kutokana na msoto kutokana na matumizi mabaya ya pesa zake na ukosefu wa menejimenti ya maana.

Hadi anafariki dunia, Defao alikuwa kwenye harakati Za kufufua taaluma yake ya muziki iliyowahi kufana miaka ya 90. Miaka aliyopata kujulikana na kuiweka jina lake kwenye ramani ya muziki wa Batoto Ba Congo.

Huko Cameroon alikofia, alikuwa huko kwa ajili ya shoo. Pia alikuwa kwenye harakati za kuandaa shoo babkubwa ya funga mwaka kwao Congo ili pia kusherehekea bethidei yake.

Lakini kwa kuwa kifo ni siri kubwa, hakujua hatafika kuiona.

General Defao hakuwa mrefu wa kimo, ila alikuwa ni bonge la jamaa. Pandikizi. Jitu ukipenda. Tabasamu lake lingeyeyusha sanamu. Lakini juu ya yote, bonge alikuwa ni mtu mchangamfu sana muda wote.

Ni sifa hizi za upole zilizomsababishia kuishi maisha ya usoto. Mapromota wengi aliofanya kazi nao, walitumia uzuri wake huu wa nafasi kumfilisi na kumlaghai pesa kila waliposhirikiana naye kuandaa shoo.

Siku moja Agosti 2016, Defao alizuiliwa kuondoka kwenye hoteli ya Rickseaside eneo la Nyali, Mombasa baada ya kushindwa kulipa bili zake.

Defao aliwafahamisha wanahabari kipindi hicho kwamba promota Rashid Osundwa alimwitia shoo Mombasa. Shoo hiyo ilikuwa imeratibiwa kufanyika Julai 30, 2016.

Lakini baada ya shoo, Defao alisema promota alimtoka na kumwacha na bili ya hotelini ya Sh20,000 ya siku mbili zaidi alizolala pale.

Kwa kukosa fedha, Defao alizuiliwa kuondoka na uongozi wa hoteli. Aidha Defao alimlia Rashid kumwosha Sh90,000 alizopaswa kulipwa baada ya shoo.

Baada ya kilio chake, msanii na mbunge wa Starehe, Jaguar akatokea na kulipa bili hizo na kumwokoa General Defao kubadilishwa mzoa taka wa hoteli hiyo.

Lakini hili halikuwa tukio la kwanza kama hilo kimkuta. 2000 akiwa kwenye shoo Kampala, Uganda, alioshwa malipo yake na kulazimika kukopa UgSh7 milioni (Sh220,000) ili kulipa bili za hotelini.

ATUPWA JELA

Miaka miwili baada ya tukio hilo la Kampala, Defao alikuwa Kenya kwa ajili ya shoo nyingine.

Alioshwa tena na promota aliyemwacha kwa mataa na bili ya mamilioni ya pesa katika hoteli ya Palacina, Nairobi.

Baadaye alishtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita katika jela ya Industrial Area Prison.

Kwa mara nyingine tena, alipata mhisani aliyetimiza matakwa ya dhamana iiliyotakiwa na mahakama na kumwezesha Defao kuachiliwa huru lakini ikiwa ni baada ya kuhudumu kwa miezi kadhaa.

ATOROKEA KENYA

Defao alitorokea Kenya mwishoni mwa miaka ya tisini kwa kuhofia usalama wa maisha yake.

Kwa miaka 19, Defao aliishi Kenya kama mkimbizi.

Sababu ya kuitoroka Congo ilitokana na utata wa tungo zake zilizomkashifu marehemu dikteta Rais Laurent Kabila na familia yake.

Wakati wasanii wenzake kama Kanda Bongo Man na Franco Luambo Makiadi, wakiamua kutunga nyimbo za kusifia utawala huo dhalimu, Defao aliamua kuchafua hewa.

Kwenye moja ya tungo hizo za kuponda, alidai kuwa Rais Laurent Kabila alishawahi kuwa dereva wake wa miaka mingi walipokuwa wakiishi Tanzania.

Baada ya kuachia hiti Mboka Ya Diogen 1998, iliyomponda Kabila na serikali yake, Defao alipakia mabegi yake pamoja na bendi lake Big Stars kwa ziara ya Zambia.

Kule Zambia akapitiliza masiku na kuanza kuhandwa na maafisa wa uhamiaji baada ya muda wa Visa yake kuisha.

Kwa kuogopa tishio la kurudishwa Congo kwa nguvu, Defao alihepa Zambia na kutua Tanzania.

Akiwa Tanzania alijaribu kuingia Kenya bila stakabadhi za usafiri na kukamatwa Januari 2002 akiwa kwenye harakati hizo.

Lakini hatimaye Defao alifanikiwa kuingia Kenya na kuishi kwa miaka 19 bila ya kukanyaga Congo hadi Agosti 2019 alipofunga safari na kurejea Kinshasa baada ya mwito wa Rais Felix Tshisekedi.

ACHOCHA KUISHI MAISHA LONDON

Licha ya masaibu yote haya, mwendazake aliishi kuchocha umma kuwa anaishi maisha ya kitajiri katika mtaa wa kifahari wa Lavington.

Alikuwa amefuga rasta ndefu ambazo wengine walidai ni za kubandika. Na licha ya umri wake mkubwa, Defao alipiga luku za kibishoo.

Shingoni alining’iniza mikufu mizito tulizozoea kuziona zikivaliwa na rapa 50 Cent enzi za G-Unit.

AJIBLICHI

Na kama kuboresha mwonekano wake hata zaidi, General Defao aliamua kujichibua ngozi na kuwa na mwonekano wa kutisha ukizingatia uso wake tayari ulishajaa makunyanzi kutoka na uzee.

Alipoulizwa ni kwa nini aliamua kutoa tint, na kujipa mwonekano nyang’au, Defao alijitetea kwa kusema alikuwa na ngozi dhaifu iliyohitaji matunzo ya mafuta mahususi Dermovate ili kukaa sawa.

“Sijui ni kwa nini watu wanasaka skendo na maisha yangu badala ya kujishughulisha na muziki wangu,” akasema.

Hata hivyo kwenye shoo yake ya mwisho Kampala 2016, Defao alimfungukia rafiki mmoja na kumweleza kuwa, kujichubua huwa ni ishara ya kujiheshimisha miongoni mwa Wakongo wenye umaarufu kama wake.

Maswahiba wake wa karibu wanasema hawana uhakika ikiwa jamaa alikuwa na mke na watoto sababu hawakuwahi kupata kuwaona au kuwasikia hata siku moja. Acha mzee apumzike.

You can share this post!

2021: Serikali yakosa kutimiza lengo la kuchanja kikamilifu...

Wazazi wanaoficha wana wao wahalifu kuadhibiwa vikali

T L