• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
BORESHA AFYA: Baadhi ya faida za mwarubaini

BORESHA AFYA: Baadhi ya faida za mwarubaini

NA MARGARET MAINA

[email protected]

PODA ya mwarubaini hutumiwa sana kuboresha afya ya ngozi na nywele, na kusaidia kusafisha ini.

Ingawa poda hii ya mitishamba sasa inapatikana katika maduka mengi ya urembo na pia yale yanayouza bidhaa kupitia jukwaa la mtandaoni, unaweza kuitengeneza kwa urahisi ukiwa nyumbani.

Poda ya mwarubaini ni ya kijani kibichi inayotengenezwa kwa kuponda majani yaliyokaushwa na jua ya mwarubaini.

Matunzo ya ngozi

Mwarubaini, pamoja na uwezo wake wa kuzuia uvimbe, unaweza kutumika kutuliza vipele, muwasho, kuungua na maambukizo kwenye ngozi. Kwa kutengeneza maski asili ili kuwa na ngozi inayong’aa, changanya vijiko viwili vikubwa vya unga wa mwarubaini, vijiko viwili vya unga wa msandali na kijiko cha maji ya waridi na utengeneze unga. Unaweza kuongeza maji kidogo zaidi ikiwa ni lazima. Paka kwenye uso wako kwa dakika kumi kisha uoshe na maji baridi.

Utunzaji wa nywele

Poda ya mwarubaini mara nyingi hutumiwa kwenye nywele na kichwani kwa ujumla ili kuondoa mba. Unaweza kuchanganya vijiko vitatu vikubwa vya unga wa mwarubaini na maji ili kutengeneza unga mzito na upake kichwani mwako. Acha kwa nusu saa na safisha vizuri.

Usafishaji wa damu

Uchunguzi umeonyesha kuwa mwarubaini huwa na ladha chungu lakini husaidia kuondoa sumu mwilini. Poda ya mwarubaini inapotumika kwa dozi ndogo inaweza kusaidia kusafisha ini na kuboresha afya kwa ujumla. Pia hufanya kama nyongeza ya kinga ya asili kwa kuondoa sumu kutoka kwa njia ya utumbo.

Inashauriwa kushauriana na mhudumu wako wa afya kabla ya kutumia bidhaa hii ikiwa wewe ni mjamzito au unanyonyesha, unatumia dawa, au una hali ya kiafya inayohitaji uangalizi wa mhudumu wa afya.

Epuka kuwapa watoto wachanga kwani bidhaa za mwarubaini zinaweza kusababisha athari mbaya hasa kwa wenye tatizo la pumu.

  • Tags

You can share this post!

Chelsea wasema hawana haja na Ronaldo tena

MAPISHI KIKWETU: Pancakes za ndizi

T L